
Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya Maafa Zanzibar ndugu Ali Juma Hamad akifungua mafunzo ya waandishi wa habari juu ya kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu katika Ukumbi wa gereji ya Wizara ya Afya Mombasa Mjini Zanzibar, (kulia) daktari dhamana Kanda ya Unguja Dkt Fadhili Mohd na (kushoto) Mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt. Ghirmay. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.

Washiriki wa mafunzo hayo wakimsikiliza kwa makini Daktari dhamana Kanda ya Unguja Dkt. Fadhili Mohamed alipokuwa akielezea njia za kukabiliana na kipindupindu katika mafunzo ya siku moja yaliyofanyika Ukumbi wa Gereji ya Wizara ya Afya Mombasa Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Rafii Haji Mkame akiwasilisha mada ya wajibu wa waandishi wa habari katika kukabiliana na maradhi ya miripuko katika mafunzo yaliyofanyika Ukumbi wa Gereji ya Wizara ya Afya Mombasa Mjini Zanzibar.

Katibu wa Jumuiya ya Maafisa wa Afya Zanzibar Ahmed Suleiman Said akitoa elimu ya kupambana na maradhi ya kipindupindu kwa wananchi wa shehia ya Shaurimoyo Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.(P.T)

Baadhi ya
wananchi wa shehia ya Shaurimoyo Mjini Zanzibar wakifuatilia juu ya
elimu ya ugonjwa wa Kipindupindu iliyotolewa na Jumuiya ya Maafisa wa
Afya Zanzibar.Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Mwashungi Tahir – Maelezo Zanzibar.
Daktari
dhamana kanda ya Unguja Dkt. Fadhil Mohammed Abdallah amewataka
wananchi kuchukua tahadhari kuhusu maradhi ya kipindupindu ambayo kwa
sasa ni tishio kubwa Zanzibar.
Hayo
ameyasema katika Ukumbi wa Gereji ya Wizara ya Afya Mombasa kwenye
mafunzo ya waandishi wa habari juu ya kujikinga na ugonjwa huo ambao
bado unaendelea katika sehemu mbali mbali Zanzibar.
Amesisitiza
kuchukuliwa tahadhari zaidi kupambana na maradhi ya kipindu pindu
ikiwemo kuweka mazingira safi, kufuata masharti ya afya, kuchemsha
maji ya kunywa ama kutumia maji yaliyotiwa dawa ya kuulia bektiria
wanaosababisha maradhi hayo..
Dkt.
Fadhil amewataka wananchi kuacha tabia ya kula ovyo njiani, kukosha
matunda na mboga mboga kabla ya kula na kuchukua tahadhari kubwa wakati
wa kumshughulikia maiti ya maradhi ya kipindu pindu kwani ni miongoni
mwa njia za maambukizi ya maradhi hayo.
Amewataka
waandishi wa habari kutekeleza majuku yao ya kutoa elimu kwa wananchi
ili wapate uelewa mkubwa zaidi kukabiliana na maradhi hayo.
Amesema
maradhi ya kipindu pindu ingawa ni tishio kwa maisha ya wananchi lakini
ni rahisi zaidi kuyadhibiti kuliko maradhi mengine iwapo wananchi
watafuata masharti ya afya.
“Waandishi
wa habari mnao mchango mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii katika
kukabiliana na maradhi ya kipindupindu hivyo tunategemea mashirikiano
makubwa kutoka kwenu,” alisisitiza Dkt. Fadhili
Akifungua
mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya Maafa Zanzibar ndugu
Ali Juma Hamad amesema juhudi za pamoja zinahitajika katika
kukabiliana na kipindupindu na mchango wa kila mtu na taasisi
unahitajika.
Amesema
kumekuwa na changamoto kubwa katika kukabiliana na maradhi hayo tokea
yalipogundulika mwezi Septemba mwaka jana ikiwa ni kipindi cha jua
kali, kuchukua muda mrefu na kusambaa sehemu mbali mbali za Unguja na
Pemba kinyume na watu walivyozoea vipindi vya nyuma.
Akiwasilisha
mada ya majukumu ya vyombo vya Habari katika kudhibiti miripuko ya
maradhi ya kuambukiza, Mkurugenzi wa Idara y Habari Maelezo Zanzibar
Rafii Haji Makame amesema vyombo hiyo vinajukumu la lazima katika
kusaidia umma kudhibiti vifo na athari nyengine za kiuchumi na kijamii
zinazosababishwa na miripuko ya maradhi .
Katika
kufanikisha majukumu hayo Mkurugenzi Rafii ametaka kuongezwa ushirikiano
kati ya vyombo vya habari na sekta ya afya ili kupata taarifa sahihi
kwa wakati katika kufikisha ujumbe kwa umma.
Aidha
amesema utoaji wa elimu ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kupitia
vyombo vya habari liwe suala endelevu ili jamii iweze kupata uwelewa na
kubadilika kitabia.
Jumla ya
kambi 18 zilifunguliwa na kuhudumia wagonjwa 1066 Unguja na Pemba na
kati yao wagonjwa 22 walifariki. Hivi sasa kuna kambi nne tu
zinazoendelea kupokea wagonjwa katika kisiwa cha Unguja.
Wakati
huo huo Katibu wa Jumuiya ya maafisa wa afya Zanzibar Ahmed Suleiman
Saidi amewashauri wananchi wa shehia ya Shaurimoyo kubadili tabia na
kuweka mazingira wanayoishi katika hali ya usafi ili kujikinga na
kipindupindu.
Alitoa
ushauri huo alipokuwa akizungumza na wananchi wa shehia hiyo katika
skuli ya Shaurimoyo walipowatembelea kutoa taaluma juu yamaradhi hayo
kwa vile shehia hiyo ni miongozi kati ya shehia zilizoathirika na
kipindupindu.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269