Breaking News

Your Ad Spot

Aug 26, 2016

CCM YAOMBOLEZA VIFO VYA POLISI WALIOUAWA NA MAJAMBAZI, SENDEKA AIVAA CHADEMA, AMJIBU TUNDULISU

Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka akizungumzaa Waandishi wa Habari, kufafanua masuala mbalimbali, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba Jijini Dar es Salaam. Ifuatayo ni Taarifa rasmi Kama ilivyosomwa na Sendeka wakati wa kikao hicho na waandishi wa Habari.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 Ndugu wanahabari,
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa sana taarifa ya kushambuliwa na kuuawa kwa askari wa jeshi la Polisi wakiwa katika kutekeleza majukumu yao ya ulinzi eneo la Mbande, Temeke jijini Dar Es Salaam.

CCM tayari imemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Ernest Mangu pamoja na familia za marehemu waliofikwa na umauti katika tukio hilo baya katika historia ya nchi yetu.

Tunalaani tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kuvipa ushirikiano wa kutosha vyombo vya dola ili kufanikisha wahusika wa tukio hilo kusakwa popote pale na kupatikana ili wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria haraka.

Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itaendelea  kuhakikisha amani ya Taifa letu inalindwa dhidi ya wachache wanaofurahia madhila kwa wananchi wetu. Wananchi wetu wanapenda, wamezoea na wanastahili amani. Ndio maana Tanzania imekuwa nchi ya kupigiwa mfano, ikionesha uongozi katika maeneo mengi. Tuendelee kuilinda taswira hii.
  
MAFANIKIO YA AWAMU YA TANO
Ndugu wanahabari,
CCM inachukua nafasi hii kumpongeza Rais Mhe Dkt John Pombe Magufuli na Serikali yake kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika muda mfupi wa uongozi wake.
Rais Magufuli aliahidi mabadiliko. Tunampongeza kwa kusimamia vema utekelezaji wa ilani ya CCM. Katika muda mfupi wa miezi tisa tu, Rais Dk Magufuli amefanya mambo makubwa.
Sote tunafahamu kuwa Shirika letu la Ndege, ATCL, limekuwa linafanya kazi na ndege moja. Serikali ya Dk Magufuli imekwisha lipia ndege tatu za abiria toka Canada, ndege mbili zitaingiza nchini mwezi ujao.
Reli ya kati inajengwa kwa kiwango cha Standard Gauge. Meli katika ziwa viktoria inanunuliwa ktk bajeti ya mwaka huu. Elimu ya msingi na sekondari inatolewa bure. Wanafunzi wetu sasa wanakalia madawati na kujifunza vizuri zaidi. Barabara zimeendelea kujengwa. Makusanyo ya kodi yameongezeka. Huduma za jamii zinaendelea kuimarika. Lakini pia, nidhamu katika utumishi wa umma sasa imeimarika. Wananchi wanastahili huduma nzuri na kuthaminiwa na wafanyakazi wa Umma.
Mataifa mengi ya Afrika na nje ya Afrika yanaiga mbinu za Rais wetu katika kuleta mabadiliko nchini mwao. Hapa Kenya tu, Waziri mmoja wa Elimu anayesifika kwa utendaji kazi mzuri, anajiita “MAGUFULI.” Hata Australia, baadhi ya wananchi waliwahi kumtaka Waziri Mkuu wao afanye kazi kama Dk Magufuli.
Dk. Magufuli ameazimia kujenga uchumi wa viwanda. Ifikapo mwaka 2025, Tanzania itakuwa nchi yenye uchumi wa kati. Maisha ya wananchi wetu yataboreka. Vijana wetu wapate ajira katika viwanda, watauza malighali na mahitaji mbalimbali ya viwanda. Wakulima watapata masoko ya bidhaa zao katika viwanda hivyo. Kilimo kitaongezeka thamani kutokana na mahitaji mbalimbali ya viwanda vyetu.  Hatua za kuelekea huko tayari zimechukuliwa.
Wapo wachache wanaelekea kutafuta mbinu chafu za kuhujumu mafanikio haya, lakini hawatafanikiwa. Watanzania wamemchagua Dk Magufuli ili awaletee maendeleo.   
Serikali ya CCM, itawasaidia vijana wa Tanzania kuendesha uongozi wa Taifa lao. Kamwe tusikubali ndoto ya kuongoza mapinduzi haya makubwa kwa ajili ya Taifa na Bara letu ikapokonywa na watu wachache wasiokuwa na dira ya kuliletea maendeleo Taifa letu. Tuwapuuze.

UPINZANI KUSUSIA VIKAO VYA BUNGE
Ndugu Wanahabari,
Bunge kama ilivyo kwa mhimili mingine linaongozwa kwa katiba, sheria na kanuni katika mijadala na maamuzi yake. Kama Mbunge hajaridhika na maamuzi ya Spika, Naibu Spika au Mwenyeki wa kikao, kuna taratibu za kufuata. Utaratibu wa kikanuni ni kuulalamikia uamuzi huo kwa Katibu wa Bunge. Wakiwa wanafahamu taratibu za kikanuni, kama kawaida yao, WAPINZANI, waliamua kuzisigina na badala yake wakataka Naibu Spika aondolewe.
Hivyo wakaratibu kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Naibu Spika. Ambapo suala hilo lilipelekwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Kutokana na kutokuwepo kwa Spika nchini, hoja hiyo haikufikia ukomo. Tunamshukuru Mungu afya ya Spika imeimarika. Sasa hoja hiyo huenda itafikishwa katika mkutano wa Bunge litakalokaa mwezi ujao.
Kana kwamba hiyo haitoshi, kama kawaida yao, hawakuwa na subira ya kufuata taratibu. Wakaamua kufanya kihoja. Wakaamua kutohudhuria vikao vyote vya Bunge vilivyokuwa vikiongozwa na Naibu Spika.

Na hata walipoingia Bungeni waliziba midomo yao na kuamua kutowasalimia wabunge wenzao wa CCM, kutopeana mikono na hata kutohudhuria misiba na sherehe zao. Vitendo vyao hivi ndivyo vimeasisi chuki ndani ya jamii yetu iliyozoea UPENDO, UDUGU, UMOJA NA MSHIKAMANO. Watanzania tunafahamika na tunaona fahari kuishi kama ndugu.

Baada ya kitendo hicho cha kuwasaliti wapigakura wao kulaaniwa kila kona ya nchi, sasa wamekubali kutumiwa kama vibaraka kuichafua taswira ya nchi yetu, nao kwa hila iliyo wazi, wamekubali kuwafitinisha watanzania kwa kuandaa maandamano ya nchi nzima, yasiyo na ukomo. Hatua hii ni uvunjaji wa katiba ya nchi, Sheria na inalenga kuvunja amani, utulivu na mshikamano wa watu wetu.
Ileleweke kwamba, wanachokifanya hawa CHADEMA ni kuchochea wananchi kwa makusudi kutotii maagizo halali ya vyombo vya dola na Serikali kwa visingizio mufilisi kuwa katika Katiba imewapa uhuru huo. Katika haitoi haki na uhuru usio na ukomo. Ibara ya 29 (5) inasema;
       “Ila watu wote waweze kufaidi haki na uhuru vinavyotajwa na katiba hii kila mtu ana wajibu wa kutenda na kuendesha shughuli zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma”
Baada ya kusema hayo, ninaomba CHADEMA wakumbuke na kutilia maanani kuwa kila haki ina wajibu na hakuna haki au uhuru usiokuwa na ukomo hususani pale inaposababisha kuingiliwa ama kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine. Rejea ibara ya 30 (1) na (2) ya Katiba.

Ndugu wahabahari,
Mwisho tunatoa pole kwa wenzetu wa CUF kutokana na mapambano huko kwao. Tumestushwa sana na yanayoendelea huko. CCM inawapa pole na tunawatakia maelewano ili waje tusaidiane kuwaletea watanzania maendeleo.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.

Top of Form
Bottom of Form

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages