.

TANZANIA YAADHIMISHA YA SIKU YA WAZEE DUNIANI 2016

Oct 3, 2016

chig1
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh, Ummy Mwalimu akipiga ngoma ya asili wakati wa madhimisho ya siku ya wazee duniani yaliyofanyika kitaifa wilaya ya mbalali, mbeya 1.10.2106
chig2
Wazee wakipita mbele ya mgeni rasmi Mh. Ummy Mwalimu wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wazeeduniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Mbeya. 1.10.2016


Na Erasto Ching’oro  na rehema Kasimoto,  Rujewa- Mbarali, Mbeya

Lengo ni kuondoa kero kwa wazee katika kupata Huduma za Afya
Waziri wa Afya kupeleka Bungeni Mswada wa Sheria ya Taifa ya Wazee  kabla ya mwezi June 2017 ili pia kuweka  wajibu wa kisheria kwa watoto na familia kuwatunza wazee wao.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu  amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuwatambua wazee wasio  na uwezo na kuwapatia vitambulisho vya matibabu bila malipo, sambamba na vitambulisho vya Bima ya Afya ya Jamii (CHF),  kabla ya tarehe 31 Desemba 2016

Agizo hilo amelitoa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika kitaifa Wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya. Maadhimisho hayo yaliyoongozwa na Kauli Mbiu “Zuia Unyanyasaji dhidi ya Wazee”.
Akiongea na hadhara iliyokusanyika kwa ajili ya maadhimisho hayo, Mhe Ummy ambye alikuwa Mgeni Rasmi, alisema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 inayotambua kuwa wazee ni kundi maalum linalohitaji kupewa huduma za Afya, hususani katika kuboresha huduma za matibabu kwa wazee wasio na uwezo.  “Lete barua ya utambulisho kutoka Serikali ya Kijiji na Mtaa” ni kauli wanayokumbana nayo wazee wengi kila wanapokwenda kupata huduma za afya katika vituo vya afya na Hospitali za umma nchini hivyo anaamini kuwepo kwa Vitambulisho hivi kutasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wazee nchini na hivyo kuondoa unyanyasaji kwa wazee nchini.
Kuhusu kauli mbiu ya Maadhimisho haya Mhe. Ummy alieleza kuwa Sera ya Wazee ya mwaka 2003 inatuelekeza kuwatumia wazee kama Hazina ya Taifa. Na kuwa tutumie mchango wao katika kuleta maendeleo kwa kuweka mazingira mazuri ya kuwalinda na kuwatetea wazee wetu siku zote za maisha yao ikiwa ni pamoja na kuzuia vitendo vya unyanyasaji.”
Pamoja na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kuwalinda na kuwaenzi wazee nchini bado wazee wetu hasa walio vijijini wanafanyiwa  vitendo vya unyanyasaji na ukatili ambavyo sio tu vinarudisha nyuma ustawi wao bali pia kuwanyima haki yao ya msingi ya kuishi. Na kinachosikitisha zaidi, vitendo hivi vya unyanyasaji vinafanywa katika jamii zetu, katika koo zetu na katika kaya zetu na watu wenye wajibu wa kuwalinda wazee hawa wengine wakiwa ndugu zao wa karibu!”.
Mhe Ummy aliwasihi wananchi kuacha vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wazee na vikongwe hapa nchini kwa kuwa ni jambo linalohuzunisha sana na kutia doa Taifa letu. Wakati tukiadhimisha Siku ya wazee Duniani, mikoa inayoongoza kwa kuwa na vitendo vingi vya  unyanyasaji na ukatili dhidi ya wazee hapa nchini ni Tabora, Geita, Mwanza na Shinyanga. Rai inatolewa kuchukua hatua kujeweka mazingira salama kwa wazee wetu.
Mhe Ummy aliwahakikishia wazee kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za kisera na kisheria kuhakikisha wazee wanalindwa na vitendo vyote vya unyanyasaji na ukatili ikiwemo vitendo vya mauaji ya wazee ambapo sababu kubwa ya vitendo hivi ni imani potofu na uelewa mdogo ndani ya jamii ya Tanzania.
‘’Uzee na Kuzeeka Hakukwepeki! Kila mtu ni mzee mtarajiwa. Hivyo kila mmoja wetu anao wajibu wa kuwaheshimu, kuwalinda na kuwaenzi wazee wetu’’ alieleza Mh, Ummy.
Waziri Ummy alitoa wito kuwa na uwajibikaji wa pamoja kwa wananchi wote katika kutokomeza vitendo vya unyanyasaji yakiwemo mauaji ya kikatili dhidi ya wazee ‘’Serikali imepanga kupeleka Bungeni Muswada wa Sheria ya Taifa ya Wazee  kabla ya mwezi June 2017 ambao siyo tu itawekwa adhabu kali kwa wote watakaokutwa na hatia ya kufanya vitendo hivi bali pia itaweka  wajibu wa kisheria kwa watoto wa familia  husika na ndugu wa karibu kuwalea na kuwatunza wazee wao’’.
Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani hufanyika kila tarehe 1 Octoba ya kila mwaka lengo likiwa ni kutafakari hali ya maisha ya wazee na changamoto zinazowakabili wazee; na hivyo kuweka mipango thabiti ya kuboresha maisha yao na kuwafanya waishi maisha ya heshima, hadhi, na kuthaminiwa utu wao.(P.T)

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช