Breaking News

Your Ad Spot

Nov 6, 2015

ENEO LA LEBANON KATIKA SOKO LA KIMATAIFA LA SAMAKI LA FERI JIJINI DAR ES SALAAM NI HATARI KWA UCHUMI, IKULU


Mwenyekiti wa Kamati ya Soko la Samaki la Kimataifa la Feri, Ali Kibwana, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi wanaotembelea masoko mbalimbali ya Manispaa ya Ilala kuona jinsi gani vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia umepungua katika soko hilo baada ya Shirika la Equality for Growth (EfG) kutoa mafunzo ya kupinga ukatili katika masoko hayo. Kushoto ni Mwezeshaji wa Sheria katika soko hilo, Bakari Said.
Mwezeshaji wa Sheria katika soko hilo, Bakari Said akizungumza katika mkutano huo.
Mama Lishe wa soko hilo, Taus Barnabas, akichangia neno katika mkutano huo.
Mama Lishe wa soko hilo, Fatuma Saijali (katikati), akizungumza katika mkutano huo.
Mwezeshaji wa Sheria katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri, Asha Malenda (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, wanaotembelea masoko mbalimbali ya Manispaa ya Ilala kuona jinsi gani vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia umepungua katika soko hilo baada ya Shirika la Equality for Growth (EfG) kutoa mafunzo ya kupinga ukatili katika masoko yaliyopo Manispaa ya Ilala. Kulia ni Mama Lishe wa soko hilo, Taus Barnabas na Fatuma Saijali.
Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa EfG, Shaban Rulimbiye (kulia), akizungumzia kuhusu mradi huo wa miaka mitatu wa Mpe Riziki si Matusi.
Kamanda wa Ulinzi na Mazingira wa Soko hilo, Nurdin Hassan akisisitiza jambo kuhusu wanavyo imarisha ulinzi katika soko hilo.
Mwonekano wa sehemu ya soko la Samaki la Feri

Na Dotto Mwaibale

ENEO la Lebanon katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri ambalo lipo jirani na Ikulu jijini Dar es Salaam limedaiwa kuwa ni hatari kwa wafanyabiashara wa soko hilo na kuwa linadhohofisha uchumi kutokana na kukithiri kwa watu wasio rasmi.

Hayo yamebainishwa na Mwezeshaji wa Sheria wa soko hilo, Asha Malenda wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi wanaotembelea masoko mbalimbali ya Manispaa ya Ilala kuona jinsi gani vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia umepungua katika soko hilo baada ya Shirika la Equality for Growth (EfG) kutoa mafunzo ya kupinga ukatili katika masoko hayo.

"Tunachangamoto kubwa sana katika soko letu la Feri tunayoipata kutoka eneo la Lebanon lenye mwingiliano wa watu wasio rasmi kutoka nje ya soko ambao ni kama wamejianzishia soko lao na wamekuwa na maamuzi yao lakini viongozi wa soko la Feri wanashindwa kuwachukulia hatua hali ambayo inatudhalilisha sisi wafanyabiashara hasa mama lishe na kuharibu uchumi wa soko letu" alisema Malenda.

Alisema wengi wa watu waliopo katika eneo hilo lisilo rasmi wamekuwa wakifanya biashara kiholela huku wakipika vyakula katika maeneo yanayoweza kuhatarisha afya ya mlaji wakati katika soko hilo kuna eneo maalumu la mama lishe na wengi wa watu hao wakienda kula eneo hilo rasmi wamekuwa hawalipi fedha na wakibanwa kulipa wanadiliki kutoa visu na silaha za jadi kuwatishia wanaodai.

"Eneo hilo la Lebanon ni hatari na kinachoshangaza linatizamana na Ikulu lakini hakuna hatua yoyote ya makusudi inayochukuliwa na viongozi wetu na linapopelekwa kwa viongozi wa kisiasa wanadai waachwe kwani ndio wapiga kura wao" alisema Mwezeshaji wa Sheria katika soko hilo, Bakari Said.

Said alisema katika soko hilo kuna changoto nyingi za udhalilishaji wanawake kwa kushikwa katika maungo yao lakini kupitia EfG wamejitahidi kupunguza changamoto hizo kwani wasaidizi wa sheria waliopatiwa mafunzo na shirika hilo wanajitahidi kuupenyeza ujuzi waliopata kuifikishia jamii ambayo imeanza kuelewa kuhusu vitendo hivyo.

Aliongeza kuwa uvaaji wa nguo za kubana na kuacha vifua wazi kwa upande wa wanawake pia ulikuwa ukichochea kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji uliokuwa ukifanywa na vijana wasio rasmi katika eneo hilo la Feri ambao hawana makazi na maisha yao yapo Feri lakini baada ya kufikiwa na mafunzo ya EfG hali hiyo imepungua kwa asilimia 80.

Mwezeshaji Fatuma Saijali alisema changamoto kubwa iliyopo hivi sasa katika soko hilo ni kuzuiliwa kupika chakula katika eneo hilo la Feri lakini wakati huo huo kuna kundi la wanawake wamekuwa wakiingiza chakula kutoka majumbano kwao na kukiuza hivyo kuharibu soko lao la chakula.

Mwenyekiti wa Kamati ya Soko hilo, Ali Kibwana alisema mafunzo waliyopata kupitia EfG yamesaidia sana kupunguza vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia katika soko hilo na kila mtu anayebainika kujihusisha na vitendo hivyo amekuwa akiitwa na kukanywa na kama akiendelea kuwa mkaidi anachukuliwa hatua nyingine kwa kufuata kanuni na sheria.

Kamanda wa Ulinzi na Mazingira wa Soko hilo, Nurdin Hassan amesema hali katika soko hilo ni nzuri kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na EfG ya kufanya semina na matamasha ya uhamasishaji hivyo kuifanyajamii kuelewa kuhusu vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.

Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa EfG, Shaban Rulimbiye alisema Shirika hilo linaendesha mradi wa miaka mitatu wa Mpe Riziki si Matusi wenye lengo la kutoa elimu ya kupinga ukatili wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na udhalilishaji na nia zaidi mradi huo ni kuusambaza hadi katika maeneo mengine ya nchi.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages