*Azim Dewji aanza kuajiri, kujenga kituo maalumu Mwanza
*Kwa kuanzia atenga sh milioni 100 kulea watoto albino
WATANZANIA
wenye ulemavu wa ngozi (albino) wapatao 76 wameuawa, na wengine
wanaokaridiwa kufikia 34 wameachwa na ulemavu wa kudumu kutokana na
viungo vyao mbalimbali kukatwa katika mashambulizi yanayoashiria
ushirikina uliokithiri.
Mauaji
na mashambulizi hayo yamefanyika kwa wingi katika mikoa ya Kanda ya
Ziwa, kati ya kipindi cha kuanzia mwaka 2005/2006 mpaka mwaka huu.
Yalitulia kidogo kati ya mwaka 2012 na 2013, lakini mwaka huu yameibuka
upya. Mikoa inayotajwa sana kwa matukio haya ni Mwanza, Tabora, Kagera,
Mara na Geita.
Kuanzia
mwaka 2006 mpaka mwaka huu, jumla ya mashauri 35 yanayohusu mauaji na
mashamnbulizi hayo yamefikishwa katika mahakama ambako watuhumiwa 139
walishitakiwa, 15 wakapatikana na hatia huku 73 wakiachiwa huru kutokana
na ushiriki wao kukosa ushahidi wa kutosha.
Hatua
kadhaa zimechukuliwa kujaribu kuwalinda ndugu zetu albino. Katika Kanda
ya Ziwa pekee, Polisi imewatia nguvuni waganga wa kienyeji 225
ikiwatuhumu kuhusika katika matukio ya mauaji hayo. Kadhalika wigo wa
kusaka watuhumiwa umepanuliwa hadi kufika katika mikoa ya Simiyu,
Shinyanga, Katavi na Rukwa.
Viongozi
wetu, wa kila nyanja, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, wamejitokeza kukemea
uovu huu. Rais amekaririwa akisema kwamba hataachwa mtu yeyote
anayeshiriki katika mauaji haya.
Desemba
14, mwaka jana mjini Dar es Salaam, akizungumza katika Harambee ya
Kusaidia Watoto Wenye Ulemavu wa Ngozi wa Kituo cha Buhangija,
Shinyanga, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alieleza kwamba takwimu za
Shirika la Afya Duniani (WHO) zilikuwa zinaonesha kwamba Tanzania ina
walemavu wa ngozi wapatao 170, 000.
Lakini
akaongeza kwamba ni vigumu sana kupata takwimu za hakika za walemavu
hawa kwa vile wengine hufichwa wanapozaliwa, na wengine wanazaliwa
katika maeneo ya mbali ambako taarifa zao haziwezi kufahamika kwa
urahisi.
Pinda
amekuwa mara kwa mara akishiriki kuelimisha jamii iwalinde albino. Yeye
mwenyewe analea albino kadhaa. Huko nyuma alipata kutoa machozi
bungeni, akielezea kusikitishwa kwake na mauaji hayo.
Tayari
Jaji Mkuu, Othman Chande, ameahidi kwamba mahakama itatoa kipaumbele
kwa kesi zinazohusu na mauaji ya albino akieleza kwamba mauaji hayo
yanakiuka haki za binadamu.
Sasa
kila Mtanzania mwenye mapenzi na nchi yetu anafahamu ni kwa jinsi gani
mauaji haya yalivyolipaka matope Taifa. Anafahamu aibu ambayo imelifika
Taifa kutokana na vitendo vya baadhi yetu kufikiri kwamba viungo vya
albino vinaweza kuwafanya wawe matajiri!
Hizo
si fikra za kweli. Hakuna njia ya mkato kuelekea kwenye utajiri. Hatuna
matajiri wengi hapa Taazania, na hao wachache tunaowaona, mali zao
zimetokana na jasho na jitihada zao kubwa. Wengine tumo kwenye biashara
kwa zaidi ya miaka 30 sasa, na bado hatuwezi kujiita matajiri.
Mauaji
haya, yana sababu nyingi, lakini mimi naona kwamba sababu kubwa ni
elimu ndogo. Hakika kama mtu uelewa wake ni mdogo kiasi cha kufikiri
kwamba kiungo cha albino kinaweza kumpa utajiri, hata akiweza kupata
hiyo mali hataweza kudumu nayo kwa sababu hiyohiyo ya elimu duni.
Nimeomba
nikutane na waandishi wa habari ili kwa pamoja tujaribu kutafuta
suluhisho la mauaji haya ya albino. Njia ya kuanzia, kwa maoni yangu, ni
kuwajua wako wapi.
Mimi,
familia na kampuni yangu ya Simba Trailer Manufacturers Ltd tumejaribu.
Tumeajiri mmoja wa hawa ndugu zetu. Yeye sasa ni sehemu ya familia yetu
pana kama kampuni. Nimekuja naye hapa. Anaweza baadaye kutoa ushuhuda.
Lakini mipango yetu kama kampuni ni kuajiri walau wawili wengine.
Maoni
yetu ni kuwa kama kila mtu mwenye kampuni, si lazima iwe kampuni kubwa,
angeajiri walau albino watatu, tungekuwa nao karibu.
Natoa
mwito kwa Watanzania wote wenye uwezo wa kuajiri watu watatu na zaidi,
kuwaajiri ndugu zetu albino. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza sana
uwezekano wa wao kuwindwa kama vile si binadamu. Makampuni 350
yakiajiri kila moja angalau albino watatu, tutakuwa na uhakika wa
kuingiza albino zaidi ya 1000 katika ajira rasmi, hii ni kwa kuanzia.
Kadhalika
nina mpango wa kujenga kituo mkoani Mwanza ambacho kitaweza kuhifadhi
albino 100 kwa wakati mmoja pia tutakuwa tunawahudumia chakula na
mavazi.vile vile tutaomba serekali ya mkoa kuwapatie shule na sisi
upande wetu tuta wapa usafiri.
Kutokana
na dhamira hiyo ambayo nimeitengea sh milioni 100 kwa kuanzia, namuomba
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza atutengee angalau ekari kumi za ardhi kwa ajili
ya ujenzi wa kituo hicho. Itapendeza zaidi kama kitakuwa karibu na eneo
la barabara kuu na pia karibu na huduma muhimu zikiwemo za maji na
umeme.
Shime Watanzania, hasa wafanyabiashara tuungane katika hili. Tumevuka mengi, hakika hata hili la mauaji ya albino tutalishinda.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269