Breaking News

Your Ad Spot

Oct 21, 2017

MAHAFALI YA KIDATO CHA NNE YA SHULE INAYOTOA ELIMU KATIKA MFUMO USIO RASMI KWA YATIMA NA WAATHIRIWA WA NDOA NA MIMBA ZA UTOTONI MKOANI SHINYANGA

Shule ya Sekondari  ya Agape Knowledge Open School inayotoa elimu katika mfumo usio rasmi kwa yatima na waathiriwa wa mimba za utotoni,  imefanya Mahafali yake ya kwanza ya Kidato cha Nne ambapo jumla ya wahitimu 29 wametunukiwa vyeti.

Mahafali hayo yamefanyika jana, katika shule hiyo iliyopo mtaa wa Busambilo Kata ya Chibe Manispaa ya Shinyanga, mgeni akiwa Afisa Elimu Taaluma mkoa wa Shinyanga, James Malima ambaye alimwakilisha Mkuu wa mkoa huo, Zainab Telack. 

Mkuu wa shule hiyo, Adili Haruni Nyaluke alisema wahitimu ambao wote ni watoto wa kike walioanza masomo yao mwaka 2014 wakiwa 54 lakini kutokana na changamoto mbalimbali ni wasichana hao 29 tu waliofanikiwa kuhitimu masomo. 

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Agape AIDS Control Programme (AACP), linalomiliki shule hiyo, John Myola alisema mahafali hayo ya kwanza ni ya watoto wa kike ambao wengi wao wamepoteza wazazi kutokana na ukimwi na waliookolewa kutoka katika ndoa na mimba za utotoni na kurudishwa shuleni kupitia mfumo wa elimu usio rasmi wa masafa au elimu ya watu wazima. 

Myola aliwataka wazazi na walezi kuwasaidia watoto hao pindi watakaporudi nyumbani kusubiri matokeo ya kidato cha nne na kukumbusha kwa wahitimu hao hawarudi nyumbani kuolewa.

“Wanaporudi nyumbani siyo kwamba wanarudi kuolewa, bado hawajamaliza masomo, watoto hawa wana uwezo mkubwa darasani, tuna imani watafaulu vyema katika mtihani wao, mnachotakiwa kufanya ni kuwalea katika ustawi unaotakiwa, msiwaache peke yao, msiwaozeshe”, alisema Myola. 

Katika risala yao  wahitimu hao walisema elimu waliyoipata imewapatia msingi mzuri wa kujiunga na elimu ya juu lakini pia imewajengea uwezo mzuri wa kujitambua, kufikiri, kufanya maamuzi sahihi na mambo kadhaa ikiwemo elimu ya ujasiriamali, stadi za maisha na stadi za kazi na afya ya uzazi. 

Wahitimu hao waliomba mamlaka zinazohusika kuhakikisha kesi za watoto wa kike wanaopatiwa mimba udogoni, kuozeshwa mapema, kubakwa, kupigwa na kutelekezwa zinapofikshwa katika vyombo vya sheria haki zisimamiwe ipasavyo na haki  itendeke, wakisema kuwa kesi nyingi za aina hiyo zimekuwa zikichezewa sana na kuwa na mwisho mbaya. 

Wahitimu hao pia walitaka wazazi wanaolazimisha watoto kuolewe na wanaume wanaotia mimba wapatiwe adhabu kali na wanapofikishwa mahakamani kesi zao zisichukue muda mrefu kama sheria zinavyoelekeza. 

Aidha waliyaomba mashirika mbalimbali kushirikiana na shirika la AGAPE linalomjali, kumlinda, kumthamini na kumsaidia mtoto wa kike katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni mkoani Shinyanga. 

James Malima alisema serikali inatambua jitihada mbalimbali zinazofanywa na shirika la AGAPE katika kumkomboa mototo wa kike kielimu na kuahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanapata elimu. 

“Watoto wa kike wanapitia changamoto nyingi, kinachotakiwa wazazi na walezi pamoja na jamii kwa ujumla tushirikiane kuwalinda watoto wa kike na tuwapatie elimu, mtoto anapaswa kwenda shule siyo kuozeshwa au kuwapeleka kwenda kufanya kazi za ndani", alionya. PICHA ZA MAHAFALI- BOFYA HAPA

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages