.

ZUNGU ALAZWA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE (JKCI)

Dec 2, 2016
Mbunge wa Jimbo la Ilala Mhe. Azzan Musa Zungu akiwa amelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya moyo ambapo kwa sasa hali yake inaendelea vizuri. Kutoka kulia ni Muuguzi Mwandamizi Sr. Chagui Mgaza na kushoto ni Mwinyi Maulidi ambaye ni dereva wa Mhe. Zungu.Picha na Anna Nkinda - JKCI.


Na Anna Nkinda – JKCI.
1/12/2016 Mbunge wa Jimbo la Ilala Mhe. Azzan Musa Zungu amewashukuru wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma nzuri ya matibabu wanayompatia na kuiomba taasisi hiyo kutoa huduma kama hiyo kwa watanzania wote.

Mhe. Zungu ambaye amelazwa katika Taasisi hiyo amezitoa  shukrani hizo leo wakati akiongea na waandishi wa habari waliotaka kufahamu kuhusu maendeleo ya afya yake.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu naendelea vizuri hali yangu siyo kama jana. Nilianza kuumwa majira ya saa nane  8:30 mchana nikiwa nyumbani katika mazingira magumu ambapo mapigo ya moyo yalipanda ghafla nikapelekwa Hospitali ya Amana na baadaye  Muhimbili  kitengo cha Huduma ya dharula majira ya saa 12jioni  kisha  nikaletwa  hapa”. 

“Kwa namna ya pekee nawashukuru sana wafanyakazi wa Amana, Muhimbili na Taasisi ya Moyo ambao wamenipokea na kunipa  huduma nzuri na kama mnavyoniona afya yangu inaendelea vizuri tofauti na nilivyokuja jana”. alisema Mhe. Zungu.

Aidha Mhe. Zungu aliwataka watanzania kujiunga na mfuko wa Taifa wa Bima ya afya ambao hata yeye ni mwanachama  kwa kuwa mwanachama wa mfuko huu kutawasaidia kupata matibabu pindi watakapoumwa bila ya kutoa fedha  mfukoni.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji  wa JKCI Prof. Mohamed Janabi alisema hali ya Mhe. Zungu  inaendelea vizuri tofauti na walivyompokea jana.  Hivi sasa madaktari wako katika uchunguzi wa matatizo ya Moyo baada ya hapo watajuwa tatizo na kumpatia tiba  na anaamini baada ya siku tatu zijazo anaweza kuruhusiwa.

“Kipindi cha nyuma viongozi wenye matatizo kama haya walikuwa wanapelekwa  nje ya nchi kwa ajili ya matibabu  hivi  sasa Serikali imeboresha  huduma za matibabu ya Moyo  hivyo basi wagonjwa  wengi wanatibiwa hapa nchini”, alisema Prof. Janabi.

Aliwashauri wananchi kupima afya zao japo mara moja kwa mwaka, wakiona dalili za viashiria vya ugonjwa wa Moyo waende haraka  Kituo cha Afya kilichopo jirani kwa ajili ya matibabu. 

Prof. Janabi alimalizia kwa kuwasisitiza wananchi kufanya  mazoezi na kula vyakula sahihi na kwa upande wa wagonjwa wa Moyo wanatakiwa kumeza  dawa kipindi chote cha maisha yao wasiache kunywa dawa kwani wagonjwa wengi wanaorudi kupata matibabu ni wale walioacha  kumeza dawa.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช