Breaking News

Your Ad Spot

May 31, 2015

UMOJA WA MATAIFA WAWAENZI WALINDA AMANI WAKE

Na MwandishiMaalum, New York
Mashujaa Private Ally Salum Jumanne, Private Mohamed John Mbizi, Private Vasco Adrian Msigala na Sajent Hamis Juma Nyange kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ) ni miongoni mwa mashujaa 126 ambao Ijumaa ya Mei 29, 2015, Umoja wa Mataifa uliwatunuku medali ya Dag Hammarskjold.

 Umoja wa Mataifa umeitenga Mei 29, kuwa siku maalum ya kutambua na kuenzi mchango wa walinda Amani ambao wamepoteza maisha wakati wakitekeleza majukumu ya ulinzi wa amani kupitia operesheni za Umoja wa Mataifa.

Katika adhimisho hilo na ambalo lilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki moon, Naibu wake Jan Eliasson, na Wakuu wa Idara za Ulinzi za Umoja wa Mataifa,  jumla ya mashujaa 126 kutokanchi 38 waliopoteza maisha mwaka jana(2014) walienziwa kwa kutunukiwa medali maalum ya DagHammarskjold.

 Adhimisho hilo lilitanguliwa na uwekaji wa shada la maua kwa heshima ya mashujaa hao,  shada liliwekwa na Katibu Mkuu Ban Ki Moon  katika sehemu maalum ambayo imeandaliwa kwa ajili ya kumbukumbu hiyo.

 Akizungumza kwa masikitiko makubwa wakati wa hafla hiyo,  Katibu Mkuu, Ban  Ki Moon,  amesema, katika maadhimisho yote ya nayofanyika katika Umoja wa Mataifa,   hakuna adhimisho lenye kutia simanzi na ngumu kama hili la kuwakumbuka na kuwaenzi walinda amani ambao wamepoteza maisha yao wakati wakitoa ulinzi kwa watu wengine.

 “ Ninasikitika kusema kwamba,   hii ni mara ya saba mfululizo ambapo zaidi ya walinda amani 100 wamepote za maisha katika kipindi cha mwaka mmoja. Hatari wanayokumbana nayo walinda amani wetu inazidi kuongezeka kwa kasi kubwa,  kutokana na kushambuliwa na makundi ya wahafidhina na makundi ya wanamgambo wenye silaha mpaka hatari ya magonjwa ambukizi kama Ebola” amesema Katibu Mkuu.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akaendelea kusema. “ Tumekusanyika hapa kuwaenzi mashujaa wetu waume kwa wake ambao wamepoteza maisha yao wakati wakiwalinda wananchi katika maeneo hatari duniani. 

Kujitoa kwao muhanga na namna walivyo yaishi maisha yao,  wanatufanya sisi tujisikie fahari na kututia shime ya kufanyakazi kwabidii zaidi ili kudhihirisha kwamba maisha yao hayakupotea bure.

 Ban Ki Moon, awaeleza wawakilishi kutoka nchi ambazo zimepoteza mashuja wake kwamba,  operesheni za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa zitaendelea kuwa zenye changamoto na hatari kubwa, na cha kusikitisha ni kwamba adhimisho lililofanyika ijumaa la kuwaenzi mashujaa hao halitakuwa la mwisho.
 
“ Walinda amani wetu wanabeba jukumu zito kwa ajili yetu sote. Natoa heshima zangu kwa mashujaa na salamu zangu za pole kwa familia za mashujaa hawa” akasisitiza KatibuMkuu.

Walinda amani hao 126 na raia 19 wamepoteza maisha wakati wakihudumu  katika misheni zilizopo, Afghanistan,  Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ivory Coast, Cyprus,  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Haiti, Mali, Masharikiya Kati, Liberia, Sudan na Sudan yaKusini.

 Pamoja na Tanzania  nchi nyingine ambazo zimepoteza mashujaa wake katika misheni mbalimbali za kulinda amani katika mwaka uliopita ni Senegal, Afrika yaKusini,  Hispania, Togo,  Rwanda, Benin,  Burkina Faso, Bangladesh, na  Burundi.

 Nyingine ni, Cambodia, Chad, El Salvador, Ethiopia, Fiji, Ufaransa, Ghana,  India, Indonesia, Kenya, Malawi, Niger,  Pakistan, Philippines, Tunisia na Zimbabwe.

Pamoja na mashujaa hao ambao ni wanajeshi, wapo pia raia 19 wakiwamo pia polisi, madaktari, watumishi na watoa misaada ya kibinadamu ambao wamepoteza maisha wakati wakitoa misaada kwa binadamu wenzao.

 Wakati Umoja wa Mataifa ukiwaenzi mashujaa hao waliopoteza maisha mwaka jana. Tayari mwaka huuwa 2015 mashujaa wapatao 49 wamekwishapoteza maisha wakitekeleza majukumu yao ya kuleta Amani ,utulivu na ulinzi wa raia wasio na hatia katika nchi zenye migogoro.
Kati yamashujaa 49 hao wapo Watanzania wawili.

 Jumla ya walinzi wa amani 3,300 wamekwisha kupoteza maisha tangu kuanzishwa kwa Operesheni za Ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa Mataifa mwaka 1948.

HABARI KATIKA PICHA
 Mpiga  Buluji akiimba wimbo maalum wa  maombolezo kama ishara ya kuwakumbuka mashujaa 126 walinda amani waliopoteza maisha  mwaka jana. shughuli za utoaji wa medali  maalum  zilitanguliwa na uwekaji wa  shada maalum la maua katika eneo ambalo limetengwa katika viunga vya Umoja wa Mataifa.  Pichani anaonekana Katibu Mkuu Ban Ki Moon akitoa salamu za heshima kwa wahanga hao anaonekana pia Naibu Katibu Mkuu  Jan Eliasson
 Katibu Mkuu Ban Ki Moon, akiwa na Naibu Katibu Mkuu, Jan  Eliasson, na  Viongozi wakuu wa Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani ( DPKO) muda mfupi kabla ya utoaji wa medali maalum kwa mashujaa 126 walinda amani ambao walipoteza maisha mwaka jana. katika  salamu zake Katibu Mkuu alieleza kwamba katika  maadhimisho yote yanayofanyika katika Umoja wa Mataifa, adhimisho la kuwakumbuka na kuwaenzi walinda amani ni adhimisho lenye  kutia simanzi na gumu.

 Charge d' affaires a.i  Maura Mwingira wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akiandika katika kitabu maalum,  baada ya kupokea  kwa niaba ya  familia  za mashujaa wanne wa JWTZ waliopoteza maisha wakati wakihudumu katika misheni za kulinda amani mwaka jana.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages