Wanapiganaji 20 wa ash-Shabab wauawa na jeshi la Somalia
Wapiganaji wa kundi la kigaidi na kitakfiri la ash-Shabab nchini
Somalia wameuawa na askari wa serikali, kaskazini mwa nchi hiyo.
Ismail Khalifah Shira, kamanda wa jeshi la Somalia amethibitisha
habari hiyo mapema leo na kuongeza kuwa, wanachama wa kundi hilo la
kigaidi la ash-Shabab, wameuawa asubuhi ya leo katika eneo la Dainunay,
lililopo karibu na mji wa Baidoa. Shira ameongeza kuwa, magaidi hao
wameuawa baada ya kuvamia kambi ya jeshi la serikali katika eneo hilo
kwa lengo la kutekeleza shambulizi la kushtukiza, na kwamba jaribio lao
lilifeli baada ya askari kufahamu mapema njama hiyo na kuwaua magaidi
hao katika eneo la tukio. Hata hivyo kamanda Ismail Khalifah Shira
hakutaja hasara yoyote iliyopata jeshi katika hujuma hiyo. Hii ni katika
hali ambayo kundi la ash-Shabab limedai kupata ushindi katika hujuma
hiyo. Ripoti iliyotolewa na kundi hilo maarufu kwa kutenda jinai dhidi
ya binaadamu, imedai kuwa wapiganaji wa ash-Shabab wamefanikiwa pia
kudhibiti kambi ya kijeshi la eneo hilo la Dainunay. Aidha limeongeza
kuwa, katika hujuma hiyo askari 10 wa serikali wameuawa.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269