.

BAN KI MOON AISIHI TANZANIA KUTOCHOKA KUZISAIDIA NCHI ZENYE MIGOGORO

Sep 22, 2016

Katibu Mkuu Ban Ki Moon akiwa 
Waziri wa Mambo ya Nje na 
Ushirikiano wa Afrika  Mashariki
Dk.Augutine Mahiga ambaye 
anamwakilisha Rais John Magufuli
katika Mkutano wa 71 wa Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa
Na  Mwandishi Maalum, New  York
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban  Ki Moon,  ameitaka  Tanzania kuendelea na  kazi nzuri ya  usuluhishi wa  migogoro   katika baadhi ya nchi za Maziwa Makuu.

Ban Ki Moon ametoa wito huo jana   ( jumatano) wakati alipokutana  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Augustine Mahiga, ambaye  anamwakilisha  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  katika mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea hapa Jijini New  York, Marekani.

Katika  mazungumzo hayo Mkuu  huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, Tanzania ni kutovu cha Amani, usalama na demokrasia, na  kutokana na sifa hizo   Tanzania, inapashwa kuendelea na juhudi zake za kuzisaidia nchi zenye  migogoro.


Akazitaja nchi hizo  kuwa ni Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi na Sudani ya  Kusini ambayo ameitaja kuwa  ipo katika kipindi kigumu sana.

“ Ninawashukuru sana  viongozi  wa  Serikali ya  Tanzania kwa kazi nzuri ya  utafutaji wa Amani katika nchi  zenye matatizo,  Sudani ya Kusini ni nchi ambayo inatupa  mashaka makubwa. Rais asaidie katika kurejesha  hali ya utulivu.Tanzania ni  nchi kubwa kwa hiyo bado  ninaendelea kuitumainia.”  akasisitiza Ban Ki Moon.

Vile vile  Katibu Mkuu  Ban Ki Moon  ametoa pia  shukrani wa  ushiriki wa Tanzania katika  operesheni za ulinzi wa Amani na kazi  na  weledi mkubwa unaoonyeshwa  na wanajeshi wa Tanzania.
Akatumia fursa hii kuishukuru Tanzania  na viongozi  wake kwa  mchango wao mkubwa uliofanikisha   yeye kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Na  akatoa pole  zake kwa serikali na kwa watanzania baada ya kupata taarifa   kuhusu tetemeko la ardhi lililosababisha  vifo na   uharibifu wa  mali.

“Naishukuru sana Tanzania,  namshukuru Rais Mstaafu Jakaya Kiwete na wewe ( Waziri) na  viongozi wengine,  mlichangia sana kwangu mimi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Ninawashukuru sana sana.
” .
Katibu Mkuu  Ban Ki Moon anamaliza kipindi chake cha uongozi  cha  miaka kumi  mwishoni wa  Mwaka huu.Na tayari  mchakato wa  upigaji kura wakumtafuta mrithi wake unaendelea   katika Baraza  la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake,  akiwasilisha salamau za Rais  John Pombe Magufuli, Waziri  Mahiga amesema.  “  Ninawasilisha  salamu za Mhe.  Rais,  alipenda sana kuhudhuria mkutano huu wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  kwa  bahati mbaya ilimbidi  kuahirisha  safari yake kutokana na  tetemeko la ardhi lililotokea  hivi karibu  nchini kwetu ”.

Aidha  Waziri Mahinga ametumia pia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza   Katibu Mkuu kwa utekelezaji wa kutukuka wa majukumu yake  katika kipindi cha miaka  kumi ya uongozi wake.

“Kwa niaba ya serikali ya Tanzania  nikupongeza kwa   utekeleaji wa majukumu yake. Ulionyesha ushirikiano  wa karibu na Tanzania, ushirikiano uliokuwezesha kumteua Dkt. Asha-Rose Migiro kuwa  Naibu  Katibu Mkuu na msaidizi wako wa karibu. Lakini pia uliniteua mimi kuwa Mjumbe wako Maalum huko   Somalia  . Tanzania inashukuru kwa haya na mengine” akasema  Mahiga.

Aidha  amemwelezea  Katibu Mkuu  kama kiongozi ambaye aliifanya Afrika kuwa kipaumbele  chake, lakini pia aliibeba sana ajenda ya  wanawake jambo  ambalo  amesema limemjenga sifa kubwa.
Akizungumzia  kuhusu Tanzania  kuendelea  na juhudi za usuluhishi wa migogoro. Waziri amemhakikisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba, Tanzania na viongozi wake wataendelea na kujukumu hilo.


“Ni kuhakikishie kwamba Serikali yangu itendelea na jukumu hili la usuluhisi. Na kwa upande wa Burundi Tanzania, inaushukuru Umoja wa Mataifa,  kwa kutambua na kuamini  kwamba  Jumuiya ya  Afrika Mashariki inaweza kuushughulikia mgogoro huu.  Tanzania ambayo imekabidhiwa jukumu la uwezeshaji wa mazungumzo ya Amani inataka kufanya kazi kwa karibu na Umoja wa Mataifa  hivyo  misaada ya hali na mali kutoka  Idara za  Umoja wa Matifa  ni jambo  muhimu”.Amesisitiza  Waziri Mahiga. 

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª