Na. Ahmad Mmow, Kilwa-LINDI.
Uhifadhi
wa msitu katika kijiji cha Nanjirinji A, wilayani Kilwa mkoani Lindi,
umeendelea kuwanufaisha wananchi wakazi wa kijiji hicho baada ya kuanza
kuwapatia ruzuku akina mama wajawazito wanaoishi katika kijiji hicho.
Hayo
yameelezwa na mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Jafari Nyambate,
mwanzoni mwa wiki iliyopita alipozungumza na Lindiyetu.com mjini Kilwa
masoko.
Nyambate
alisema baada ya kutekeleza miradi mbalimbali ya jamii kwa kutumia fedha
zilizotokana na mauzo ya mazao ya msitu waliohifadhi, unaofahamika kwa
jina la Mbumbila, Kijiji kimeanza kuwapa ruzuku ya shilingi 30,000 akina
mama wajawazito wakazi wa kijiji hicho.
Ikiwa ni mchango wa maandalizi ya gharama za matibabu wakati wakujifungua.
“Fedha
hizo zinatolewa kwa mama ambaye mimba yake imefikisha umri wa miezi
tisa, muda ambao anatarajia kujifungua ili aweze kufanya maandalizi
ikiwamo kununua vifaa vitakavyotumika wakati huo,”alisema Nyambate.
Alibainisha
kuwa huo nimwendelezo wa huduma mbalimbali za jamii zilizotekelezwa
kutokana na mapato ya msitu huo. Ambapo baada ya kufanikiwa mpango
huo,wanajipanga kuanza kutoa ruzuku kwa wazee wasiojiweza.
Mwenyekiti
huyo aliitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kutokana na mapato ya
msitu huo kuwa ni vyumba vi 3 vya madarasa ya shule ya msingi, visima
vifupi 7 vya maji, soko, vyoo vya kudumu vya shule ya msingi vyenye
matundu 6.
Aliitaja
miradi mingine kuwa ni pamoja na nyumba moja ya mwalimu, madawati 26,
bomba la maji la shule na viti 100 vinavyotumika wakati wa mikutano
mikuu ya kijiji.
Hata
hivyo pamoja na mafanikio hayo, mwenyekiti huyo alisema wanakabiliwa na
changamoto mbalimbali. Ikiwamo uvamizi unaofanywa na wakulima, hasa wa
zao la ufuta ambao wanalazimisha kuendesha shughuli za kilimo ndani ya
msitu waliouhifadhi.
“Lakini
pia wapo wanaopasua mbao kwa njia haramu, nao wanatusumbua sana ila
tunakabiliana nao kwa kufanya doria za mara kwa mara, hasa baada ya
kamati ya maliasili kuwezeshwa pikipiki tatu zinazotumika kwa doria,”
aliongeza kusema.
Uvunaji katika msitu huo wenye hekta 61724, ulianza rasmi mwaka 2012.(P.T)
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269