Breaking News

Your Ad Spot

Oct 2, 2015

VIJANA SITA WA JKT BULOMBORA KIGOMA WAMEPOTEZA MAISHA, 21 WAJERUHIWA KATIKA AJALI

VIJANA sita waliokuwa katika mafunzo ya kijeshi ya kujitolea katika kikosi cha 821 JKT Bulombora mkoani Kigoma wamefariki dunia na wengine 21 kujeruhiwa vibaya kutokana na ajali ya gari iliyotokea jioni hii.
Mganga Mfawidhi wa hospital ya mkoa wa Kigoma Dkt. Fadhil Kibaya amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
"Ni kweli leo majira ya saa moja jioni tumepokea miili minne ya vijana wa JKT ambao waliletwa hapa tayari wamefariki na majeruhi 21. "Wengine wawili wamefariki hapa hapa wakati tukiendelea kuwapa huduma"alisema Dkt Fadhili.
Alisema hali za majeruhi mpaka sasa siyo nzuri sana kwani wengi wameumia sehemu za kichwa na mwilini. "Bado tunaendelea na jitahada za kuwapatia matibabu na majina ya waliopoteza maisha pamoja majeruhi tutatoa kesho, sababu majeruhi wengi hawana fahamu"alisema.
Naye kamanda wa polisi mkoa wa kigoma Afande Ferdinand Mtui alisema chanzo cha ajali hiyo ni gari hilo la jeshi kushindwa kupanda mlima na kusababisha tairi mbili za nyuma kupasuka.
Alisema ajali hiyo imetokea katika eneo la Kasaka karibu na mizani ambapo lori hilo la jeshi lilikuwa likitoka mjini kwenda kambini likiwa limebeba makreti ya soda na unga.

Credit: Michuzi

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages