Breaking News

Your Ad Spot

Jul 26, 2016

DK.KIKWETE :NI NGUMU VYAMA VYA UPINZANI KUSHINDA CHAGUZI ZIJAZO

Rais Mstaafu Dkt Jakaya Kikwete,akizungumza na wanaCCM Bagamoyo mkoani Pwani,katika sherehe za kumkaribisha nyumbani.
Mwenyekiti mstaafu wa chama cha mapinduzi (CCM)dk.Jakaya Kikwete akipewa zawadi na baadhi ya wazee wa wilayani Bagamoyo, kwenye sherehe  za kumpokea na kumkaribisha nyumbani baada ya kumaliza muda wake wa uongozi wa chama,sherehe  zilizofanyika ukumbi wa chuo cha sanaa  (TASUBA).(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
MWENYEKITI mstaafu wa chama cha mapinduzi (CCM),Dkt Jakaya Kikwete amesema ni ndoto vyama vya upinzani kushinda katika chaguzi kuu zijazo kutokana na chama tawala kuwa imara na kujidhatiti katika kutekeleza ilani yake na kuwatumikia wananchi.
Aidha amesema anaimani nchi itaendelea kuwa na maendeleo makubwa na kuinua uchumi kutokana na kasi aliyonayo rais John Magufuli.

Sambamba na hayo dk.Kikwete ameeleza kuwa kwasasa anahitaji kupumzika na atakuwa anajishughulisha kilimo na ufugaji ambapo hayupo tayari kutoa ushauri wa mambo ya kiserikali na chama kwani kazi hiyo ina wenyewe na wanatosha.
Dkt Kikwete alisema anashukuru mungu kipindi chake ameongoza na kuiacha nchi ikiwa na utulivu mkubwa licha ya uchaguzi mkuu uliopita kupitia kwenye kipindi kigumu.
Aliyasema hayo jana majira ya jioni huko mjini Bagamoyo kwenye ukumbi wa chuo cha sanaa (TASUBA)wakati wa sherehe za kumkaribisha baada ya kustaafu na kumkabidhi nafasi ya uenyekiti dk.John Magufuli.

“Namshukuru mungu  nchi iko salama na chama kiko imara nami kwa sasa nataka  nipumzike sitajihusisha na masuala ya kisiasa ama kiserikali nataka nipumzike badala yake nitajikita katika shughuli za kijamii ikiwemo kufuga na kilimo”

“Mkija kufuata ushauri pale mtakapohitaji ,lakini naomba mkija mje kwa ajili ya suala la maendeleo nitakuwa tayari na sio kwa suala la kutoa ushauri kuhusu serikali hapana kwani kwa sasa kuna viongozi ambao wanauwezo na nawaamini kwa kiasi kikubwa”alisema Kikwete. 
Dkt Kikwete hakuna kitu kilichokuwa kikimpa wakati mgumu kama chama ama serikali kushindwa kufanikiwa malengo yake kwenye uongozi wake.
Alisema hali ya kushindwa ilikuwa ikimpa wakati mgumu na kujiona endapo angeshindwa basi angewaangusha Wanabagamoyo na Pwani nzima.

Dkt Kikwete alieleza kwamba anamshukuru mungu katika uongozi wake aliweza kufanya kazi na kuleta maendeleo makubwa na kuiacha nchi mahali pazuri na salama huku ikiwa imetulia.
Aliwataka watanzania kumuombea na kumuunga mkono rais dk. John Magufuli ili aweze kuleta maendeleo .
Awali wabunge wa mkoa huo wakiongozwa na mbunge wa jimbo la Bagamoyo dk Shukuru Kawambwa alisema wataendelea kumuenzi Kikwete kwa kujenga mnara wa kumbukumbu kwenye ofisi ya CCM mkoani Pwani.
Alisema kuwa ujenzi huo utaanza mara moja na watamwalika kuuzindua utakapokamilika ili iwe kielelezo kwa wabunge na kumbukumbu ya kizazi kijacho.
Dk .Kawambwa alisema baada ya kung'atuka mwenyekiti huyo mstaafu wataendelea kuchota hekima na burasa zake zilizomfanikisha kukiongoza chama hicho na serikali kwa kipindi cha miaka 10.

Kwa upande wake katibu wa CCM mkoani Pwani Joyce Masunga alieleza mkoa unampongeza kwa kuiongoza nchi na kuiletea mafanikio makubwa . 

Nae mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo ,Maskuzi alisema dk Kikwete alifanikiwa kuleta maendeleo makubwa kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu na mpango wa shule za kata ambao mpango huo umeonyesha mafanikio kwa mwaka huu kuongoza kwenye matokeo.
Alisema eneo jingine la kujivunia ni nishati ya umeme ambayo ni moja ya mafanikio kupitia mpango wa umeme vijijini( REA) na miundombinu ya madaraja makubwa ,vivuko,viwanja vya ndege na barabara kwa kiwango cha lami.

Sauti ya Rais Mstaafu Dkt Jakaya Kikwete akizungumza na wana Bagamoyo Mkoani Pwani.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages