Breaking News

Your Ad Spot

Jul 5, 2015

TASWIRA, KAULI YA MKWASA STARS IKIIKALIA KOONI UGANDA VIKO HAPA..

Mshambuliaji wa Taifa Stars, John Bocco akishangilia goli lake 
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premieum Lager imetoka sare ya bao 1- 1 dhidi ya wenyeji Uganda (The Cranes) katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za CHAN mwaka 2017 nchini Rwanda uliofanyika uwanja wa Nakivubo. 
Stars ambayo imeonekana kabadilika ikicheza soka la kuvutia tangu mwanzo mpaka mwisho wa mchezo na hali hiyo iliyowaduwaza wenyeji Uganda. 
Mshambuliaji wa Taifa Stars, Rashid Mandawa (kushoto) akijaribu kumtoka Hassan Waswa 
Mpaka dakika 45 za mchezo za kipindi cha kwanza zinamalizika, Uganda 0 - 0 Tanzania. Kipindi cha pili kilianza kwa Stars kufanya mashambulizi mfululizo kupitia kwa washambuliaji wake John Bocco na Rashid Mandawa. 

Dakika ya 58, John Bocco aliipatia Tanzania bao la kwanza kwa mkwaju wa penati kufuatia mlinzi wa Uganda Bakaki Shafik kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari. 
Baadhi ya Watanzania waliokwenda Uganda kuipa sapoti Stars 
Mara baada ya bao hilo Uganda walifanya mashambulizi mfululizo langoni mwa Stars na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 82, kupitia kwa mchezaji Kizito Hezron. 


Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika Uganda 1 - 1 Tanzania. Kwa matokeo hayo Uganda wanasonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 4 - 1 na sasa watakutana na Sudan. 
Kikosi cha Stars kilichoanza dhidi ya Uganda 
Mara baada ya mchezo huo kocha mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema anashukuru vijana wake wamejitahidi kucheza vizuri, mchezo ulikua mzuri, timu ilitengeneza nafasi chache na kuweza kutumia nafasi moja iliyopatikana. 


Mkwasa amewaomba watanzania kuendelea kuwapa sapoti kwani wamekaa na kwa wiki moja tu lakini imeonesha mabadiliko , hivyo wanahitaji muda mrefu kukaa na vijana ili kujenga timu bora. 


Stars inatarajiwa kurejea Tanzania siku ya Jumatatu mchana kwa usafiri wa shirika la ndege la Rwanda Air. 


Taifa Stars: Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Haji Mngwali, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Mudathir Yahya, Deus Kaseke, Frank Domayo,/Said Ndemla John Bocco, Rashid Mandawa/Salum Telela, Saimon Msuva/Ramadhan Singano. 


The Cranes: James Alitho, Muzamiru Mutyaba, Brian Ochwo, Hassan Waswa, Denis Oola, Faruk Miya, John Shemazi/Robert Sentongo, Bakaki Shafik, Tekkwo Derick/Kizito Hezron/Kalanda Frank.
-Na Baraka Mpenja

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages