Na Mwandishi Maalum, New York
Ushiriki wa askari wanawake katika Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa, ni baadhi ya mafanikio ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajivunia miaka 20 baada ya Mkutano wa Kihistoria wa wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba ( Mb) ameyasema hayo leo ( alhamis) wakati alipokuwa akitoa tathmini na changamoto za utekelezaji wa maazimio muhimu yaliyofikiwa katika mkutano huo wa wanawake Beijing.
Mhe. Waziri Simba, anaongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Hadhi ya Wanawake ( CSW) unaoendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, katika Ujumbe huo wa Tanzania unajumuisha na washiriki kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar akiwamo Mhe. Zainab Omar Mohammed, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, vijana, wanawake na watoto, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“ Katika miaka miaka 20 iliyopita, yapo mambo mengi ambayo Tanzania tumepiga hatua za kuridhisha, katika maeneo ya uwezeshwaji na fursa sawa kwa wanawake. Katiba za pande zote mbili za Muungano zinaainisha vema kuhusu hadhi ya mwanamke. Na Katika katiba mpya inayopendekezwa hivi sasa kuna eneo ambalo linazungumzia kwa kina Usawa wa Jinsia na Uwezeshwaji wa wanawake.” anasema Waziri Simba
Vile vile ameeleza baadhi ya sheria ambazo ama zimefanyiwa marejeo au kutungwa kwa lengo la kuboresha usawa wa kijinsia. Amezitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni sheria zinazohusu watoto, sheria zinazohusu usafirishaji wa binadamu, sheria ya ardhi, HIV/AIDS na sheria ya makosa ya kujamiana.
Kuanzishwa kwa dawati la jinsia na watoto katika vituo vya Polisi, vituo vya kuhifadhi watoto, vituo kwaajili ya wanawake wanaofanyiwa ukatili na mtandao wa viongozi wa madhehebu ya dini kuhusu ukatili dhidi ya wanawake. Ni baadhi ya mafanikio ambayo yameelezewa na Mhe. Waziri
Ameeleza zaidi kwa kusema, Wanawake wengi sasa wanashiriki katika siasa ambapo kwa mfano asilimia 36 ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ni wanawake na kwa upande wa Zanzibar asilimia 33 ya Wawakilishi ni wanawake. Na kwamba kumekuwapo pia ongezeko la idadi ya wanawake Majaji na Mahakimu na wanaoshika nafasi za uongozi.
Mhe. Simba amewaeleza wajumbe wanaoshiriki mkutano huo kwamba katika kuhakikisha panakuwa na fursa sawa katika ajira utumishi wa Umma, kuna kifungu katika sheria za utumishi wa umma vinavyoainisha kwamba pale mwanamke na mwanaume wanapokuwa na sifa zinazolingana, basi mwanamke atafikiriwa kwanza.
Kwa upande wa elimu, pamoja na kuwa na uwiano sawa kati ya wavulana na wasichana katika shule za msingi. Anasema elimu ya msingi inatolewa bure katika shule za serikali na kwamba utaratibu huo pia utafanyika katika shule za sekondari za umma. Aidha ameelezea ongezeko la wanafunzi wa kike wanaochukua masomo ya sayansi.
Kwa upande wa Afya, Mhe. Waziri amesema Tanzania imepiga hatua za kuridhidha katika upunguzaji wa vifo vya wanawake wajawazitio na vya watoto wachanga.
Hata hivyo pamoja na mafanikio hayo na mengine mengi ambayo Tanzania inajivunia kuhusu hadhi ya wanawake na watoto wa kike, anasema kama ilivyo kwa mataifa mengi yanayoendelea, Tanzania pia bado inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo za uhaba wa fedha kwa miradi inayohusu masuala ya jinsia, ndoa na mimba za utotoni, umaskini wa kaya na ukatili dhidi ya wanawake.
Mhe. Waziri Simba, Tanzania imejifunza kutokana na changamoto hizo na nyinginezo na kwamba imejipanga vema kutekeleza baadhi ya changamoto hizo hususani upunguzaji wa umaskini, kupitia malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya 2015.
Mhe. Asha-Rose Migiro ( Mb) wakati huo akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa na baadhi ya askari wanawake kutoka JWTZ wanaoshiriki katika operesheni ya kulinda amani kupitia Umoja wa Mataifa huko Lebanon. Katika mchango wake, Mhe. Simba pamoja na mafanikio mengine ambayo Tanzania imeyapata katika miaka 20 tangu mkutano wa Beijing ni pamoja na askari wanawake kupata fursa za kushiriki katika operesheni za kulinza amani zinazoratibiwa na Umoja wa Mataifa.> Picha ya Maktaba
Your Ad Spot
Mar 14, 2015
Home
Unlabelled
TANZANIA: NI MAFANIKIO KUWA NA ASKARI WANAWAKE WANAOSHIRIKI ULINZI WA AMANI
TANZANIA: NI MAFANIKIO KUWA NA ASKARI WANAWAKE WANAOSHIRIKI ULINZI WA AMANI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269