Breaking News

Your Ad Spot

Jan 25, 2015

FLAVIAN MATATA KUNADI VIVUTIO VYA UTALII KIMATAIFA

Na mwandishi wetu
MWANAMITINDO maarufu nchini anayetamba Marekani, Flaviana Matata, atashiriki kwenye tangazo la kunadi vivutio vya utalii.

Tayari wataalamu wa kampuni ya Pursuit Productions ya nchini Marekani, wameanza kazi ya kuandaa tangazo hilo visiwani jana.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema jana kuwa, hatua hiyo ni mkakati wa kukuza na kuendeleza utalii wa Tanzania ndani na nje ya nchi.

Alisema wizara yake itaendelea kutekeleza mikakati hiyo kwa lengo la kuvutia watalii hasa wa nje na kwamba, ana uhakika hilo litafanikiwa.

Miongoni mwa mikakati inayotekelezwa kwa sasa wizara hiyo ni pamoja na kutangaza vivutio vya utalii nchini kupitia viwanja vikubwa vya michezo Barani Ulaya na Marekani.

Alisema kampuni ya ambayo pia inafanya kazi na wasanii wakubwa wa Hollywood, wanaendelea na kazi ya utayarishaji wa tangazo hilo kisha watakwenda Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Nyalandu alisema tangazo hilo litainadi Tanzania na vivutio vyake katika televisheni kubwa za kimataifa na pamoja na zile za hapa nchini.

“Wataalamu wa Hollywood wapo Zanzibar na wameanza kazi hiyo leo (jana), litakuwa tangazo zuri na litakalotangaza vivutio vyetu vyote vya utalii kimataifa.

“Tangazo hili ni mkakati wa kuendelea kunadi vivutio vyetu na kuvutia wageni wengi zaidi, litakuwa fupi na lenye kuvutia zaidi,” alisema Nyalandu.

Alisema matayarisho ya tangazo hilo yatachukua wiki tatu hadi kukamilika kwake na kwa kuanzia litarushwa kwenye luninga za CCN ya Marekani na BBC World mwezi Machi, mwaka huu.

Aliongeza kuwa mpango huo ni utekelezaji wa mkakati wake wa kuhuisha mtazamo wa dunia kuhusu Tanzania alioutangaza bungeni mwezi Juni, mwaka jana.

Alisema Flaviana, ambaye anafanya shughuli zake nchini Marekani na kuiletea sifa kubwa Tanzania, ushiriki wake katika tangazo hilo utaongeza hamasa kubwa.

“Tangazo la watanzania kwa ajili ya kuvutia watalii katika kona zote za dunia, Flaviana ni Mtanzania hivyo maslahi ya watanzania yamezingatiwa,” alisema Nyalandu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages