Na Anna Nkinda – Maelezo, Liwale
…………………………………………..
Wananchi wa mkoa wa Lindi wameaswa
kufanya kazi kwa bidii ili waweze kujiletea mabadiliko ya kweli katika
maisha yao kwani kuna baadhi ya watu hawapendi kufanya kazi huku
wakisubiri mabadiliko.
Rai hiyo imetolewa jana na Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wananchi
wa vijiji vya Ngunichile na Mbaya vilivyopo katika majimbo ya
Nachingwea na Liwale waliohudhuria mkutano wa kampeni ya kuwanadi
wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kupitia tiketi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini
alisema mabadiliko ya kweli hayawezi kupatikana bila ya kufanya kazi
kwani kuna baadhi ya watu hasa vijana hawafanyi kazi wakiamka asubuhi
kitu wanachokifanya ni kucheza pool huku wakisubiri mabadiliko.
“Hata katika vitabu vya dini
imeandikwa asiyefanya kazi na asile kwani kazi ni msingi wa maendeleo,
hata ukipiga kelele kiasi gani kama hufanyi kazi huwezi kupata
mabadiliko katika maisha yako”.
“Ndugu zangu Mwenyezi Mungu
ametupa akili ya kutambua mema na mabaya tusikubali kudanganywa,
mabadiliko ya siku hizi siyo mazuri yanaleta uvunjifu wa Amani kwani
watu wamepandikizwa maneno ya chuki wanafanya vurumai na kuharibu vya
kwao, wanawachukia ndugu zao imefikia hatua watu hawazikani,
hawasalimiani. Lakini hao aliowapandikiza chuki kwao kuna maendeleo”,
alisisitiza.
Mama Kikwete alisema yeye kama
MNEC anadhamana kubwa ya kuhakikisha anakisemea na kukipigania chama
chake na kuwataka wananchi hao kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa
kufanya hivyo wataitunza Amani ya nchi na kuzidi kudumisha upendo katika
jamii yao.
Aidha aliwasihi wananchi hao
kutokubali kurubuniwa na kitu chochote bali wazitunze kadi zao za
kupigia kura na siku ya uchaguzi ikifika wasipoteze haki yao ya msingi
ya kupiga kura wajitokeze kwa wingi na kuwachagua viongozi kutoka CCM
ambao watawaletea maendeleo ya kweli.
Kwa upande wake mgombea ubunge
jimbo la Nachingwea Hassan Massala aliahidi kama atachaguliwa kuwa
mbunge wa jimbo atasimamia ilani ya uchaguzi ya CCM na kuhakikisha
huduma za elimu zinaboreshwa hii ni pamoja na shule kuwa na vitabu na
walimu wa kutosha na kujenga nyumba za walimu ili watoto wapate elimu
bora. Ataboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila
kijiji kinakuwa na Zahanati na dawa zinapatikana kwa wakati.
Massala alisema, “Katika jimbo
hili, maeneo ya mjini kuna maji ya kutosha lakini kijiji cha Ngunichile
kuna tatizo ingawa vyanzo vya maji vipo. Nitahakikisha maji
yanapatikana. Kuhusu umeme Serikali inampango wa kusambaza katika
vijiji vyote, nguzo zimeanza kusambazwa kinachohitajika ni kusimamia
ili zoezi hili liende haraka”.
Mgombea huyo wa nafasi ya Ubunge
alimuomba Mama Kikwete awasaidie ili mnara wa mawasiliano ya simu uweze
kujengwa katika kata ya Ngunichile kwani eneo hilo linashida ya
mawasiliano.
“Ukiwa katika kijiji hiki huwezi
kuwasiliana na mtu yeyote kwa njia ya simu kwa kuwa hakuna mnara wa
mawasiliano. Hivi sasa simu ni pesa na simu ni Benki tunaomba Mama yetu
utusaidie ili mnara wa mawasiliano ujengwe katika kijiji hiki”, Massala
aliomba.
Kuhusu ombi la kujengewa mnara wa
mawasiliano ya simu katika kijiji hicho ambacho ni kata ya Ngunichile
Mama Kikwete aliahidi kulifanyia kazi na kulifikisha kunakohusika.
Naye mgombea ubunge wa jimbo la
Liwale Faith Mitambo aliwaomba wananchi wamchague ili aendelee
kuwatumikia kwa kipindi kingine cha miaka mitano na kuhakikisha
maendeleo yanazidi kupatikana katika jimbo hilo.
Mitambo alisema, “Ilani ya
uchaguzi ya CCM inasema itaendelea kuboresha huduma ya afya na ndani ya
mwaka mmoja baada ya uchaguzi Zahanati ya kijiji cha Mbaya itakuwa kituo
cha Afya. Aidha Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa
ajili ya kuhakikisha umeme unapatikana vijijini kati ya vijiji hivyo
kimojawapo ni kijiji hiki.
“Nawaomba kura zenu ili mtuchague
viongozi kutoka CCM ambao ni madiwani, mbunge na rais ili tuweze
kusimamia na kutekeleza kwa vitendo na kuhakikisha yale yote
yaliyoandikwa katika ilani ya uchaguzi yanatekelezwa”,.

No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269