ACP Advera J. Bulimba msemaji wa Polisi |
Uzinduzi
huo utafanyika siku ya Jumamosi, tarehe 25 Juni, 2016 katika viwanja
vya Biafra, Kinondoni Dar es Salaam, kuanzia saa tatu asubuhi, ambapo
Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mhe. Dr
John Joseph Pombe Magufuli. Sambamba na uzinduzi huo wa mpango, Mhe.
Rais ataanza kuzindua kituo cha Mawasiliano ya simu za dharura za Polisi
111, na 112 (Police Call Centre) na kituo cha Polisi cha kuhamishika
kilichopo maeneo ya Coco beach mkabala na jengo la Coco Plaza, ambacho
ni miongoni mwa vituo 13 vitakavyowekwa kwenye maeneo tete kiuhalifu
yaliyoainishwa katika mkoa wa kipolisi wa Kinondoni.
Lengo la
Mpango huu ni kuimarisha usalama wa wananchi katika jamii na mali zao.
Huu ni ubunifu wa Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu yake ambapo
Jeshi la Polisi limeamua kuondokana na utendaji wa kimazoea kwa
kuanzisha mikakati mikuu minne ambayo ni kuongeza ufanisi katika
shughuli za kipolisi, kuongeza ubora katika utoaji wa huduma za
kipolisi, kuimarisha mawasiliano na ushiriki wa wadau pamoja na kubuni
vyanzo mbalimbali katika kutafuta rasilimali fedha.
Kupitia
mikakati hiyo, Jeshi la Polisi litaanzisha mpangilio mpya wa ulinzi na
doria katika maeneo yaliyokithiri kwa uhalifu, litaboresha Vituo vya
Polisi kuwa katika muonekano bora na wa aina moja nchi nzima,
litaimarisha ubia na sekta binafsi za ulinzi, litaongeza uharaka wa
kufika kwenye matukio ya uhalifu yanayoripotiwa, litaimarisha na
kudumisha misingi ya maadili, litaweka mifumo thabiti ya kusimamia
rasilimali watu, litaimarisha mawasiliano ya ndani na nje ya Jeshi, na
mwisho litatafuta vyanzo mbadala vya fedha zinazohitajika ili
kuliwezesha Jeshi la Polisi kutekeleza wajibu wake. Vyanzo mbadala
vitaongeza wigo wa kutafuta rasilimali fedha kutokana na ufinyu wa
Bajeti ya Serikali ambayo Jeshi la Polisi limekuwa likipata kila mwaka.
Aidha,
uzinduzi huo utasindikizwa na Wasanii mbalimbali wa Muziki wakiwemo,
Bendi ya Polisi, ya Moto Band, Manfongo, Ndolela, Man Prince pamoja na
wasanii wengine na burudani mbalimbali zitakuwepo.
Wananchi
wote kwa ujumla wanakaribishwa ili kupata maelezo ya kina na uelewa
juu ya mkakati huu mpya wa kimageuzi ulioandaliwa kwa kushirikiana na
Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (President’s Delivery
Bureau-PDB) inayoratibu Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Asanteni .
Imetolewa na:
Advera J. Bulimba – Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269