Breaking News

Your Ad Spot

Jul 2, 2017

MAKAMU WA RAIS MAMA SAMIA AENDA ETHIOPIA LEO

Mama Samia
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameondoka nchini leo jioni kwenda Addis Ababa, Ethiopia ambako atahudhuria Mkutano wa 29 wa Wakuu wa  Nchi na Serikali  wa Umoja wa Afrika (AU).


Katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameagwa na Viongozi mbalimbali  wa Serikali.



Katika Mkutano huo wa siku mbili kuanzia tarehe 03-hadi 04 Julai-2017, Makamu wa Rais  Samia Suluhu Hassan atamuakilisha Rais Dk. John Magufuli kwenye mkutano huo.



Kabla ya ufunguzi rasmi, Mkutano huo ulitanguliwa na vikao vya Baraza la Utendaji linalowashirikisha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Kamati ya Uwakilishi wa Kudumu  inayowahusisha Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje kutoka nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika.



Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi  na Serikali  utafunguliwa rasmi tarehe 03-Julai-2017 katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika Jijini Addis Ababa, Ethiopia na  utajikita katika kujadili masuala mbalimbali yanayohusu umoja huo.



Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika Mkutano huo ni pamoja na taarifa  kuhusu Maboresho katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na maboresho ya kitaasisi katika AU na  hali ya Ulinzi na Usalama katika bara la Afrika.



Kuhusu  hali ya  ulinzi na usalama katika Bara la Afrika majadiliano ya Viongozi hao yatajikita zaidi kwenye nchi za Sudan Kusini, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- DRC na Libya.  Aidha, majadiliano hayo pia yatagusa  hali ya usalama kwenye baadhi ya nchi ambazo ziliathiriwa na kundi la Boko Haram za  Nigeria, Niger, Chad na Cameroon.



Mkutano huo 29 wa AU, unatarajiwa kuhuduhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.



Mkutano huo 29 wa AU utakaofanyika Jijini Addis Ababa, Ethiopia utaongozwa na Mheshimiwa  Alpha Conde  Rais wa Jamhuri ya Guinea ambaye ndiye Mwenyekiti wa AU.


Kauli Mbiu ya Mkutano huo ni Kuimarisha Mgawanyiko wa Idadi ya Watu Kupitia Uwekezaji katika Vijana (Harnessing Demographic Divident Through Investments in the Youth)

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages