Breaking News

Your Ad Spot

Sep 27, 2016

UVCCM TAIFA KUTUMA MKAGUZI WA HESABU ZA MALI ZA JUMUIYA HIYO ZILIZOPO ARUSHA

Na Woinde Shizza,Arusha
UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi, UVCCM, taifa itatuma mkaguzi wa hesabu na mali  za jumuia hiyo mkoa wa Arusha, katika kipindi cha wiki mbili kuanzia Septemba 27 mwaka huu ili kupata ukweli zilipo shilingi milioni 112.8 za umoja huo zinazokusanywa kila mwaka kutokana na kodi ya maduka.
     Makamu mwenyekiti UVCCM, Taifa, Mboni Mhita, aliyasema hayo jana mara baada ya kikao na wajumbe wa baraza la UVCCM ,mkoa wa Arusha, kilichofanyika ukumbi wa ccm ,mkoa na baada ya muda huo kamati ya taifa ya UVCCM, itarejea mkoani Arusha kufanyia kazi yaliyobainishwa na mkaguzi wa hesabu.

       Mhita,ambae anaongoza kamati ndogo ya watu watatu ya UVCCM,taifa,alisema anawashangaa wajumbe wa baraza hilo kushindwa kuchukua hatua na kusimamia jumuia hiyo hadi washikane mashati wakati wao wakiwepo na sasa wanagombea vibanda vya maduka ambavyo hawakuvijenga na wala hawajajenga vipya.
        Mhita,  alisema baadhi ya wajumbe wa baraza la UVCCM, Mkoa wa Arusha, hawaelewi  maana ya UVCCM, majukumu yao kwa kuwa hawajasoma kanuni za umoja huo  na wameingia kwenye uongozi bila kuwa na sifa na ndio chanzo cha migogoro.

        Wajumbe hao walikutana  na UVCCM kwenye mchakato  wa kugombea uongozi  na hawajosoma kanuni na katiba ya UVCCM hivyo kuwepo mitafaruku ndani ya umoja huo mkoani Arusha, ambayo inakwamisha maendeleo na ufanisi  wa shughuli za umoja huo.

        Alibanisha kuwa  baraza lazima libebe lawama  kwa kushindwa kusimamia majukumu kutokana na kushindwa kuendana na sera  za ccm kutokana na kukosa uadilifui, na kutokutambua majukumu yao.
         Kamati hiyo ndogo inafuatilia mgogoro wa UVCCM ,mkoa wa Arusha, ambapo  miongoni mwa majukumu ya kamati hiyo ni kuwasikiliza wajumbe wa baraza hilo kutokana na mgogoro uliojitokeza  hivi karibuni.
          Mhita, alilitaja jukumu lingine la kamati hiyo ndogo kuwa ni kupatiwa nyaraka za mikataba ya wapangaji wa maduka yote ya UVCCM, mkoa huo.

          Aidha alisema kuwa   baadhi ya viongozi wa baraza hilo waliandika barua ya kuwatukana na kuwadharirisha viongozi wa UVCCM taifa lakini leo walipoulizwa kwenye kikao hicho wamekana saini zao.
         Kwa upande wake Naibu katibu mkuu wa UVCCM taifa, Shaka Hamdu Shaka, alisema   UVCCM ni taasisi kubwa ya Chama cha Mapinduzi hivyo lazima wazingatie  heshima, umoja  na ushirikiano  kwa kuwa ndizo nguzo za uvccm.
        Amewaambia kuwa UVCCM, Inaongozwa na  kanuni, mbili za Utumishi na  Utawala  ,taratibu za fedha , maadili ya viongozi

         Alisema kilichotokea kwenye uongozi wa UVCCM, mkoa wa Arusha ni kutokufuatwa kwa kanuni ,taratibu  na miongozo ya jumuia hiyo.
           Alibainisha kuwa  ukiukwaji huo wa kanuni kumesababisha mgogoro wa uongozi uliopelekea aliyekuwa mwenyekiti wake, Lengai kusimamishwa uongozi huku aliyekuwa katibu wa mkoa Ezakiel Mollel, nae akiondolewa kutokana na kukaidi maelekezo ya mwajiri wake kuhamia makao makuu.
           Alisema kuwa  anashangazwa kuona UVCCM ikiwa na wajumbe 16 wa kamati ya miradi jambo ambalo ni kinyume na kanuni za UVCCM kwa kuwa hakuna kifungu kinachoelekeza kamati iwe na wajumbe wengi kiasi hicho hata taifa haipo.
           Aidha alisema  UVCCM mkoa wa Arusha, inakusanya shilingi milioni 112.8 kwa mwaka makusanyo yanayotokana na maduka yaliyopo kwenye jengo la UVCCM mkoa lakini hazijulikani ziliko.
           Awali mjumbe wa kamati hiyo kutoka mkoa wa Lindi,Amir Mohamed,aliwataka wanachama wa UVCCM mkoa wa Arusha, kujenga umoja na,upendo  na kuacha kushughulikiana wao kwa wao na kusababisha migawanyiko ili kuiwezesha jumuia hiyo iweze kufikia malengo na kutimiza majukumu yake ya kisiasa.
          Mohamed, alikuwa akitoa salamu za UVCCM taifa, kwenye kikao maalumu cha baraza la umoja wa Vijana mkoa wa arusha, iliyofanyika ukumbi wa CCM, Mkoa kilichokuwa kikisikiliza mgogoro wa uongozi wa jumuia hiyo.
           Alisema UVCCM ni tanuru la  kuoka viongozi  na wajumbe wote wa baraza hilo wana wajibu  kufahamu mipaka  na misingi ya uongozi.
        Alisema  UVCCM,haitawavumilia watakaokiuka  misingi na maadili  itawatimua  hivyo lazima watumie rasimilami za umoja huo walinde zingine  kwa manufaa  kwa kuwa  UVCCM ni walinzi wa mali za chama na  viongozi wake.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages