Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki (Mb)
akisalimiana na watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
alipoitembelea ofisi hiyo mapema leo jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Salome S.Kaganda (kushoto) akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alipotembelea ofisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Picha na Avila Kakingo wa Globu ya Jamii.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora , Angela
Kairuki amewataka watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma kuzingatia viapo vyao na kufuata sheria, kanuni na taratibu wakati
wa kutekeleza majukumu yao.
Mhe. Waziri Kairuki amesema hayo alipotembelea ofisi za Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kukukutana na menejimenti na baadhi ya
watumishi wa ofisi hiyo jijini Dar es salaam leo.
“Nimekuja hapa kujionea na kujifunza juu ya taasisi yenu, nataka
mfanye kazi msikiuke taratibu na sheria kwakuwa tu mna nafasi ya kuwa
katika ofisi hii, mna jukumu la kuhakikisha mnatekeleza majukumu yenu
kwa kuzingatia sheria, taratibu na viapo mlivyokula,”alisema mhe.
Waziri
Aidha ameitaka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
kuhakikisha jukumu la utoaji wa elimu ya maadili kwa umma linatiliwa
mkazo kwani kufanya hivyo kutahamasisha maadili nchini na hivyo kufanya
viwango vya juu vya maadili vinazingatiwa na kuongeza kuwa hali hiyo
itawezesha viongozi kutenda haki, kuwa na matumizi mazuri ya rasilimali
za umma na kuwa na huruma kwa wananchi.
Mhe Waziri pia ameongelea kutokuridhishwa na mienendo ya viongozi wa
umma baada ya kuacha utumishi ambayo haiendani na viapo walivyoapa
wakati wakiingia katika nafasi zao na ameitaka Sekretarieti ya Maadili
ya Viongozi wa Umma kuangalia namna ambavyo jambo hilo linavyoweza
kudhibitiwa na hivyo kuimarisha uwajibikaji wa pamoja.
Mhe. Kairuki alikuwa katika ziara zake za kutembelea taasisi zilizoko chini ya ofisi yake.


No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269