Hapa ni katika viwanja vya
Shycom mjini Shinyanga ambapo April 05,2016 kumefanyika mkutano wa
mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga mheshimiwa Anne Kilango Malecela
amejitambulisha kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga na kueleza vipaumbele
vyake katika kuwaletea maendeleo wananchi.
……………………………………………………………
Mkutano
huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya
siasa,viongozi wa dini na kimila huku mamia ya wakazi wa Shinyanga
wakijitokeza kwa wingi kumsikiliza mkuu huyo wa mkoa.Akiwahutubia
wakazi wa Shinyanga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela
ambaye anakuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga wa 19 tangu nchi ipate uhuru na
mwanamke pekee kuongoza mkoa huo, amesema amekuja mkoani Shinyanga kwa
ajili ya kumsaidia rais John Pombe Magufuli kuwaletea maendeleo wananchi
kwa kutekeleza kauli mbiu ya Hapa Kazi tu.
Kilango amesema atahakikisha
tatizo la uhaba wa madawati katika shule za mkoa wa Shinyanga
linamalizika haraka iwezekanavyo huku akisisitiza nia yake ya kutaka
mkoa kushika nafasi ya kwanza mfululizo katika matokeo ya mitihani
mbalimbali kitaifa pamoja na kwamba tangu mwaka 2012 hadi 2015 mkoa
umekuwa ukishika nafasi ya kwanza na ya pili katika matokeo ya kidato
cha nne.
Mkuu huyo wa mkoa aliyepewa
jina la Mbula amepongeza viongozi wa mkoa kwa kupunguza kwa kiasi
kikubwa mauaji ya vikongwe na albino na kuhamasisha jamii kuachana na
mila na desturi zilizopitwa na wakati.
Katika hatua nyingine Kilango
ambaye amekuwa mbunge kwa kipindi cha miaka mitano amesema hatakuwa
kiongozi wa kukaa ofisini na badala yake atakuwa kiongozi
anayewatembelea wananchi ili kutatua matatizo yao.
“Nitatenga walau siku moja
kila wiki kuwatembelea wananchi katika mitaa na vijiji…watendaji wa
serikali walioko chini yangu, nataka kuanzia sasa iwe mwisho kunyanyasa
wananchi, naombeni msikilize kero zao badala ya kuwapa majibu ya ovyo
ovyo”, ameeleza Kilango.
“Zile shilingi milioni 50
alizoahidi mheshimiwa rais wakati wa kampeni za uchaguzi
zitaletwa,naomba mzitumie vizuri,nataka mkoa huu uwe wa mfano kwa
maendeleo,naombeni ushirikiano,naahidi kushirikiana kwa ukaribu pia na
viongozi wa dini,hawa ni watu muhimu sana”, ameongeza Kilango
Pamoja na mambo mengine wazee
wa kimila/machifu wa kabila la Kisukuma wamesimika mheshimiwa Kilango
kuwa chifu wa kisukama na wamemkabidhi dhana mbalimbali za kimila mkuu
huyo wa mkoa ili azitumie katika uongozi wake kuwaongoza wananchi wa
Shinyanga ambao wengi wao ni wasukuma.
Viongozi hao wa kimila pia
wamemtangaza mheshimiwa Anne Kilango Malecela kuwa “Kanumba” maana yake
mtendaji na msimamizi mkuu kwa mkoa na kumpa jina la Kimila “Mbula”
likiwa na maana ya mvua.
Mkuu huyo wa mkoa pia
ameombewa dua na viongozi wa dini waliohudhuria mkutano huo ambao
umefurahiwa na wakazi wengi wa mkoa wa Shinyanga waliodai kuwa haijawahi
kutokea mkuu wa mkoa akajitambulisha kwa wananchi mara tu anapoteuliwa
kushika nafasi hiyo.
“Mbula” ni jina kiongozi mkubwa wa kimila,Mbula alikuwa mganga wa 33 kati ya waganga 54 maarufu nchini Tanzania.
Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog, Kadama Malunde alikuwepo eneo la tukio ametuletea picha 22 angalia hapa chini
Machifu wa Kisukuma na
wasaidizi wa machifu kutoka maeneo mbali mbali ya mkoa wa Shinyanga
wakijitambulisha kwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga mheshimiwa Anne Kilango
Malecela ambaye amepewa jina la “Mbula”
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269