Breaking News

Your Ad Spot

Dec 31, 2016

VIONGOZI WA CLUB YA WAANDISHI SHINYANGA WAKUTANA NA DC KAHAMA, KUHUSU MWANDISHI ALIYEFIKISHWA MAHAKAMANI

UONGOZI wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga (SPC), na baadhi ya waandishi wa habari wilayani Kahama, wakiwa Ofisini kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu kupata muafaka kufuatia kukamatwa na kufikishwa mahakamani mwandishi wa habari wa kujitegemea Paul Kayanda.
Kikao hicho cha usuluhishi kilichofanyika leo Jumamosi Desemba 31,2016 katika ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo,kimehudhuriwa pia na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Kahama.

Kayanda alikamatwa jana Desemba 30,2016 na kufikishwa mahakamani kwa agizo la Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akimtuhumu kuandika habari za kumdhalilisha na kuzisambaza kwenye barua pepe mbalimbali za vyombo vya habari.

Katika kikao ,Uongozi wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga ,ulimuomba mkuu wa wilaya Nkurlu kutaka kufahamu kilichomsukuma kuchukua maamuzi hayo,na nini ushauri wake juu ya suala hilo lakini pia kumsikiliza mwandishi Paul Kayanda.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili,kikao kilibaini kuwepo kwa mapungufu katika habari iliyoandikwa na Kayanda kuhusu habari ya laptop mbili zilizoibiwa nyumbani kwa mkuu huyo wa wilaya.

Mkuu huyo wa wilaya alikiri kuwepo kwa tukio la wizi nyumbani kwake lakini mwandishi huyo aliandika habari kwa kuingilia uhuru binafsi wa kiongozi huyo akielezea watu wanaoingia na kutoka nyumbani kwake lakini maisha anayoishi na kijana wake.

Kwa kuangalia maslahi mapana ya umma kutokana na kutegemeana katika kusukuma maendeleo ya jamii baina ya uongozi wa serikali na waandishi wa habari, kikao kimemtaka Kayanda kumwomba radhi mkuu huyo wa wilaya kwa kuingilia uhuru wake binafsi na kuuhusisha na habari ya wizi wa laptop badala ya kujikita kwenye tukio la wizi wa laptop pekee.

Kikao pia kimebaini kuwa pamoja na mapungufu ya mwandishi, ni ukweli ulio wazi kuwa mkuu huyo wa wilaya aliibiwa kompyuta mpakato (lap top) mbili nyumbani kwake na kuagiza vijana watatu wakamatwe kwa mahojiano polisi akiwemo mmoja anayeishi nyumbani kwake japo ameelezea kuwa hakujua walishikiliwa kwa siku ngapi.

Mkuu huyo wa wilaya pia alieleza kukerwa na ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia simu ya mkononi (sms) alizodai kutumiwa na Kayanda kwa kutumia simu nyingine (tofauti na anayotumia) zenye lugha ya kumtuhumu na kumdhalilisha.

Hata hivyo kikao hakikuona kuwepo kwa ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha kama ni za mwandishi huyo kweli au la huku kikao kikiomba sms hizo zifuatiliwe ili wamiliki wa namba hizo wajulikane .

Baada ya kujadiliana kwa kina katika kikao hicho kilichodumu kwa muda wa saa mbili,Kayanda amemwomba mkuu wa wilaya msamaha kwa mapungufu yaliyojitokeza katika habari hiyo aliyoiandika, na mkuu wa wilaya ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kahama amekubali kumsamehe mwandishi huyo akiahidi kufuata taratibu zingine kuondoa kesi mahakamani na kutaka kusafishwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ilikoandikwa habari hiyo.

Nkurlu amesema anatambua kazi nzuri inayofanywa na waandishi wa habari wilaya ya Kahama na mkoa wa Shinyanga kwa ujumla katika kuandika habari zinazohusu serikali na akaomba kudumishwa kwa ushirikiano uliopo baina ya viongozi wa serikali na waandishi wa habari ili kusaidia kuharakisha maendeleo ya wananchi huku akiwasisitiza waandishi wa habari kuzingatia weledi katika kazi zao.

Aidha Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga imewasisitiza waandishi wa habari kuzingatia weledi na kufuata maadili katika kutekeleza majukumu yao ili kuepuka migongano isiyokuwa na tija kwa umma.

Pia tunawashauri wadau wote wa habari pindi inapotokea kuingia katika mgogoro wowote ama na waandishi wa habari au chombo cha habari si vyema kwenda mahakamani moja kwa moja bali wawasiliane na viongozi wa klabu za waandishi wa habari katika mkoa husika ili kusuluhishana na kuwekana sawa.

Imetolewa na 
Kadama Malunde
MWENYEKITI –SPC
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu,waandishi wa habari na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kahama wakiwa katika kikao cha usuluhishi
Waandishi wa habari wakiwa katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kahama
Kikao kinaendelea
Waandishi wa habari wakiondoka katika ofisi ya mkuu wa wilaya baada ya kikao kumalizika

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages