Breaking News

Your Ad Spot

May 8, 2017

TANZANIA YASHIKA NAFASI YA TATU AFRIKA KWA SHERIA BORA YA USIMAMIZI NA UDHIBITI WA KEMIKAL

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Tanzania imeshika nafasi ya tatu barani Afrika ikiongozwa na nchi ya Afrika Kusini na Nigeria kwa kuwa na Sheria bora ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Prof. Samweli Manyele alipokua akizungumza na waandishi wa habari juu ya mkutano wa Kimataifa wa Udhibiti wa Kemikali na Kemikali Taka uliofanyika Geneva, Uswisi kuanzia Aprili 24 hadi Mei 5 mwaka huu.

Prof. Manyele amesema kuwa katika Bara la Afrika Tanzania ndio nchi pekee ambayo ina taasisi ya Serikali inayosimamia kemikali wakati nchi zingine usimamizi wa masuala ya kemikali upo katika taasisi za mazingira kitu ambacho kinapelekea usimamizi hafifu wa kemikali hizo.

“Tanzania ni nchi pekee Afrika ambayo taasisi inayohusika na masuala ya kemikali ipo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na pia ni taasisi yenye kusimamiwa na wataalamu wa kemikali waliobobea pamoja na kuwa na maabara kubwa inayojulikana kimataifa,”alisema Prof. Manyele.

Akiongelea kuhusu mkutano huo, Prof. Manyele amesema kushiriki katika mkutano huo ni jambo la kisheria hivyo kupeleka watumishi watatu kutoka kwenye taasisi hiyo inadhihirisha kuwa Tanzania imetimiza majukumu yake kama Taifa.

Amefafanua kuwa mkutano huo unaisaidia taasisi kutoa taarifa kuhusu utendaji kazi, kujifunza nchi zingine wanafanyaje kazi zao, kupata majibu ya moja kwa moja pamoja na kujadiliana namna ambavyo wataboresha utendaji kazi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Huduma ya Ubora wa Bidhaa, Daniel Ndiyo ametaja wadau wanaotakiwa kupata taarifa na maamuzi ya mkutano huo kuwa ni wafanyabiashara, watumiaji wa kemikali hizo pamoja na mamlaka mbali mbali za usimamizi wa kemikali. 

Naye Meneja wa Kanda ya Kaskazini GCLA , Christopher Anyango amesema mkutano huo unawasaidia wananchi kupata msaada wa haraka kutoka katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwa wana uelewa pamoja na kupata mafunzo ya kemikali zinazoruhusiwa na zisizoruhusiwa kulingana na mahitaji kwa wakati husika.

Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ilishiriki katika mkutano huo wa utekelezaji wa mikataba mitatu ikiwemo ya usafirishaji wa taka sumu kimataifa (Basel), mkataba unaohusu kemikali zenye madhara na zinazochukua muda mrefu kuoza katika mazingira (Stockholm) pamoja na mkataba wa Rotterdam unaohusu upashanaji taarifa juu ya kemikali hatari na viuatilifu katika biashara ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages