Breaking News

Your Ad Spot

Sep 30, 2016

MAKAMU WA RAIS WA BARAZA LA TAIFA LA CUBA KUWASILI NCHINI OKTOBA 2, 2016

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba Nchini, Mhe.Salvador Antonio Valdes Mesa anayetarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 2 hadi 4 Septemba 2016.
Mhe. Waziri Mahiga akiendelea kuzungumza na Waandishi wa Habari kama wanavyoonekana pichani. =============================================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba nchini Tanzania
Makamu wa Rais wa Baraza la Taifa la Jamhuri ya Cuba, Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa anatarajiwa kuwasili nchini tarehe 02 Oktoba, 2016 kwa ziara rasmi ya siku tatu. Lengo la ziara hiyo ni kukuza na kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Cuba pamoja na kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano. Nchi nyingine anazotarajiwa kuzitembelea ni pamoja na Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Botswana na Zimbabwe.
Shughuli mbalimbali zitakazofanyika wakati wa ziara
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Valdes Mesa atapokelewa na mwenyeji wake Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tarehe 03 Oktoba, 2016 Mhe. Mesa atakutana kwa mazungumzo ya faragha na Mhe. Samia Suluhu Ikulu yakifuatiwa na mazungumzo rasmi kati yao na wajumbe waliofuatana nao.
Aidha, Mhe. Mesa atakutana kwa mazungumzo mafupi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli.
Baada ya mazungumzo hayo, Mhe. Mesa na Mhe. Suluhu watakuwa na mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mesa atakutana kwa mazungumzo mafupi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Y. Ndugai katika Hoteli ya Hyatt Regency. Baadaye siku hiyo hiyo, atakutana na Ujumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Hotelini hapo kabla ya kushiriki Chakula rasmi cha Mchana, Ikulu kilichoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake Mhe. Suluhu.
Mhe. Mesa ataondoka Dar es Salaam tarehe 03 Oktoba, 2016 alasiri kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kuendelea na ziara yake Visiwani humo. Akiwa Zanzibar, Mhe. Mesa ambaye atapokelewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi atakutana kwa mazungumzo rasmi na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt.  Ali Mohamed Shein, Ikulu ya Zanzibar.
Tarehe 04 Oktoba, 2016 Mhe. Mesa akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba atarejea Dar es Salaam akitokea Zanzibar kwa ajili ya kuendelea na ziara yake ambapo atatembelea Makumbusho ya Taifa.
Uhusiano wa Tanzania na Cuba
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Cuba ulianzishwa zaidi ya  miaka 50 iliyopita  na Viongozi Waasisi wa mataifa haya mawili, Rais Mstaafu wa Cuba, Mheshimiwa Fidel Castro na Baba wa Taifa, Hayati Julius K. Nyerere. Tangu Tanzania ipate uhuru Cuba imekuwa ikitusaidia katika maeneo mbalimbali ikiwemo afya, utamaduni, elimu, michezo, utalii, nishati, teknolojia na kilimo.
Ushirikiano katika Sekta ya Afya
Tanzania na Cuba zimekuwa zikishirikiana kwenye sekta ya afya ambapo hadi sasa kuna jumla ya Madaktari 30 kutoka Cuba wanaofanya kazi kwenye Hospitali mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar. Kati ya Madaktari hao 10 wapo Bara na 20 wapo Zanzibar wakiwemo wanaofundisha katika Kitivo cha Tiba, Chuo Kikuu cha Zanzibar na kutibu katika Hospitali mbalimbali Zanzibar.
Aidha, katika jitihada za Serikali za kupambana na malaria Serikali ya Cuba na Tanzania zilikubaliana kujenga Kiwanda cha Viuatilifu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu ambacho kimejengwa kwenye eneo la Viwanda Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani na kuzinduliwa mwezi Julai, 2015.
Kiwanda hicho ambacho kilijengwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya LABIOFAM ya Cuba kimekamilika na kwa sasa kinazalisha dawa za majaribio. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 6 za viuatilifu kwa mwaka ambazo zinatosheleza kwa matumizi ya Tanzania na hata kuuzwa nchi nyingine za Afrika.
Sekta ya Elimu
Katika Sekta ya Elimu Tanzania na Cuba zimekuwa zikishirikiana kwenye programu mbalimbali ikiwemo nafasi za ufadhili wa masomo nchini Cuba kwa wanafunzi kutoka Tanzania. Kuanzia mwaka 2008 hadi 2014 jumla ya Watanzania 64 walipata ufadhili wa mafunzo nchini Cuba katika fani mbalimbali ikiwemo udaktari, uchumi, TEHAMA na Michezo.
Pia Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Cuba ilianzisha Programu ya Elimu kwa Vijana na Watu Wazima ambayo hutolewa kwa kutumia vifaa vya kufundishia vinavyomwezesha mwanafunzi kusikia na kuona (audiovisual). Inatarajiwa kwamba zaidi ya vijana na watu wazima milioni 3 watakuwa wameshiriki programu hii ifikapo mwaka 2017. Mradi wa majaribio ya program hii ulizinduliwa mwaka 2014 katika Manispaa za Ilala, Temeke, Kinondoni, Ilemela, Mwanga, Bagamoyo, Mkuranga na Songea.
Sekta ya Michezo
Katika Sekta ya michezo Serikali ya Cuba wametupatia Wakufunzi wa Ngumi, Judo na Riadha. Hivi sasa wanatoa nafasi za mafunzo nne kila mwaka kwenye mafunzo ya michezo na utaalamu wa mazoezi ya viungo.
Hivyo, pamoja na kutumia fursa ya ziara hiyo kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizi mbili Tanzania itatumia nafasi hiyo kujikita katika kuanzisha ushirikiano kwenye maeneo mapya hususan biashara na uwekezaji.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 30 Septemba 2016

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages