Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu akiwasilisha
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango
ya Bunge Zima kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere
jijini Dar es salaam.
Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu akiwasilisha
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango
ya Bunge Zima kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.
Baadhi
ya Wabunge wakifuatilia kwa makini hotuba ya uwasilishaji wa Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge
Zima.
Katibu
Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Kulia)
akimpongeza Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe.
Dkt. Mary Nagu (Kushoto) mara baada ya kuwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima.
Naibu Katibu Mtendaji (Sekta za Uzalishaji) kutoka Ofisi
ya Rais, Tume ya Mipango, Bw. Maduka Kessy (Kulia) akimpongeza Waziri
wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu
(Kushoto) mara baada ya kuwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima.
Naibu
Katibu Mtendaji (Huduma za Jamii na Idadi ya Watu), Bibi Florence
Mwanri (Kushoto) akiongea na Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilila
(Kulia) mara baada ya uwasilishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima. Anayewasikiliza ni
Naibu Katibu Mtendaji (Sekta za Uzalishaji) kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bw. Maduka Kessy.
Katibu
Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango
(Kushoto) akiongea na viongozi waandamizi wa Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango mara baada ya uwasilishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima.
viongozi waandamizi wa Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango wakifuatilia uwasilishaji wa Mpango wa Maendeleo
wa Taifa wa Mwaka 2015/16 uliokuwa ukifanywa na Waziri wa nchi (Ofisi ya
Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu katika Kamati ya Mpango
ya Bunge Zima.
……………………………………………………………………….
Na Saidi Mkabakuli
Serikali imesema kuwa ipo katika
hatua za mwisho za kukamilisha miradi ya kitaifa ya kimkakati
iliyoibuliwa katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo unaofikia kikomo mwaka
ujao wa fedha wa serikali.
Hayo yalisemwa na Waziri wa nchi
(Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu wakati
akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 katika Kamati
ya Mpango ya Bunge Zima kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa
Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Dkt. Nagu alisema kuwa mpaka
kufikia mwezi machi mwaka huu, serikali imefanikiwa kutandika reli za
uzito wa ratili 56.12 kwa yadi kwa umbali wa km 9 kati ya stesheni za
Lumbe, Mto Ugalla na Katumba; kukamilisha malipo ya ununuzi wa mabehewa
274 ya mizigo ambapo mabehewa yameshaanza kupokelewa Novemba 2014;
kukamilika kwa matengenezo ya njia ya reli iliyoharibiwa na mafuriko
katika maeneo ya Ruvu – njia panda ya Mruazi.
Waziri Nagu aliongeza kuwa kwa
upande wa Barabara hatua iliyofikiwa ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi
wa kilometa 502.6 za barabara kuu kwa kiwango cha lami dhidi ya lengo la
kilomita 560, na ukarabati wa kilomita 78.8 za barabara kuu kwa kiwango
cha lami dhidi ya lengo la kukarabati kilomita 131.5. Kwa upande wa
madaraja hatua iliyofikiwa ni: kuendelea na ujenzi wa madaraja ambapo
daraja la Kigamboni limefikia asilimia 75, Sibiti asilimia 22, Kilombero
asilimia 26, Mbutu asilimia 99, Lukuledi II asilimia 25 na Kavuu
asilimia 36.
Katika sekta ya Uchukuzi, Dkt.
Nagu aliyataja mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa
shehena iliyohudumiwa katika bandari ya Dar es Salaam kufikia tani
milioni 14.3 Machi 2015 dhidi ya lengo la tani milioni 13.0 kwa mwaka
2014/15; kuongezeka kwa ufanisi wa bandari katika kupakua magari kwa
kila shifti moja ya saa 8 kufikia magari 886 kwa shifti kufikia Machi
2015 ikilinganishwa na lengo la magari 600 kwa shifti katika mwaka
2014/15; kupungua kwa muda wa meli kupakia na kupakua mizigo bandarini
kutoka lengo la wastani wa siku 5 mwaka 2013/14 hadi wastani wa siku 3.7
kufikia Machi 2015; kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa malipo kwa njia
ya mtandao mwezi Julai, 2014; na kuanza kutoa huduma katika bandari ya
Dar es Salaam kwa masaa 24 kwa siku zote za juma. Aidha, kwa upande wa
bandari ya Bagamoyo, hatua iliyofikiwa ni kusainiwa kwa makubaliano ya
ujenzi wa bandari; na kutangazwa kwa zabuni kwa ajili ya kupata
wawekezaji katika bandari za Mtwara na Mwambani -Tanga.
“Katika sekta ya nishati, hatua
iliyofikiwa ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi kutoka
Mtwara hadi Dar es Salaam (km 542) Machi 2015, na ujenzi wa mitambo ya
kusafisha gesi Madimba (Mtwara) na Songosongo (Lindi) umefikia asilimia
86.9 ambapo unatarajiwa kukamilika Juni 2015. Kwa upande wa usambazaji
wa umeme vijijini, wateja wapya 2,602 wameunganishiwa umeme katika mikoa
ya Simiyu, Singida, Kagera, Tanga, Ruvuma, na Iringa,” alisema Dkt.
Nagu.
Kwa mujibu wa Waziri Nagu,
shughuli nyingine zilizotekelezwa nia katika sekta ya nishati, ni pamoja
na kukamilika kwa usimikaji wa mitambo 4 ya kufua umeme yenye uwezo wa
jumla ya MW 150, kuendelea na ujenzi wa vituo vya kupoza na njia za
kusafirisha umeme, na kuendelea na ujenzi wa karakana, majengo ya
utawala, na barabara za ndani katika mradi wa Kinyerezi I; kukamilisha
ulipaji fidia kwa eneo la Makambako katika mradi wa usafirishaji umeme
wa Makambako – Songea; na kuanza ujenzi wa nguzo za njia ya umeme
katika mradi wa msongo wa kV 400 wa Iringa – Shinyanga.
Akiwasilisha kazi zilizotekelezwa
katika sekta ya Maji, Dkt. Nagu alisema kuwa ulazaji wa mabomba katika
mradi wa maji Ruvu Chini kutoka Bagamoyo hadi Dar es Salaam kazi ambayo
imekamilika kwa kilomita 52.43 kati ya kilomita 55.93 za mradi sawa na
asilimia 93.8; kwa upande wa mradi wa maji Ruvu Juu: mkandarasi
amekamilisha utafiti wa udongo na uchunguzi wa awali wa mahali
yatakapojengwa matanki Kibamba na Kimara; na kwa upande wa mradi wa
Bwawa la Kidunda, wananchi wamelipwa fidia ya shilingi bilioni 7
kupisha ujenzi wa barabara na eneo litakapojengwa bwawa.
“Kwa upande wa miradi ya maji
vijijini, jumla ya miradi 123 ya maji ilijengwa na kukamilika. Idadi hii
imenufaisha wananchi wapatao 463,750 na kuongezeka kwa ufanisi katika
masuala ya ununuzi wa huduma katika mikataba kutoka siku 265 hadi siku
90. Aidha, Serikali imeendelea na ujenzi wa mabwawa ambapo bwawa la
Iguluba (Iringa) na Wegero (Mara) yamekamilika. Vile vile, ujenzi wa
bwawa la Kawa (Rukwa) umefikia asilimia 95, bwawa la Sasajila (Dodoma)
asilimia 66.09 na Mwanjoro (Shinyanga) asilimia 45.4,” aliongeza Waziri
Nagu.
Katika sekta ya kilimo, Dkt. Nagu
aliyataja mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kupatikana kwa hati za
mashamba mawili ya Bagamoyo na Mkulazi; maghala 30 yamekarabatiwa na
kupatiwa watoa huduma binafsi katika Wilaya za Mbozi na Momba. Vile
vile, skimu 30 za umwagiliaji zimepatiwa watoa huduma binafsi katika
Wilaya za Mbarali, Kyela na Iringa; na mafunzo juu ya kubaini na
kudhibiti visumbufu, matumizi bora ya maji, utunzaji na matengenezo ya
miundombinu ya umwagiliaji na kutumia mwongozo wa uendeshaji skimu za
umwagiliaji yametolewa. Aidha, ujenzi wa maghala 2 katika Wilaya ya
Mlele umekamilika.
Vile vile katika sekta ya viwanda,
Waziri Nagu alizitaja kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kukamilika kwa
ukarabati wa barabara ya Itoni – Mkiu – Liganga na Mchuchuma kwa kiwango
cha changarawe ili kuwezesha mitambo kufika maeneo ya Mchuchuma na
Liganga; na kuanza uthamini wa mali za wananchi watakaohama eneo la
Mchuchuma. Vile vile, fidia shilingi bilioni 53 imelipwa katika eneo la
kujenga kituo cha Biashara na Huduma Kurasini; na fidia ya shilingi
bilioni 7 imelipwa katika eneo la uwekezaji Bagamoyo na Serikali
imesaini mkataba na kampuni ya China Mechants Holding International
kwa ajili ya kujenga bandari na eneo la viwanda. Aidha, katika kiwanda
cha kuzalisha dawa ya kuua viluwiluwi wa mbu, Kibaha, kazi ya ufungaji
wa mitambo na ujenzi wa miundombinu inaendelea na inatarajiwa kukamilika
kabla ya Julai, 2015.
Akizungumzia upande wa maendeleo
ya rasilimali watu, Dkt. Nagu alisema kuwa kazi zilizofanyika ni pamoja
na kuendelea kugharamia wanafunzi 159 wanaoendelea na mafunzo katika
fani za mafuta na gesi kwa ngazi mbalimbali za mafunzo ndani na nje ya
nchi ambapo wanafunzi 124 wanagharamiwa na Serikali na wanafunzi 35
wanagharamiwa na nchi wahisani; na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa
miundombinu katika vyuo vikuu na vyuo vya ualimu, ufundi na ustawi wa
jamii.
Kwa upande wa utafutaji wa
rasilimali fedha, Waziri Nagu alisema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania
inatumia kanzidata bora inayohifadhi taarifa inayoweza kuthaminisha
bidhaa na hivyo kutoa makadirio bora zaidi ya viwango vya kodi.
Vilevile, alisema kuwa tozo kwa ajili ya uwekezaji katika elimu umeanza
Julai 2013 ikiwa asilimia 2.5 ya mapato ghafi ya kampuni za simu.
“Katika sekta ya fedha, kazi
zilizotekelezwa ni pamoja na kuongezea Benki ya Maendeleo ya Kilimo
mtaji wa shilingi bilioni 60; kuendelea kuongeza mtaji wa Benki ya
Rasilimali kufikia shilingi bilioni 212 ambapo mtaji kutoka Serikalini
ni shilingi bilioni 152.2 na shilingi bilioni 59.8 zimetokana na
malimbikizo ya faida; na mali za Benki ya Maendeleo ya Wanawake
Tanzania ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 26.5 mwaka 2013 hadi
shilingi bilioni 34.8 mwaka 2014,” alisema Dk. Nagu.
Kuhusu eneo la huduma za utalii,
Dkt. Nagu aliongeza kuwa kazi zilizofanyika ni pamoja na usanifu wa
ujenzi wa Utalii House awamu ya pili na kuboreshwa kwa mfumo wa
ukusanyaji mapato (utalii, uwindaji na upigaji picha). Aidha, idadi ya
watalii kutoka nje iliongezeka kutoka watalii 1,090,905 mwaka 2013 hadi
watalii 1,102,026 mwaka 2014. Vile vile mapato yatokanayo na utalii
yaliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.81 mwaka 2013 hadi dola
za Marekani bilioni 1.98 mwaka 2014.
“Kwa upande wa Biashara, hatua
iliyofikiwa ni kurekebisha sheria ya mfumo wa stakabadhi ghalani na
kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu mfumo huo; kuanzishwa kwa
kampuni ijulikanayo kama Tanzania Mechantile Exchange plc kusimamia
na kuendesha soko la mazao ya bidhaa na kuhamasisha matumizi ya fursa
za masoko ya mipakani, Kikanda na Kimataifa,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Dkt. Nagu maandalizi
ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2015/16 yamezingatia maeneo
ya kipaumbele yaliyoainishwa katika malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 –
2015/16). Aidha, Mpango huu umezingatia Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umaskini – MKUKUTA II (2010/11 – 2014/15), Malengo ya Milenia,
Mwongozo wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2014/15; Mapendekezo ya Mpango
wa Taifa wa Maendeleo 2014/15 yaliyojadiliwa na Bunge Novemba, 2014;
Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2010 – 2015); na sera na
mikakati ya kisekta.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269