Breaking News

Your Ad Spot

May 23, 2016

WITO WA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA WA KUONGEZWA MISAADA YA KIBINADAMU

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema umoja huo unawataka viongozi wa nchi duniani kutekeleza ahadi zao za kuongeza michango yao kwa watu wanaohitaji misaada.
Ban Ki-moon ametoa wito huo sambamba na kukaribia kufanyika mkutano wa kimataifa wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa huko nchini Uturuki. Amesema nchi za dunia zinapaswa kuwasaidia watu wanaohitajia misaada na kwamba Umoja wa Mataifa unahitaji kupata ahadi ya hakikisho la viongozi wa nchi hizo ya kutekeleza suala hilo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameashiria mapigano ya utumiaji silaha na mabalaa ya kimaumbile yanayotokea duniani na kueleza kwamba watu wasiopungua milioni 130 wanahitaji misaada ya kibinadamu ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku. Ban aidha ameongeza kuwa milioni 60 kati yao ni watu waliopoteza nyumba na makazi yao.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa idadi ya watu wanaohitaji misaada inaongezeka, na umoja huo hauna uwezo wa kudhamini mahitaji yao.
Maelezo hayo ya Ban Ki-moon yanatolewa katika hali ambayo vita na umwagaji damu katika maeneo mengi ya dunia yakiwemo ya Asia na Afrika yamewafanya watu wengi walazimike kuhama na kuwa wakimbizi katika nchi na maeneo mengine na kuishi katika hali na mazingira mabaya kabisa ya kibinadamu kwenye kambi na maeneo ya mipakani.
Vita katika maeneo mengi ya Afrika ikiwemo Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati na mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi kama Zimbabwe na Ethiopia yamesababisha ukame mkubwa na kuteketeza mazao ya kilimo.
Kwa mujibu wa duru za habari barani Afrika zaidi ya watu 50 wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa kwa sababu mazao ya kilimo yamepungua tena.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo hivi sasa kuna watu wanaokadiriwa kufika milioni 31 barani humo ambao wanahitaji chakula, na ifikapo mwaka ujao wa 2017, watu wengine milioni 20 wataishiwa na akiba yao ya chakula na kutokuwa na chochote cha kukila.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa watu milioni 10 nchini Ethiopia, milioni sita nchini Sudan Kusini na wengine milioni tano katika nchi ya Yemen watakabiliwa na baa la njaa katika mwaka ujao kutokana na kufurika maji na ukame.
Aidha mabadiliko makubwa ya hali ya hewa yaliyotokea mashariki na kusini mwa Afrika yamesababisha watoto wadogo milioni moja kukumbwa na hali mbaya ya utapiamlo na kuwaacha pia watu wapatao milioni 32 wakiwa hawana chakula cha kutosha.
Kitambo si kirefu nyuma, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) lilitangaza kuwa linatiwa wasiwasi na hali isiyoridhisha ya maelfu ya wakimbizi Wanigeria ambao wamelazimika kuzihama nyumba na makazi yao kwa kuhofia mashambulio ya kundi la Boko Haram.
Taarifa iliyotolewa na shirika hilo la kimataifa imeeleza kuwa kushtadi mashambulio ya kundi la Boko Haram katika maeneo mengi ya Nigeria kumesababisha mamilioni ya raia wa nchi hiyo kubaki bila makazi. Hali iko vivo hivyo pia katika eneo la Ziwa Chad.
Na hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Mpango wa Chakula Duniani hakuna chakula cha kutosha na cha kuridhisha katika kambi za wakimbizi na kwamba uhaba mkubwa wa chakula unasababisha wakimbizi hao kugombania na kupigania chakula kwa ajili ya kuokoa maisha yao.
Kwa mujibu wa ripoti ya ofisi ya uratibu wa masuala ya huduma za kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu elfu 69 kutoka Sudan Kusini nao pia wamezihama nyumba na makazi yao kutokana na mapigano na kukosa uhakika wa kupata chakula na kujitafutia makazi katika maeneo kadhaa ya nchi jirani ya Sudan ikiwemo mikoa ya Darfur Mashariki, Darfur Kusini na Kordofan Magharibi. Wakimbizi hao wanahitaji misaada ya haraka ya chakula na dawa.
Hayo yote yanajiri huku viongozi wa nchi za Afrika wakitoa wito wa kutengwa bajeti ya dola bilioni moja na milioni 500 ili kutatua tatizo la uhaba wa chakula linalowakabili wananchi wao. Hata hivyo mashirika na nchi watoaji misaada hiyo ya chakula zimeahidi kuchangia asilimia 25 tu ya bajeti hiyo.../

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages