Breaking News

Your Ad Spot

Jul 22, 2015

KURA ZAANZA KUHESABIWA BURUNDI

Rais Pierre Nkurunziza
Na RFI
Zoezi la kuhesabu kura limeanza Jumanne jioni wiki hii nchini Burundi baada ya uchaguzi wa urais ambao umesusiwa na upinani na kufutiliwa mbali na jumuiya ya kimataifa.
Rais anaye maliza muda wake Pierre Nkurunzinza anatarajiwa kushinda kwa asilimia kubwa, baada ya kushindana na vyama vidogo vitatu ambavyo ni washirika wa utawala.
Marekani imeonya kuwa uchaguzi uliofanyika Jumanne Julai 21 katika mazingira yanayojiri kwa sasa nchini Burundi hautakuwa wa kuaminika na utazidi kuidhoofisha serikali, amesema John Kirby, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani.(P.T)
John Kirby amesema ana hufo kuwa zoezi hilo la uchaguzi lililogubikwa na utata, huenda liikazua vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Wakati huo huo Ubelgiji imesema haiutambui uchaguzi huo ambao umefanyika katika mazingira ya kutatanisha, huku ikibani kwamba haitozitambua taasisi zitakazotokana na uchaguzi wa urais na ule wa wabunge na madiwani.
Pierre Nkurunzinza anawania awamu ya tatu madarakani, licha ya awamu mbili za kukaa madarakani zilizowekwa kwa mujibu wa katiba.
Wagombea wengi kupitia vyama vya upinzani wamesusia uchaguzi huo. Wakati huohuo katika kijiji cha Buye kaskazini mwa nchi, alikozaliwa Rais Nkurunziza mlolongo wa watu wamejitokeza kupiga kura.
Uchaguzi huu umefanyika katika hali ya wasiwasi ya kisiasa baada ya kusitishwa kwa mazungumzo kati ya serikali na upinzani. Kama ilivyokua katika uchaguzi wa wabunge na madiwani Juni 29, upinzani umeamua kususia uchaguzi huu.
Marais wa zamani, Sylvestre Ntibantunganya na Domitien Ndayizeye, ikiwa ni pamoja na kiongozi wa chama cha Frodebu Nyakuri, Jean Minani, walionesha msimamo wao, kwamba matokeo ya uchaguzi huo yatakua batili. Lakini kwa upande wake mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi (Ceni), amesema zoezi la kuondoa faili zao kwenye Tume huru ya Uchaguzi halikufuata utaratibu. Wangelipaswa kila mmoja kuandika barua yake binafsi ya kuondoa faili zao kwenye tume huru ya Uchaguzi, amesema Pierre Claver-Ndayicariye.
" Hatutashiriki katika uchaguzi huu wa kuigiza na tunatoa wito kwa wafuasi wetu kususia uchaguzi huu ", wamesema viongozi hawa wa kihistoria katika siasa nchini Burundi.
Hata hivyo mshauri mkuu wa rais katika masuala ya mawasiliano, Willy Nyamitwe amesema uamzi wa viongozi hao hauna uzito wowote wakati huu.
" Wakati wanajua kuwa hawana usemi wala nguvu yoyote wakati huu nchini, ni lazima watafute kisingizio cha kujiondoa katika uchaguzi ", amesema Willy Nyamitwe.
Mashambulizi ya guruneti na milio ya risasi
Hayo yakijiri Jumatatu alaasiri wiki hii utawala wa Bujumbura ulikutana na mabalozi wa Umoja wa Ulaya, ambapo kulijitokeza mvutano kati ya pande hizi. Mabalozi wa Umoja wa Ulaya wameitaka serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo ili kutafutia ufumbuzi mgogoro unaendelea kushuhudiwa nchini humo. Mabalozi hao wameendelea kusema kuwa kuna hatari nchi ya Burundi kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Wakati huo huo milio ya risasi na milipuko ya mabomu imeendelea kusikika Jumatatu jioni hadi usiku kucha mjini Bujumbura, hasa katika wilaya za Bwiza na Nyakabiga.
Inaarifiwa kuwa watu watatu ikiwa ni pamoja na raia mmoja na askari polisi wawili wameuawa usiku wa Jumatatu kuamkia Jumanne wiki hii mjini Bujumbura.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages