Breaking News

Your Ad Spot

Jan 27, 2016

JK AKABIDHI REPOTI YA JOPO LAKE KWA BAN KI MOON NAYE AMSHUKURU

Na  Mwandishi Maalum, New York
Mwenyekiti wa Jopo la  Ngazi ya juu kuhusu  Mwitikio wa Kimataifa wa   Majanga ya Kiafya, Rais Mstaafu, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete,  jana  Jumatatu, amemkabidhi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa    Ban ki  Moon,   Ripoti ya  Jopo lake.
Mhe. Jakaya  Kikwete aliteuliwa na  Ban Ki Moon, kuongoza Jopo lililokuwa na  wajumbe watano   mwezi  Aprili 2015.  kwa  mujibu wa hadidu za rejea Jopo hili lilitakiwa kutekeleza majukumu  yake   kuanzia mwezi Mei hadi Desemba 2015.
Akipokea  ripoti  hiyo,  katika hafla fupi iliyofanyika    Ofisini kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa  .  Ban Ki Moon,  pamoja na kumshukuru  Mwenyekiti wa Jopo  Mhe. Jakaya     Kikwete pamoja na  timu yake,  amesisitiza kwamba, mapendezo yaliyotolewa na  Jopo hilo   yatazingatiwa na kufanyiwa kazi.
“ Ninatoa   shukrani zangu za pekee na za dhati kwako wewe kama Mwenyekiti kwa uongozi wako , na pia kuwashukuru wajumbe uliofanya nao  kazi. Ripoti hii ambayo imesheheni mapendekezo na ushauri   itazingatiwa na kufanyiwa kazi”. Amesema Ban Ki  Moon
Akabanisha  kwamba,   mapendekeo  na ushauri  uliomo  ndani ya  Ripoti ya Jopo  atauwasilisha pia kwa  Shirika la Afya Duniani (  WHO).
Katibu Mkuu pia amesema  Ripoti hiyo itasaidia  sana  katika kutoa mwongozo kwa Jumuiya ya Kimataifa juu ya namna  ya kuimarisha na  kuboresha   miundombinu ya afya  ili iweze  kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
Vile vile Katibu Mkuu wa  Umoja wa  Mataifa amemhakikishia Mwenyekiti wa Jopo  Mhe. Jakaya Kikwete na  wajumbe wake  kwamba,   Ripoti hiyo  itawekwa hadharani mapema  iwezekanavyo ili  Nchi wanachama wa Umoja wa  Mataifa na makundi mbalimbali ya jamii waweze kuisoma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jopo,  Rais Mstaafu  Mhe. Jakaya  Mrisho Kikwete, amemshukuru  Katibu Mkuu  Ban  Ki Moon, kwa kumpatia heshima ya kuongoza  Jopo hilo, jopo ambalo amesema walifanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu.
Wajumbe  wengine  wa Jopo hilo walikuwa ni     Bw.    Celso Amorim ( Brazil), Micheline Calmy ( Switzerland), Marty Natalegawa  ( Indonesia) Joy Phumapi ( Botswana) na  Rajav Shah ( USA).
Jukumu  kubwa ya  jopo hilo  kwa mujibu wa hadidu za rejea,  pamoja na mambo mengine,  lilikuwa  ni kutoa mapendekezo ya  namna ya  kuimarisha mifumo  ya kitaifa na kimataifa katika   kuzuia na kukabiliana na  majanga ya kiafya yakiwamo magonjwa  ya mlipuko, ikiwa ni pamoja na  kujifunza   kuhusu   mwitikio wa Jumuiya ya Kimataifa kufuatia  kuibuka kwa   janga la ugonjwa wa Ebola.
Katika utekelezaji wa majukumu yake  Jopo  lilikutana  na kufanya majadiliano ya kina na makundi mbalimbali yakiwamo ya  wataalamu,   wawakilishi wa  nchi tatu ambazo  ziliathirika sana na ugonjwa wa Ebola (  Liberia,  Siera Leone na Guinea),Mashirika ya Kimataifa na Kikanda , Taasisi za Fedha za kimataifa, wahudumu wa Afya, Wasomi , Watafiti,  Sekta Binafsi na wataalam wa  fani  na kada mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages