Breaking News

Your Ad Spot

Jun 23, 2015

MKUU WA WILAYA WA ZAMANI MARGARET KIPAYA AFARIKI DUNIA

MKUU wa Wilaya (DC) mstaafu, Margaret Kipaya (75) amefariki dunia kutokana na matatizo ya kisukari baada ya kuugua kwa miezi kadhaa.

Taarifa ya familia ya DC huyo ilisema Margaret alifariki dunia alfajiri ya kuamkia jana katika Hospitali ya Emilio Mzena jijini Dar es Salaam na anatarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwake Makongo Juu.


“Marehemu atazikwa keshokutwa (kesho) kwenye makaburi ya Makongo baada ya makubaliano ya familia kufikiwa,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.


Miaka ya mwisho ya utumishi wake, Margaret ambaye anatokea Kahama mkoani Shinyanga, alifanya kazi kama Mkuu wa wilaya za Nzega na Igunga mkoani Tabora kwa nyakati tofauti na Songea mkoani Ruvuma hadi alipostaafu.
Alianzi utumishi wakekwa kufanya kazi kwa mtindo wa kujitolea akiwa Katibu wa UWT Wilaya ya Mzizima, Dar es Salaam mwaka 1967.


Mwaka 1968, alichaguliwa kufanya kazi ya kumhudumia mke wa hayati Patrice Lumumba akiwa Ikulu, Dar es Salaam na baadaye mwaka huo huo alijiunga na kozi ya miezi tisa katika Chuo cha Siasa Kivukoni.


Mwaka 1969 alirudi UWT Mzizima, lakini safari hii akiwa Katibu wa Wilaya kwa kuajiriwa na mwaka uliofuta alichukuliwa na Makao Makuu ya Umoja wa Vijana Tanzania (UVT) kwa ajili ya mafunzo ya halaiki yaliyokuwa yakitolewa na Wakorea.


Baada ya mafunzo hayo, aliteuliwa kuzunguka nchi nzima kwa ajili ya kutathmini maendeleo yaliyopatikana baada ya miaka 10 ya Uhuru kwa ajili ya kuwaonyesha Waingereza waliokuwa wamealikwa kwenye sherehe za Uhuru za mwaka 1971. Pia, alikuwa msimamizi wa halaiki.


Mwaka uliofuata aliteuliwa kwenda Zanzibar kuongoza walimu 10 kufundisha vijana halaiki kwa ajili ya tamasha la Vijana wa Afrika lililofanyika Zanzibar mwaka 1973.


Pia, mwaka huo huo aliteuliwa kuandaa tamasha la sherehe za miaka 20 ya TANU zilizofanyika mwaka uliofuata jijini Dar es Salaam.

Marehemu ameacha watoto watatu, wajukuu 14 na vilembwe wanne.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages