.

TAMASHA LA KIMATAIFA LA SANAA NA UTAMADUNI KUFANYIKA SEPTEMBA 21-27, 2015 WILAYANI BAGAMOYO

Aug 14, 2015

 Mwenyekiti wa Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, John Mponda (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu tamasha hilo litakalofanyika kwa mara ya 34 kuanzia tarehe 21-27 Septemba katika ukumbi na viunga vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ambao ndio wenyeji na waandaaji wa tamasha hilo kongwe Tanzania. Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maonyesho ya tamasha hilo, Christa Komba na kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi na Majukwaa, Frank Sika.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Maonyesho ya tamasha hilo, Christa Komba (kulia), akizungumza katika mkutano huo.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi na Majukwaa, Frank Sika (kushoto), akizungumzia maonyesho yanavyofanyika katika majukwaa.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ikichukuliwa na wanahabari.

............................................................................................................................................................. 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU .TAMASHA LA 34 LA KIMATAIFA LA SANAA NA UTAMADUNI BAGAMOYO

Tamasha la kimataifa la sanaa na utamaduni Bagamoyo liliasisiwa mwaka 1981 na Chuo cha Sanaa Bagamoyo ambacho kwa sasa ni Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo. Lengo kuu la Tamasha kwa wakati huo ilikuwa ni kuwapa nafasi wanafunzi wa chuo cha sanaa kuonyesha kwa vitendo yale waliojifunza kwa mwaka mzima kwa kuwashirikisha wakazi wa Bagamoyo, baada ya Tamasha hilo kufanikiwa uongozi wa chuo uliamua tamasha hilo lifanyike kila mwaka kwa kushirikisha Vikundi mbalimbali vya ndani na nje ya nchi ili kubadilishana Uzoefu  na hivyo kujizolea umaarufu ndani na nje ya Tanzania.

Tamasha la kimataifa la sanaa na utamaduni Bagamoyo mwaka huu litafanyika kwa mara ya 34 kuanzia tarehe 21-27 Septemba katika kumbi na viunga vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ambao ndio wenyeji na waandaaji wa tamasha hilo kongwe Tanzania.

Tamasha la mwaka huu linabeba Kauli mbiu isemayo SANAA NA UTAMADUNI KATIKA UCHAGUZI HURU NA WA AMANI’  Aidha kutakuwa na mada ndogondogo zitakazotolewa kupitia kongamano na warsha zitakazohusu  Haki za binadamu, Rushwa na kupinga Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino)

Tamasha la mwaka huu litahusisha Ngoma za Asili, Maigizo, Sarakasi, Mazingaombwe, Muziki wa kisasa na asili, Sanaa za Ufundi  na bidhaa mbalimbali.

Hadi sasa jumla ya vikundi 48 kutoka ndani na nje ya Tanzania vimethibitisha kushiriki,ambapo vikundi 43 ni kutoka ndani ya Tanzania na vikundi 5 kutoka nchi za Kenya, Namibia, Afrika Kusini, Korea na Congo.
Hadi kufikia sasa hakuna mdhamini yoyote aliyejitokeza kudhamini Tamasha hili na hii imepelekea vikundi kujigharamia na TaSUBa kugharamia Uendeshaji,hivyo Taasisi inatoa wito kwa wadau mbalimbali wa sanaa,Makampuni,Taasisi za serikali na zisizo za serikali kujitokeza kudhamini tamasha hili muhimu kwa mustakabali wa sanaa na utamaduni wa Mtanzania.

Kwa yeyote anayehitaji kuchangia tamasha hili anaombwa awasiliane na Kamati ya maandalizi kwa mawasiliano hapo chini. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª