Breaking News

Your Ad Spot

Sep 28, 2016

UFALME WA OMAN WAPANIA KUKARABATI MAJENGO YA KALE YA BEIT EL JAIB, ZANZIBAR

Beit Al Jaib, Zanzibar
Na Mwandishi Maalum, New  York
Ufalme wa Oman umeonyesha nia ya kukarabati majengo ya makubusho ya kale ya  Beit Al Jaib  maarufu kama “ House  of  Wonders” yaliyopo mjini Unguja, Zanzibar.

Nia hiyo imeonyeshwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman,  Yusuf bin Alawi bin Addullah, katika mazungumzo yake, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga na kufanya mazungumzo maalum wakati wa mkutano wa 71 wa  Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa, ambapo  Mawaziri hao walikuwa wakiongoza ujumbe wa nchi  zao.

Katika mazungumzo ya mawaziri  hao ambayo yalijikita  katika uimarishwaji wa uhusiano  na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Oman na Tanzania,  pamoja na mambo mengine,  Waziri  Mahinga  aliomba serikali ya Oman kuangalia uwezekano  wa kuanzishwa  kwa mradi wa kutunza mambo ya kale zikiwamo nyaraka muhimu zinazohusu uhusiano  baina ya nchi  hizo mbili.

Waziri Mahiga  alimweleza Waziri huyo wa Omani kwamba,  moja ya majengo yenye nyaraka za kumbukumbu muhimu za za kihistoria ni lile la  Beit Al Jaib ( House of wonders) lililokuwa Ikulu ya Utawala wa Kifalme, Zanzibar.

Alisema jego hilo lenye makubusho yaliyosheheni historia ya uhusiano na ushirikiano kati  ya Zanzibar na Sultanate of Oman na Afrika Mashariki kwa Ujumla limekuwa chakavu kutokana na kuwa la mda mrefu sasa.

Na kutokana na historia hiyo na  umuhimu wa  jengo hilo ambalo limejengwa mwaka 1883, Waziri ameiomba  Serikali ya  Oman kuangalia  uwezekano wa kulihifadhi ili pia liendelee kuwa kivutio kikubwa cha utalii.

Akijibu  ombi  hilo na  mengine yaliyowasilishwa na   Waziri Mahinga,  Waziria wa Mambo ya Nje wa Oman,  Yusuf bin Alawi bin Addullah amemtaka  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa  Afrika   Mashariki kuandaa andiko  na  kuliwasilisha  katika Serikali ya  Oman ili  pendekezo  hilo liweze  kufanyiwa kazi pamoja na mapendekezo mengine.

Katika  hatua nyingine,  Waziri wa Mambo ya Nje  na  Ushirikiano wa   Afrika Mashariki,  Augustine  Mahiga amekuwa na   kuwa  na mazungumgo na  Linda Thomas Greenfield,   Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayehusika na  masuala ya   Afrika.

Mazungumzo ya  Waziri Mahinga na  Linda Greenfield yalijikita zaidi  katika uhusiano na  ushirikiano  baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marekani.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sultanate of Oman  Yusuf bin Alawi bin Abdullah wakizungumzia kuhusu namna ya kuendelea kuimarisha uhusiano  mzuri baina ya  nchi hizo mbili.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages