Breaking News

Your Ad Spot

May 12, 2017

DK. SALIM AHMED SALIM AWAFUNDA WA TANZANIA NA BARANI AFRIKA

Utambuzi wa historia ya nchi una mchango mkubwa kwa vijana kuweza kufahamu madhila yaliyotokea na jinsi viongozi walivyopigana katika kuleta uhuru na maendeleo ya Taifa. Katika makala haya Judith Mhina wa Idara ya Habari MAELEZO anaelezea.

Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Kwanza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Dkt Salim Ahmed Salim amesema kuwa vijana barani Afrika wana wajibu wa kujua historia ya nchi na viongozi waliojitolea kuleta uhuru, umoja, amani na maendeleo ya watu.

Amesema, athari za vijana kutojua historia ya nchi na viongozi waliopigania uhuru ni pamoja na kukosa uzalendo na uwajibikaji katika kutekeleza malengo ya Serikali katika kuleta mapinduzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Ameeleza kuwa, nafasi waliyonayo kama vijana ni kujifunza jinsi viongozi wetu walivyoweza kuweka misingi ya umoja, amani, mshikamano na changamoto zilizowakabili na jinsi walivyoweza kuzitafutia ufumbuzi badala ya kukata tamaa na kuilaumu Serikali kuwa haiwasaidii.

Dkt Salim amefafanua kuwa nchi yetu imeonyesha muelekeo mzuri katika  kulikomboa kundi kubwa la vijana kuelekea kwenye uchumi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. “Mimi binafsi naipongeza Serikali yetu kwa kuonesha nia njema ya kupunguza au kuondoa changamoto, zinazowakumba vijana wetu. Vijana ni wengi kuliko kundi lolote nchini na hawana uhakika wa maisha yao ya kila siku hivyo wanahitaji kubadilika.”

Mwana-diplomasia huyo mkongwe nchini ameendelea kusema kwamba maamuzi ya Serikali ya Tanzania kuelekea kuwa Taifa la viwanda yatahamasisha vijana kupenda kujishughulisha na kazi mbalimbali za uzalishaji kama vile kilimo.

“Jambo la msingi kwa Serikali ni kuhakikisha kwamba inaweka mazingira mazuri na rafiki kwa vijana kuvutiwa katika sekta mbalimbali kwani nchi yetu inayo ardhi ya kutosha tofauti na nchi nyingine barani Afrika. Lakini pia napenda kuchuku fursa hii kuwaasa vijana kuchangamkia fursa hiyo kwani ni mtaji mkubwa kwao katika kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.”

“Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba malighafi zote zinapata masoko katika viwanda, miundombinu ya uhakika. Aidha, hii itachochea uzalishaji na ajira kuongezeka maana bidhaa zote zitaongezwa dhamani hapa nchini badala ya kuagiza nje bidhaa zilizoongezwa thamani na kudidimiza uchumi wa nchi yetu.” Amesisistiza Dkt Salim.
  
Akitoa Mfano wa athari za vijana kutojua historia yao Dkt Salim amesema Afrika ya Kusini ni moja kati ya nchi za Afrika amabazo vijana wake wamekata tamaa na kutowathamini Wazee walioshiriki katika harakati za kuleta ukombozi. Amesema, kitendo hiki cha kuwadharau wazee kimepelekea mfarakano kati ya makundi haya mawili ambayo yanawajibu mkubwa wa kushirikiana na kuijenga Afrika ya Kusini yenye neema kwa wananchi wake wote bila kubagua.

Ameeleza kwamba vijana hao wamejenga chuki na kuwachukia vijana wenzao waliotoka katika nchi nyingine za Afrika na kuwaona maadui kwa kwenda nchini mwao na kufanya kazi ambazo wao wanadhani ni za kwao. Athari hii inajitokeza kwa kuwa hawajui historia ya nchi yao na nini viongozi wao walipigania katika kuweka misingi ya umoja, amani na mshikamano Barani Afrika. 

Hata hivyo siwalaumu vijana hata kidogo kwa hakika vijana wana hali ngumu ya maisha kweli kweli, wanahangaika kutafuta riziki, bila mafanikio. Ni vema kukaa nao na kuongea kuhusu hali zao za maisha na changamoto zinazowakabili kwa pamoja kutafuta ufumbuzi wa changamoto husika.

Bara la Afrika lina changamoto nyingi, kama za uongozi, vita vya madaraka, makundi yanayohamisiana, vita vya wenyewe kwa wenyewe , ukabila na mengineyo ambayo hayaleti picha nzuri kwa Afrika na yanadhoofisha ustawi wa Bara letu na vijana kukata tamaa.

Taasisi ya Mwalimu Nyerere ina jukumu la kutoa elimu kwa vijana wote Barani Afrika juu ya mustakabali wao na kuweka misingi imara ya umoja, amani,  mshikamano  na Maendeleo kwa watu wote katika nchi zao bila kubaguana.

Tunaendesha makongamano, midahalo na semina katika majukwaa mbalimbali ili kuwaelimisha vijana kuhusu historia za nchi zao , viongozi wao na misingi waliyoiweka na umuhimu wa kutanzua kwa pamoja changamoto zilizopo na kuongea yale yote ambayo wanadhani hayaendi vizuri.

Dkt. Salim amewomba vijana kuzingatia elimu wanayopewa maana Taasisi ya Mwalimu Nyerere inahitaji kupata viongozi miongoni mwa vijana wa Tanzania. Ni vema kujua changamoto zilizopo ili vijana hao watakaochukua uongozi kuendelea kuelezea, kufundisha, kuuisha katika misingi ya umoja, amani, mshikamano na maendeleo kwa watu wote na pia ustawi wa Mataifa yote ya Afrika.

Akizungumzia suala la uongozi na ushiriki wa vijana katika kujenga Taifa, Dkt Salim amesema ni vema vijana kushirikishwa katika uongozi kwa kuwa bado wana nguvu ya kuleta maendeleo katika nchi zao. Hata hivyo alitoa tahadhari na kusema “Kijana sio kigezo cha uongozi hata kidogo”,

Akitoa mfano Dkt Salim amesema, “Mimi niliteuliwa  kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri  nikiwa na miaka 22, nadhani ni umri mdogo kuliko vijana wa sasa wanaoteuliwa,  lakini niliaminiwa na kutimiza wajibu wangu kwa nchi na viongozi wangu walioniteua, kwa kuwa nilijua tulikotoka, tulipo na tunakotaka kuelekea. Hayo nilijifunza kutoka kwa viongozi wangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume.”

Dkt Salim muda wote wa uongozi kama Balozi na mwakilishi wa nchi kimataifa alielezea msimamo, matakwa na mapendekezo tunayokubaliana nayo kimataifa. Aidha, alisisitiza suala la umoja, amani, mshikamano na jinsi ya kuleta maendeleo katika nchi zote za Afrika kwa kuwa nchi yetu inaona bila umoja hakuna suluhisho la amani katika nchi zetu na alifanya hayo kwa kuwa nilijua historia ya nchi yangu.

“Wito wangu kwa vijana ambao watakuja kuiongoza Taasisi ya Mwalimu Nyererer ni vema wakajipanga kwa kuwa kazi iliyopo mbele yao ni kuwaelimisha vijana wenzao ili kuthamini na kuuisha umoja, amani na kuleta maendeleo kwa watu wote iwe ni sehemu ya maisha yao.”

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume ni mfano wa kuigwa katika kudumisha umoja, amani na mshikamano katika Bara la Afrika. Umoja wao ulizaa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Dkt. Salim alimalizia kwa kusema Mwalimu Nyerere siku zote za maisha yake, alikuwa akitembea na kuwaasa Watanzania juu ya umoja, aman, mshikamano na Maendeleo kwa watu wote bila ubaguzi. Mwalimu alitambua wajibu wake.

Akitoa hitimisho Dkt Salim amesema: “Hapa Tanzania asilimia 60 ya idadi ya watu milioni 50 ni vijana, hawa wasipoelewa na kuuisha misingi ya Taifa lao yaani umoja, amani, mshikamano na Maendeleo kwa watu wote bila ubaguzi tutakuwa tumefanya kosa kubwa sana na dunia itatulaumu kwa hilo, kwa sababu Tanzania ndio mfano wa kuigwa.”

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages