Waziari wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ametoa hotuba, iliyojaa matumaini wakati
akifungua
mkutano wa majadiliano kuhusu uboreshaji wa mfumo wa usimamizi na uendeshaji Maeneo
ya Jumuia ya Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (WMA), ulioanza jana, Julai 2, 2015, katika ukumbi wa Hotel ya Naura Spring, jijini Arusha. theNkoromo Blog inakuletea hotuba hiyo kama alivyoioma Waziri Nyalandu.
Mhe.
Mahmood Mgimwa - Naibu Waziri,Wizara ya Maliasili na Utalii;
Dkt. Adelherm Meru - Katibu
Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii;
Bw. Herman Keraryo - Mkurugenzi,
Idara ya Wanyamapori;
Dkt. Simon Mduma - Mkurugenzi
Mkuu,Taasisi ya Utafiti wa
Wanyamapori;
Dkt.
Freddy Manongi - Mhifadhi Mkuu, Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorogoro;
Bw. Allan Kijazi - Mkurugenzi Mkuu, Hifadhi za Taifa;
Mwenyekiti, Muungano wa
Jumuiya Zilizoidhinishwa;
Wakurugenzi/ Wawakilishi wa
Mashirika yasiyo ya Kiserikali
(USAID, WWF, FZS, AWF,
WCS);
Viongozi wa Maeneo ya
Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori;
Wawakilishi kutoka Sekta
binafsi;
Watumishi wa Wizara ya
Maliasili na Utalii;
Maafisa Wanyamapori wa
Wilaya;
Mabibi na Mabwana.
Napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wote katika
mkutano huu muhimu unaolenga kutathmini ustawi na changamoto
zilizojitokeza/zinazojitokeza katika usimamizi wa shughuli za uhifadhi kwenye Maeneo
ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori “Wildlife Management Areas” (WMAs) nchini.
Wageni
Waalikwa, Mabibi na Mabwana
Sera ya wanyamapori ya mwaka 1998 kwa mara ya kwanza
nchini ilielekeza kuanzisha dhana ya ushirikishaji wa jamii katika uhifadhi wa
wanyamapori. Dhana hii inatoa fursa kwa wananchi kushiriki katika uhifadhi kwa
kutenga maeneo ya ardhi ya vijiji ili kusimamia na kunufaika moja kwa moja kupitia
rasilimali ya wanyamapori. Utekelezaji wa dhana hii ulianza rasmi mwaka 2003 na
hadi sasa maeneo ya WMAs 21 zenye ukubwa wa kilometa za mraba 36237.7 yameidhinishwa
na kutangazwa katika gazeti la serikali. Aidha, maeneo mengine 17 ya WMA yapo
katika hatua mbalimbali za uanzishwaji.
Wageni
Waalikwa, Mabibi na Mabwana
Kwa miaka 12 ya utekelezaji wa dhana hii tumeshuhudia
mwamko katika jamii kushiriki katika kiuhifadhi, na wao kujipatia manufaa ikiwemo
ajira, kipato katika ngazi ya jumuia, vijiji husika na kuchangia katika miradi
ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji. Pamoja na mafanikio haya bado
kumekuwepo na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa dhana
hii nchini. Hivyo mkutano huu ni
mwendelezo wa matokeo ya tuliyojifunza wakati wa kutekeleza dhana ya
kushirikisha jamii katika uhifadhi kwa kuwaleta pamoja wadau muhimu na wataalamu
ili kubadilishana uelewa, uzoefu, matokeo ya tafiti, na kutoa fursa ya
mjadiliano rasmi yenye malengo kujitathimini mahali tulipotoka, tulipo na tunapotakiwa kwenda.
Wageni
Waalikwa, Mabibi na Mabwana
Naomba nijikite katika changamoto chache lakini muhimu
ambazo mimi kama Waziri mwenye dhamana nimeziona katika kutekeleza majukumu
yangu ambayo ningependa kupitia mkutano huu uziangalie kwa kina na kutusaidia
kutoa ushauri wa kuandaa maelekezo ya kisera yatakayoweza kutoa majibu kama
ifuatavyo:-
1. Kuchangia
uboreshaji wa utawala bora katika rasilimali za wanyamapori na matokeo ya jamii
na uhifadhi wa wanyamapori, ikiwa pamoja na kuhakikisha utawala bora kulingana
na maslahi na haki za jamii (muingiliano wa mamlaka kati ya viongozi wa wilaya,
vijiji na wale wa jumuiya/WMA na mgongano wa maslahi).
2. Migogoro
inayotokana na uwekezaji katika maeneo ya WMA mfano MBOMIPA.
3. Mgogoro
unaotokana na gharama za watalii katika hoteli na loji zilizopo ndani ya
hifadhi za Taifa na zile zilizopo ndani ya WMAs zinazopakana.
4. Uwiano
wa mgawanyo wa mafao yatokanayo na uwekezaji katika maeneo ya WMAs kati ya
Jumuiya/WMA, Serikali kuu, halmashauri za wilaya na vijiji wanachama.
5. Matumizi
ya fedha/mapato zinazotokana katika WMA na katika vijiji kutofanya kazi
zitarajiwa.
6. Ucheleweshaji
wa mgao wa fedha unaotakiwa kupelekwa katika WMAs kutoka Serikalini.
Wageni
Waalikwa Mabibi na Mabwana,
Mkutano huu ambao ni wa kwanza kufanyika na kukutanisha
Wizara, Jumuiya Zilizoidhinishwa na Wawezeshaji wa WMAs ni fursa muhimu ambayo
ikitumika ipasavyo na kwa nia njema itatoa suluhisho lkwa changamoto
nilizozianisha hajo juu. Hivyo natoa wito kwa washiriki wa mkutano huu kuhakikisha
fursa hii haipote bali itoe tija katika ustawi wa dhana ya kushirikisha jamii
katika uhifadhi endelevu na wenye manufaa kwa jamii.
Wageni
Waalikwa Mabibi na Mabwana
Mwisho lakini sio kwa umuhimu napenda kuchukua fursa hii
kuwashukuru wawezeshaji katika uanzishaji na uendeshaji wa WMA. Kipekee
nitambue michango iliyotolewa na USAID,
WWF, FZS, AWF, WCS, KfW, BTC, DANIDA, GTZ (GIZ) na AFRICARE. Aidha,
ninawashukuru USAID, AWF na WWF kwa ufadhili wao katika kufanikisha mkutano
huu. Ni matumaini yangu kuwa mkutano huu utaleta tija inayokusudiwa ili
kuhakikisha kuwa shughuli za uhifadhi katika WMA zinaendeshwa kwa ufanisi.
Natangaza rasmi Mkutano huu
umefunguliwa.
Tutapata habari zaidi wapi?
ReplyDelete