NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amekutana na Rais wa Kampuni ya
TBEA ya China, Zhang Xin kwa ajili ya kujadili masuala ya uwekezaji kwenye
Sekta ya Nishati nchini.
Mkutano
huo wa Waziri Muhongo na Rais huyo ambaye ameongozana na Ujumbe wake umefanyika
Mei 21, 2017 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Wataalamu kutoka Wizara ya
Nishati na Madini na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Waziri
Muhongo aliuelezea ujumbe huo baadhi ya fursa za uwekezaji kwenye Sekta ya
Nishati nchini na kuwashauri wachague eneo ambalo wanahitaji kuwekeza ili
taratibu zianze mapema.
“Fursa ni
nyingi sana, ni nyinyi kuamua wapi mmelenga ili taratibu ziendelee ikizingatiwa
kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha tunakuwa na Tanzania ya Viwanda,”
alisema Waziri Muhongo.
Aliagiza
wataalamu wa Wizara ya Nishati na Madini kukutana na Ujumbe huo hapo kesho ili
kujadili kwa undani dhamira yao ya uwekezaji ikiwemo kuchagua eneo ambalo
wangependa kuwekeza.
Kwa upande
wake Xin alisema kampuni yake inaridhishwa na kasi ya Serikali ya Tanzania
chini ya Uongozi wa Rais John Pombe Magufuli na hivyo wanatarajia kuwekeza
kiasi cha Dola za Marekani bilioni 10 kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Nishati,
Barabara, Uendelezaji wa Miji, na Usafirishaji.
Alisema
uchumi wa Tanzania umezidi kuimarika na hivyo kuzidi kuvutia wawekezaji kwenye
maeneo mbalimbali hususan ikizingatiwa kuwa Tanzania ni Taifa lenye amani linalokuwa kwa kasi kubwa.
Ujumbe huo
upo nchini Tanzania na unatarajia kukutana na Wizara mbalimbali ili kubaini
fursa zaidi za uwekezaji nchini.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269