Breaking News

Your Ad Spot

Sep 25, 2015

BAKWATA YATAJA MAJINA YA WATANZANIA WALIOKUFA MECCA KWENYE HIJA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Bismilah Rahman Raheem
Assalaam alaykum warahmatullahi wa barakaatuhu.
Taarifa hii inahusu tukio lilitokea jana Mina Saudi Arabia wakati mahujaji wakielekea kwenye Jamaraat , palitokea msongamano mkubwa ( stampede) na kupelekea mahujaji zaidi ya 700 kufariki na mamia kadhaa kujeruhiwa.
Tayari tumethibitisha kutokea vifo vya watu watano waliotokea Tanzania miongoni mwao mmoja ni raia wa Kenya na wengine wanne ni Watanzania.
Watanzania waliotambuliwa hadi jana usiku wametajwa kuwa ni Bi Mwanaisha Hassan Juma, Mkungwe Suleiman Hemedi na Sefu Saidi Kitimla.
Mwanamke mwingine mmoja Mtanzania jina halijaweza kupatikana hadi Alhamisi usiku wakati tukiandaa taarifa hii.
Raia wa Kenya ametambuliwa kwa jina la Bi Fatuma Mohammed Jama.
Kuna taarifa ya mahujaji wanawake wawili ambao hadi Alhamisi usiku walikua hawajapatikana hivyo hatukua na uhakika juu ya usalama wao hadi tutakapowaona ama kupata taarifa zao.
Ifahamike kuwa majina yamepatikana kupitia vitambulisho vyao ambavyo wahanga wa tukio hili waliweza kuvichukua kutoka kwenye miili ya marehemu.
Nimepokea taarifa za majeruhi miongoni mwa mahujaji wetu wa Tanzania na baadhi ya majeruhi hao nimeonana nao mara baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Vilevile nimeagiza maafisa wetu wa Bakwata nilionao hapa Mina kuendelea kufuatilia habari na taarifa za mahujaji wetu katika hospitali na sehemu za kuhifadhia maiti.
Nimefanya hivyo ili niweze kuwa na uhakika juu ya usalama wa mahujaji wetu.
Katika kipindi hiki cha taharuki kubwa tunafanya mawasiliano na wizara husika hapa Saudi Arabia kwa kushirikiana na serikali yetu kupitia ubalozi wetu hapa Saudi Arabia.
Natambua uwepo wa mkanganyiko wa taarifa ambazo zinazidisha taharuki kwa ndugu na jamaa wa mahujaji wetu.
Nachukua fursa hii kuwaomba ndugu na jamaa wa mahujaji kuwa watulivu na kuwa na subra katika wakati huu mgumu sana kwetu sote.
Tunaendelea kufuatilia kwa karibu sana na Insha Allah mara tu tukipata taarifa za uhakika basi tutawafahamisha.
Kutokana na idadi ya maiti kuwa kubwa serikali ya Saudi Arabia wanaendelea na zoezi la kutambua uraia wa kila mwili ili waweze kutoa taarifa tunatarajia wakati wowote tutakuwa tumepata taarifa zaidi.
Wabillahi Tawfiiq.
Sheikh Abu Bakari Zuberi
Mufti wa Tanzania.
MECCA, Saudi Arabia
25/09/2015

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages