.

TAASISI ISIYO YA KISERIKALI YAJA NA MIKAKATI YA KUSAIDIA WATU WENYE ULEMAVU WA AKILI

Nov 28, 2016

KHAMISI DAR ES SALAAM

TAASISI isiyo ya kiserikali ya Safety Bridge for People with Disabilities (SBPD) ipo mbioni kuanza utafiti maalum kwaajili ya kupata takwimu ya watu wenye ulemavu wa akili (Wendawazimu) nchini ili kujua ukubwa wa tatizo na kuanza harakati za kupunguza tatizo la unyanyapaa dhidi ya kundi hilo unaoendelea kwa kasi hapa nchini.

Utafiti huo utaanza katika mkoa wa Dar es salaam na baadaye katika mkoa wa Mbeya, Mwanza,Arusha Dodoma na Tanga.

Akizungumza na ujijirahaa blog mwenyekiti wa (SBPD) Mohamed Mchingama alisema taasisi hiyo imeamua kuanza harakati za kulisaidia kundi hilo kwa kuwa limesahaulika kabisa hali ambayo inaongeza unyanyapaa na mateso dhidi yao.
"Watu wenye ulemavu wa akili ni kundi ambalo hata serikali imelisahau kabisa ndiyo maana wanaonekana wakila majalalani lakini hakuna matamko yeyote yanayotolewa kama ilivyo kwa makundi mengine ya watu wenye ulemavu" alisema Mchingama.
Mchingama alisema watu wenye ulemavu wa akili ni kundi ambalo lina ishi kwa taabu kwa kuwa halipati taarifa muhimu ambazo mwisho huleta madhara kwa jamii hivyo kujikuta wakiathirika na hakuna mtu anayeweza kuchukua hatua za kulisaidia kundi hilo katika kipindi hicho na hakuna takwimu zozote zinazotolewa kutokana na kuathirika kwao.


Alitaja baadhi ya taarifa hizo kuwa ni pamoja na taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuhusu mvua kubwa, milipuko ya magonjwa kama kipindupindu zinazotolewa na Wizara ya afya nchini au kuhusu matetemeko makubwa kama lile lililotokea mkoani Kagera siku za hivi karibuni.
Aidha aliongeza kuwa kundi hili kwa kuwa halina uwezo wa kuchukua tahadhari kuhusiana na magonjwa ya milipuko linaweza kuwa sehemu ya chanzo cha milipuko ya magonjwa hayo na muendelezo wake kutokana na kuishi bila tahadhari.


Kwa upande wake katibu wa taasisi hiyo Mohamedi Mrope alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha inapunguza ama kuondoa kabisa unyanyapaa dhidi ya kundi hilo la watu wenye ulemavu wa akili.
Alitaja baadhi ya mikakati yao kuwa ni pamoja na kuandaa kampeni maalum kwaajili ya kupinga ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu litakalo kuwa na kauli mbiu ya "Ulemavu wa akili siyo adhabu,ninapaswa kuheshimiwa na kupewa haki zangu kama binadamu mwenye akili timamu".
Kuandaa semina kwa kada mbalimbali wakiwemo mama na baba lishe,makondakta na madereva daladala,viongozi wa dini, waandishi wa habari, wabunge na madiwani, pamoja na wanafunzi  wa shule za msingi sekondari na vyuo lengo likiwa ni kuleta matokeo chanya ya kulinusuru kundi hili ambalo halipati chakula salama mavazi na malazi salama kama binadamu anavyopaswa kuishi.
MWISHO

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช