Breaking News

Your Ad Spot

Aug 22, 2016

KUAHIRISHWA UCHAGUZI WA RAIS NCHINI JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO

Tume ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imetangaza kuahirishwa uchaguzi wa rais nchini humo hadi mwezi Julai 2017.

Habari hiyo ilitangazwa, Agosti  20, 2016 na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kongo, Corneille Nangaa na kuongeza kuwa, shughuli ya uandikishaji majina ya wapiga kura iliyoanza mwezi Machi mwaka huu, itahitajia muda wa miezi 16 hadi kukamilika. Awali mahakama ya juu ya Jamhuri ya Kidokrasia ya Congo ilitangaza kuwa iwapo serikali ya Rais Joseph Kabila haitaweza kuanda uchaguzi wa rais katika wakati ulioainishwa basi kiongozi huyo anaweza kubakia madarakani hadi wakati wa kufanyika uchaguzi mkuu. Kabila alishika hatamu za kuiongoza Congo mwaka 2001 baada ya mauaji ya baba yake, Laurent Kabila, na kisha akashinda uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka 2006. Kwa mujibu  wa katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rais Joseph Kabila haruhusiwi kugombea tena kiti hicho baada ya kuhudumia vipindi viwili vya miaka mitano mitano.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Migogoro ya kisiasa imekuwa ikishuhudiwa nchini humo kwa muda sasa. Kabla ya hapo viongozi wa chama tawala walikuwa wametangaza kuwepo uwezekano wa kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais kutokana na upungufu wa bajeti na kadhalika kuchelewa shughuli ya uandikishaji wa majina ya wapiga kura, suala ambalo lilibua wimbi la malalamiko ya wapinzani nchini. Wapinzani wanamtuhumu Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwamba amechelewesha zoezi hilo kwa lengo la kusalia zaidi madarakani. Kabla ya hapo Etienne Tshisekedi, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani kinachoitwa 'Umoja kwa ajili ya Demokrasia na Maendeleo ya Kijamii' (UDPS) alimtaka rais huyo kung'atuke madarakani na kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi mkuu kufikia mwishoni mwa mwaka huu. Kadhalika mzee Tshisekedi alimtaka rais huyo kuondoka madarakani tarehe 20 Disemba mwaka huu kama ilivyopangwa, hatua ambayo ingetanguliwa na uchaguzi wa rais.

Edem Kodjo, Waziri Mkuu wa zamani wa Togo na mpatanishi wa AU Kongo DR
Mwanasiasa huyo aliitaja hatua ya kuahirisha uchaguzi kuwa ni uhaini mkubwa huku akimuonya Rais Kabila kunako kujaribu kugombea muhula wa tatu kwenye uchaguzi ujao. Licha ya kwamba wiki chache zilizopita kulikuwa kumepangwa kufanyika mazungumzo ya kitaifa kati ya wapinzani na chama tawala kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi  mgogoro wa kisiasa nchini humo, hata hivyo ghafla na katika hali ambayo haikutarajiwa mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mazungumzo hayo ameibuka na kutangaza kuahirishwa kwake. Edem Kodjo, Waziri Mkuu wa zamani wa Togo na mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mazungumzo ya umoja wa kitaifa nchini Kongo DR, ametangaza kuwa kuahirishwa mazungumzo hayo, kumetokana na pande husika kutokuwa na maandalizi kamili ya ushiriki wao kwenye mazungumzo. Kodjo ameongeza kuwa, mazungumzo ya kitaifa ndiyo njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo kwa maslahi ya taifa.

Mzee Etienne Tshisekedi, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha UDPS
Pamoja na hayo wapinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hawakuwa tayari kushiriki mazungumzo hayo. Kuachiliwa huru wafungwa wote wa kisiasa kutoka jela za serikali, lilikuwa sharti la wapinzani kwa ajili ya kushiriki katika mazungumzo hayo na serikali ya Rais Joseph Kabila. Kufuatia uamuzi wa kuahirishwa uchaguzi wa rais, Jumamosi ya jana muungano wa vyama vya upinzani ulitangaza rasmi upinzani wake wa kufanya mazungumzo na Rais Joseph Kabila kuhusiana na suala zima la uchaguzi. Aidha umoja huo umetangaza mgomo wa nchi nzima hapo siku ya Jumanne katika kulalamikia suala hilo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages