Breaking News

Your Ad Spot

Jan 6, 2016

MSAADA WA MBUNGE ULIOKATALIWA -KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA AZUNGUMZIA

Msaada wa Mbunge uliokataliwa - Katibu Mkuu Wizara ya Afya azungumzia


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza na waandishi wa habari kuhusu watumishi wa wizara hiyo nchini kote kupokea misaada inayotolewa na taasisi mbalimbali na watu wenye moyo wa kusaidia jamii bila kujali itikadi za siasa au dini isipokuwa wahakikishe misaada hiyo inakidhi viwango vinavyotakiwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema misaada inayotolewa na watu mbalimbali kwa ajili ya kusaidia jamii ni lazima iwe imekidhi viwango vya ubora, hivyo haitakiwi kuangaliwa kwa vigezo vya dini, itikadi wala siasa.

Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake baada kituo kimojwapo nchini kukataa misaada iliyotolewa na Mbunge wa Bukoba Mjini (CHADEMA), Wilfred Lwakatare hivi karibuni.

Dkt. Ulisubisya alisema hivi karibuni gazeti moja la kila siku la hapa nchini liliripoti kwamba misaada iliyotolewa na Mbunge huyo, katika baadhi vituo afya Zahanati kwa ajili ya wajawazito kukataliwa.“Serikali ina sera ya kusaidia jamii hususan misaada inayotolewa kwenye huduma za afya, ambayo inakidhi viwango vya ubora kulingana Sheria , kanuni na taratibu za Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA),” alisema Katibu Mkuu huyo. 

Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari kiliripoti kwamba baadhi ya wakuu wa vituo vya afya na zahanati katika Manispaa ya Bukoba, wamegoma kupokea misaada kwa ajili ya wajawazito uliotolewa na kwa madai ya kupewa maelekezo na Serikali.Dkt. Ulisubisya aliwataka watendaji wa afya wa vituo hivyo kuwa wasiangalie misaada hiyo kwa misingi ya dini, itikadi na kisiasa. 

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo aliwataka watu mbalimbali wenye lengo la kutoa misaada katika vituo vya afya kuhakikisha kwamba imekidhi viwango viliyowekwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA). Katika hatua nyingine aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Donan Mmbando alikabidhi ofisi hiyo kwa Katibu Mkuu huyo mpya.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akikabidhiwa nyaaraka muhimu na aliyekuwa katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk Donan Mmbando.(P.T)
Taarifa ya Magreth Kinabo – Maelezo
AWALIGAZETI LA MWANANCHI LILICHAPISHAHABARI IFUAFAYO...
Baadhi ya wakuu wa vituo vya afya na zahanati katika Manispaa ya Bukoba, wamegoma kupokea misaada kwa ajili ya wajawazito uliotolewa na Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare kwa madai ya kupewa maelekezo na Serikali. 

Mbunge huyo mwishoni mwa wiki alikuwa akisambaza vifaa tiba katika vituo vya afya na zahanati, lakini wasimamizi walikataa kuvipokea, huku wengine wakikimbia wakidai walipewa maelekezo na viongozi wao kutovipokea. 

Katika hali ya kushangaza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Richard Mihayo ambaye alikuwa katika msafara wa mbunge huyo alitoweka ghafla baada ya kufika Kituo cha Afya cha Zamzam, huku Kaimu mganga, Samwel Chaba akigoma kupokea vifaa hivyo. 

Baada ya mkurugenzi kutoweka, mbunge huyo alilazimika kutelekeza vifaa hivyo kituoni hapo na kwenda Zahanati ya Kashai ambako Kaimu Msimamizi wa zahanati hiyo, Emmanel Luviga alikubali kuvipokea. 

Katika Kituo cha Afya Rwamishenye vifaa hivyo vilipokewa na wauguzi waliogoma kuzungumza suala lolote. 

Baada ya kufika Zahanati ya Kagemu, Msimamizi wake Glory Sailo aligoma kupokea vifaa kwa ajili ya mama wajawazito kwa madai ni maelekezo ya viongozi. 

Hatua ya viongozi kuweka vikwazo kwenye upokeaji wa vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh3 milioni ililalamikiwa na Lwakatare aliyedai aliandika barua manispaa na kutoa nakala hadi ngazi ya mkoa, lakini Mganga Mkuu wa manispaa hiyo, Dk Hamza Mgula alisema hajui lolote kuhusu suala hilo. 

Akizungumzia suala hilo, Mihayo alisema kwa kawaida vifaa vya tiba ni lazima vikaguliwe na mganga mkuu wa manispaa ili kuthibitisha ubora, hivyo haviwezi kupelekwa bila kuthibitishwa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages