Breaking News

Your Ad Spot

Sep 23, 2016

KIKWETE ATUNUKIWA TUZO YA UONGOZI WA KISIASA NA UTETEZI

 
Rais  Mstaafu Jakaya Kikwete  akipokea
Tuzo ya  Uongozi wa Kisiasa na  Utetezi
 kutoka kwa  Mkurugenzi Mtendaji wa
  Speak Up Afrika  Bi Kate  Campana,
  hafla iliyofanyika  Alhamis jana ,
  New York Marekani
Na  Mwandishi Maalum, New York
Shirika lisilo la  Kiserikali    la Speak  Up for Afrika    limemtunukia tuzo, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete kutokana na uongozi wake wa kisiasa na utetezi wake  kwa  makundi ya jamii yaliyo katika mazingira magumu hususani wanawake na watoto.

Utoaji wa  Tuzo hiyo  ya  uongozi wa kisiasa na utetezi , umekwenda sambamba na   hafla ya  miaka mitano ya kuanzishwa kwa  Taasisi ya Speak up  Afrika. Hafla  hiyo iliyofanyika jana Alhamisi Jijini New York   ilikuwa  pia  ni sehemu ya kuhamasisha uchangiaji   wa shughuli za  Taasisi hiyo.

Mchango ambao umetambuliwa na  Speak Up  Afrika,   taasisi ambayo imekuwa ikifanya kazi  kwa Karibu na Rais Mstaafu Kikwete, ni  katika maeneo ya  upelekaji na usambazaji wa huduma za msingi za afya hususani afya ya mama na mtoto,  udhibiti wa  ugonjwa  wa malaria kupitia kampeni  ya malaria haikubaliki ,usambazaji wa vyandarua  vyenye viatilifu, kampeni ya  lishe bora, na  kampeni ya   chanjo kwa watoto.

Pamoja  na  kutambua  juhudi za   Rais Mstaafu  Kikwete katika  kuyasemea maeneo hayo,  Taasisi hiyo kupitia  Mkurugenzi wake  Mtendaji Bi. Kate Campana pia imemtambua  kama kiongozi ambaye    amekuwa mstari wa mbele  wa kulisema Bara la Afrika kila  mara alipopata  fursa  ya  kufanya hivyo wakati akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu.

Rais kikwete ameelezwa katika hafla hiyo iliyowashirikisha  wadau wa kada mbalimbali, kama kiongozi wa kisiasa ambaye amezigusa nyoyo za watu wengi kujitolea kwaajili ya watu wenye mahitajio ya kupata huduma za msingi za kijamii ambazo  au wameshindwa kuzipata kutokana na kipato kidogo au haziwafikii kabisa.

Akipokea  Tuzo hiyo, Rais  Mstaafu Kikwete , amesema Tuzo hiyo ni ya watoto wote  waafrika ambao ndio  waliomfanya asimame   mbele ya wageni waalikwa.

“ Ni kwa sababu yenu ndio sababu nimetenga muda wangu  baada ya kustaafu kusukuma mbele agenda ya  kuboresha maisha yanu. Ninafanya hivyo kwasababu makuzi yangu yalikuwa kama  ya mtoto yeyote yule wa  kiafrika, nimeyaishi maisha  wanayo ishi. Na kwa hiyo ninaelewa fika  hamu na kiu yao ya kuwa  na maisha bora na afya njema”. Akasema Kikwete na kushangiliwa na wageni waalikwa.

Akaongeza kuwa  ,  mafaniko ambayo ameyapata katika  juhudi hizo  za kufikisha huduma za msingi  za kijamii kwa makundi  yenye mahitaji  yametokana na mambo mawili makubwa moja ni   aina ya uongozi  alioutumia kusukuma harakati hizo. Na pili  uhamasishaji uliofanyika katika  kupiga vita malaria kupitia Speak Up Afrika na    kampeni yao ya  malaria haikubaliki.

“ Nisingeweza kuyafanya niliyoyafanya   bila uungugwaji mkono na  ushirikiano  wa karibu nilioupata  na ninaoupata kutoka taasisi za kimataifa  ikiwamo hii ya  Speak Up  Afrika. Ndio maana  kwa mfano,  tumeweza kupunguza visa vya malaria kwa   theluthi mbilli,  tumefanikisha  upatikanaji wa chanjo kwa asilimia 96 kwa watoto wote na kupunguza vifo vitokanavyo na  malaria kwa   nusu.” Akaeleza Kikwete na kushangiliwa  tena.

Akasema, anamini katika ushirikiano na wadau mbalimbali  kama akina Ray Chambers kupitia kampeni ya  hakuna tena malaria, Taasisi ya  Bili na Melinda Gates na Gavi Vaccination   Alliance ambayo anashirikiano  nayo kwa karibu katika  kampeni ya chanjo kwa wote.

Rais  Mstaafu amewahakikishia   watendaji wa Speak  Up Afrika kwamba  ataendelea kufanya kazi nao kwa karibu  kutokana  kile alichosema amejionea mwenye kazi nzuri wanayoifana.

 Akawasihi  wadau mbalimbali  kuichangia taasisi hiyo  kwa kile alichosema, inafanya kazi kubwa  ya siyo tu kufikisha huduma za kijamii pale zinapotakiwa lakini  pia imekuwa ni kipaza sauti cha Afrika.

Wengine waliopewa Tuzo kwa kutambua michango yao kwa jamii ni  pamoja na   Professa Awa Marie Coll- Seck, Waziri wa Afya  wa Senegal, Bibi Toyin  Saraki,  mwanzilishi wa Taasisi ya  Wellbeing  Afrika ambayo  pia imekuwa ikitoa  elimu na misaada kwa wanawake na watoto pamoja na elimu  kwa wakunga na kutambua kazi nzuri, kubwa na ngumu  ya kuwahudumia wanawake wenzao wanapojifungua.  Na  Bwana Kabirou Mbodje ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa  Taasisi ya  Wari.

Taasisi ya  Speak  Up  Afrika  imeanzishwa  na wanawake na inaongozwa na wanawake. Ni taasisi ambayo imejijengea uweo na sifa kubwa ndani  ya kipindi cha miaka mitano tangu  kuanzishwa kwake.   

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages