Mgeni rasmi wa katika Kongamano
hilo Mhe. Getrude Mongella akiwa na baadhi ya wabunge wanawake wa bunge
la jamhuri ya muungano wa Tanzania wakiimba nyimbo mbalimbali.
Kikundi cha ngoma za kiasili kutoka mkoani Dodoma tayari kwa kutumbuiza katika kongamano hilo.
…………………………………………..
Na Mwandishi wetu
Kwa Mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Idadi ya
Watanzania sasa imefikia milioni 44.9 huku wanawake wakiwa ni asilimia
51.3 ilihali wanaume ni asilimia 48.7. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya Mwaka 1977 inabainisha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ni ya kidemokrasia, ya kidunia ambayo inaendeshwa kwa misingi ya
kidemokrasia na haki ya kijamii. Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inatamka wazi kwamba nchi hii ni nchi ya
kidemokrasia na haki za kijamii.
Akidi nzima ya Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ni Wabunge 357 kwa mujibu wa Katiba. Hata hivyo
viti maalum pekee ni 102 (28.6%) vilivyogawanywa miongoni mwa vyama vya
siasa kwa kuzingatia matokeo yao ya uchaguzi, kati ya viti 239 vya
majimbo (vikiwemo kutoka Zanzibar), ni wanawake 21 tu (8.8%) ndio
walipata viti vya kuchaguliwa bungeni. Idadi ya madiwani wa kuchaguliwa
asilimia 4, Wenyeviti wa Vijiji Asilimia 2, Wenyeviti wa Mitaa ni
asilimia 12 wakati Wenyeviti wa Vitongoji ni asilimia 3tu!!.
Pengo hili la ushiriki wa Wanawake
katika nafasi za uongozi zimepelekea asasi za kiraia kuendeleza
harakati za kudai ushirikishwaji sawa au usawa katika vyombo vya
uawakilishi kati ya Wanawake na wanaume. Kama sehemu ya kuendeleza
mapamabno ya kudai ushiriki wa Wanawake kwenye uongozi, ActionAid
Tanzania kwa kushirikiana na TGNP Mtandao waliandaa Kongamano la
Wanawake wagombea kwa nafasi zote za uongozi katika uchaguzi mkuu wa
mwaka huu 2015 kuanzia tarehe 14 hadi 15 Juni 2015 lililofanyika mjini
Dodoma, ambapo wagombea Wanawake, vijana na watu wanaoishi na ulemavu
zaidi ya 200 walikutana na kujadiliana kwa pamoja changamoto
wanazokumbana nazo katika harakati za kutafuta ushindi. Waliokutana ni
Wanawake , vijana na walemavu walioonesha nia ya kuomba ridhaa ya vyama
vyao ili wawe viongozi.
Katika kongamano hilo la aina yake
viongozi/wabunge na viongozi wastaafu Wanawake ambao wamekuwa
madarakani kwa muda mrefu na kupambana na changamoto mbalimbali ambazo
zinawakabili Wanawake katika nafasi za uongozi waliweza kushiriki na
kutoa ushauri kwa waonesha nia hao.
Akizungumza katika Kongamano hilo,
Meneja wa Haki za Wanawake kutoka ActionAid Scholasitica Haule alisema
jinsi mchakato ulivyo na kasi kubwa ni lazima makundi yote yawe makini
na vyama vya siasa navyo viangalie nyuma ili kuhakikisha kila
anayestahili kuwa kwenye kasi ya mchakato anapata nafasi.
“tunajua mchakato wa uchaguzi mkuu
unakwenda kwa kasi sasa, tunavitaka Vyama vya siasa vioneshe kwa
vitendo nia ya kujenga demokrasia ya ushindani kwanza kwa kuonesha
mabadiliko ndani ya uongozi wa vyama. Vyama vya siasa sharti viwe mstari
wa mbele kwenye kuonesha kwa vitendo dhana wanazosimamia, kama vile
demokrasia, utawala bora na wa sheria. Kwa mantiki hii, sharti mifumo
iliyoko ndani ya vyama pamoja na taratibu zake zijengeke kwenye misingi
shirikishi, ya kidemokrasia isiyowabagua wanawake au makundi mengine
yaliyoko pembezoni” alisema Haule
Naye Mkuu wa wilaya ya Chamwino
Farida Mgomi, aliyekuwa mgeni wa heshima katika ufunguzi wa Kongamano
hilo, aliwataka Wanawake walionesha nia ya kugombea uongozi kutokukata
tamaa wala kuogopa.
“msiogope, masikate tamaa, simameni imara ili kuhakikisha
mnashinda, wanawake walipata fursa wamefanya vizuri na sote tumneona, na
hata wao ukiwauliza wanakuambia kwamba wamekumbana na changamoto nyingi
lakini wamefanikiwa, jambo la msingi ni kuwa na msimamo, kutaa kwa
dhati rushwa, matumizi makubwa ya fedha kwenye uchaguzi ili mnakundi
yote hasa wanawake, vijana na wanaoishi na ulemavu waweze kushiriki na
kufanikiwa” alisema DC Mgomi.
Alieleza kwamba Ili kuwapa fursa
wanawake, vijana na watu wanaoishi na ulemavu washinde katika uchaguzi
huu ni lazima Jamii nzima iunganishe nguvu katika kudai vyama vya siasa
vizingatie usawa wa kijinsia katika kupendekeza majina ya wagombea,
kuwawezesha kifedha na kuwaunga mkono ili washinde.
Pia Mkuu huyo wa wilaya alivitaka
Vyama vya siasa vitoe fursa za pekee kwa wagombea wanawake katika
kutumia vyombo vya habari vyote kutangaza habari za uchaguzi kwa
kuzingatia usawa wa kijinsia bila kujali itikadi na kuweka taratibu za
kuwezesha watu wenye ulemavu washiriki kikamilifu katika uchaguzi kama
wapiga kura na kama wagombea uongozi katika nyadhifa mbalimbali.
Balozi Mstaafu na aliyekuwa Rais
wa Bunge la Afrika Dk. Getrude Mongela ambaye aliwafunda Wanawake hao
namna ya kuwa viongozi bora na mbinu za kushinda uchaguzi alisema
kwamba, Wanawake wanatakia kujenga hoja na kubeba ajenda za msingi za
wananchi wote bila kuwabagua na sio kushambulia wanasiasa wengine
majukaani.
Aidha Mongela aliwataka Wanawake
kuhakikisha kwamba wao wenyewe wanaunganisha nguvu bila kujali itikadi
zao za kichama, kuvua tofauti zao wanapokutana ili kuwa na ajenda moya
ya kuhakikisha Wanawake wenye uwezo wanashinda na wanabeba ajenda ya
wananchi wote.
“Tukishaanza mipango ya kujigawa
kwa itikadi zetu, hatuwezi kushinda, ninawataka kuunganisha nguvu pamoja
na kuhamkikisha hakuna anayeachwa nyuma, lakini tusijenge chuki za
kivyama, achana na chama, sema ni mwanamke kwanza, halafu mengine ya
vyama yatakuja baadaye, hapo tutaona mabadiliko” alisema Dk. Mongela
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269