Breaking News

Your Ad Spot

Feb 17, 2015

MAMA KIKWETE AWATAKA WAKAZI WA MKOA WA LINDI KUIPIGIA KURA YA NDIYO KATIBA PENDEKEZWA

indexNa Anna Nkinda – aliyekuwa Lindi
 Wananchi wa mkoa wa Lindi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuipigia kura ya ndiyo katiba inayopendekezwa kwani ni bora na imegusa maeneo yote kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.
Rai hiyo imetolewa na  Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wananchi waliohudhuria sherehe ya kushangilia ushindi wa uchaguzi wa Serikali za mitaa katika mtaa wa Ruaha kata ya Mingoyo wilayani humo.
Katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana wananchi wa mtaa wa Ruaha waliwachagua Mwenyekiti na wajumbe wote watano kutoka Chama Cha Mapinduzi.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema katiba inayopendekezwa imeangalia maeneo yote yanayomgusa binadamu ikiwa ni pamoja na haki za wanawake na watoto, watu wenye mahitaji maalum wakiwemo walemavu na wazee.
“Katiba iliyopo sasa ilitungwa na baadhi ya watu waliokuwa madarakani kwa wakati ule na haikuwahusisha wananchi, lakini hii inayopendekezwa  wananchi wameshiriki kuitunga kwa kutoa maoni yao”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mwantumu Mahiza aliwahimiza wananchi hao kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili wasipoteze haki yao ya msingi ya  kupiga kura.
Mahiza alisema kama kuna watu waliojiandikisha katika miaka ya nyuma wabebe vitambulisho vyao  ili viweze kunukuliwa na kwa wale wenye umri wa kuanzia miaka 18 wakajiandikishe na walio na umri wa chini ya hapo wasijiandikishe.
Aliwaasa wananchi hao  kutokubali  wageni waliokaa katika maeneo yao  kwa kipindi cha chini ya miezi sita kujiandikisha.
Akisoma taarifa ya CCM tawi la Ruaha Mohamedi Ngashona ambaye ni mjumbe alisema viongozi hao wamejipanga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa mtaa huo ambazo ni uharakishaji wa ujenzi wa zahanati, ukarabati wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa nyumba za walimu.
Kuwatambua kaya maskini na wazee kwa kuwapatia huduma muhimu, uimarishaji wa barabara ya kutoka Mnazimmoja hadi Ruaha na utekelezaji wa sera ya umeme vijijini hasa vilivyopitiwa na mradi wa bomba la gesi.
Katika mkutano huo jumla ya wanachama 43  walijiunga na chama hiyo kati yao wanne walitoka Chama cha Wananchi CUF .

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages