SAKATA la walimu wa Shule ya Msingi Nambaza, katika Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, kufanyiwa vitendo vya kishirikina na kutishiwa maisha, limeendelea kuumiza vichwa vya viongozi wilayani humo.
Viongozi
hao, leo wanatarajia kukutana katika kikao ambacho kitamshirikisha
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Ofisa Utumishi na Ofisa Elimu wa
Wilaya hiyo ili kujadili hatima ya walimu wa shule hiyo ambao wote
wamefungasha mizigo yao na kutoweka kijijini hapo wakihofia kuuawa na
baadhi ya ndugu wa watuhumiwa.
Kaimu
Ofisa Elimu wa Wilaya hiyo, Bw. Ruben Kaswamila, amesema kuwa kikao
hicho pamoja na mambo mengine, pia kitajadili tukio zima la Nambaza
ambalo ni la aibu na kushangaza ili kuangalia uwezekano wa kuwahamisha
walimu wote wageni na kuwapangia vituo vingine.
"Kesho
(leo) tutakuwa na kikao ambacho kitamhusisha Mkurugenzi, Ofisa Utumishi
na mimi Kaimu Ofisa Elimu ili kujadili suala zima la Nambaza na hatima
ya walimu wa shule hiyo waliodhalilishwa.
"Mwelekeo
wa kikao ni kuwahamisha walimu wote wageni na kuwapangia vituo vingine
vipya vya kazi kwani kuendelea kuwaacha hapo ni kuwahatarishia maisha
maana hata kisaikolojia hawawezi kufundisha shuleni hapo kwa ufanisi," alisema.
Alisema
uhamisho huo hautawahusu walimu watatu wa shule hiyo, Bw. Sospeter
Mafuru ambaye ni Mwalimu Mkuu, Bw. Medard Munaku anayestaafu Juni, 2016
na Bw. Renatus Molla ambaye naye anastaafu Februari, 2016 ambao ni
wazaliwa wa kijiji hicho ambao watabaki hapo shuleni kuwafundisha
watoto.
Aliongeza kuwa, Serikali ya kijiji na wanakijiji kwa ujumla watatafuta wenyewe walimu ili waongeze nguvu shuleni hapo.
"Kwakuwa
wanakijiji ndio waliosababisha hayo, watafute wenyewe walimu wa
kuwafundishia watoto wao kama ni wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na
cha sita wakubaliane, mshahara wawalipe wao kwa sababu walimu
walioletwa na Serikali, hawahitajiki kijijini," alisema.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, walimu wazawa kijijini hapo ambao inadaiwa ndio
watabaki kufundisha watoto, walisema hawako tayari kurudi kufundisha
shuleni hapo na kama mwajiri alikuwa na mpango wa kuwafukuza kazi afanye
hivyo si kurudi Nambaza.
Bw.
Mafuru alisema jana alifuatwa na watu ambao walimtukana, kumtemea mate
na kutishia kumuua tukio ambalo ameliripoti polisi sasa kwanini aendelee
kukaa kijijini hapo.
"Mimi
ni mzawa wa kijiji hiki lakini ni mtumishi wa Serikali kama walivyo
watumishi wengine, utumishi wangu ndio umesababisha nitendwe vibaya,
nitishiwe kuuawa na kuonekana sifai na adui miongoni mwa wanakijiji,
natishiwa sasa iweje niendelee kuwepo kijijini.
"Nambaza
sitakiwi tena nitauawa, uhai wa maisha yangu ni bora kuliko kazi, kama
mwajiri anataka kunifukuza kazi afanye hivyo lakini siwezi kurudi
Nambaza kufundisha," alisema.
Kwa
upande wake, Molla alisema, hawezi kurudi kufundisha Nambaza kwani
amevumilia mengi pamoja na kumpoteza mtoto wake katika mazingira ya
kishirikina lakini bado anatishiwa kuuawa hivyo ni bora afukuzwe kazi
akafanye shughuli nyingine kama mwajiri anaona kumbakiza kijijini hapo
atakuwa amemtendea haki kwa sheria za utumishi.
"Sitarudi
Nambaza, nipo tayari kufukuzwa kazi, mizigo na familia yangu nimeitoa
Nambaza baada ya kutendwa vibaya na wanakijiji, nimetishiwa kifo na hao
hao wanakijiji, kurudi hapo ni kwenda kufa, siwezi kufuata kifo
ninachokiona hadi Mwenyezi Mungu atakapoamua," alisema.
Aliongeza
kuwa, mwaka 2014 mwanaye alikufa katika mazingira ya kutatanisha
kishirikina kwani hakuugua bali alianguka njiani akitembea na kufa papo
hapo.
Mwalimu
Munaku, ambaye tayari amekwishajiondosha kijijini hapo akihofia kuuawa
kutokana na vitisho kutoka kwa wanakijiji, hakuweza kupatikana ili
kuzungumza kama yuko tayari kuendelea kufundisha shuleni hapo ama la.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269