Breaking News

Your Ad Spot

Nov 9, 2017

LABOUR PARTY CHA UINGEREZA CHAMPONGEZA RAIS DK. MAGUFULI KWA UTENDAJI WAKE

DAR ES SALAAM
Chama cha Labour cha nchini Uingereza kimepongeza juhudi za Rais Dk. John Magufuli na Serikali yake ya awamu ya tano kwa utendaji mzuri katika kulinda na kugawanya rasilimali za nchi kwa watu wake.

Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na Viongozi wa Labour Party katika Mkutano na vyama mbali mbali vya kisiasa vikiwemo vya Kiafrika vya CCM, SWAPO na ANC, uliofanyika Uingereza na kuhudhuriwa na Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga.

Akizungumza na mwandishi Jonas Kamaleki wa Idara ya Habari (MAELEZO) Lubinga amesema Chama cha Labour kinataka haki sawa kwa wote, kwa hiyo kitendo cha Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli kusimamia rasilimali na kuhakikisha rasilimali zetu zinazoibiwa zisiibiwe tena, kimewapa faraja.

Lubinga amesema Labour Party wanaamini kuwa hatua ya Serikali ya Awamu ya Tano kujikita katika kusimamia rasilimali za nchi kitaleta maandeleo kwa kuwa hakuna maendelo yanyoweza kupatikana bila usimamizi mzuri wa rasilimali.

“Chama cha Labour kinapigana kuhakikisha wananchi wake wanapata makazi bora, hivyo suala la Accacia ambao walikuwa wakifanya vitendo visivyoendana na hali  halisi ya rasilimali hasa kwetu sisi walengwa kimewafurahisha sana na kuona kuwa mazungumzo yamekamilika katika mazingira ya kukubaliana namna ya rasilimali hizo zinavyotumika kuwanufaisha Watanzania,”alisema Lubinga.

Kuhusu mwelekeo wa uchumi, Kanali Mstaafu Lubinga amesema kuwa uchumi wa Tanzania unakua na utakuwa wa kuvutia kwa kuwa ni juhudi za makusudi zinafanyika hivyo amewataka wanachi wawe na subira.

Ameongeza kuwa wazazi wawaandae watoto wao kufanyakazi na wasiwaachie tu kwenda wanavyotaka akitoa mfano kuwa mtu akiona mtoto wake amenunua gari la kifahari inabidi amuulize fedha ametoa wapi za kununua gari hilo wakati mshahara wake unajulikana na ni  mdogo.

Lubinga amewataka Watanzania wawe wavumilivu kwa kuwa mabadiliko huleta kiwewe kwa watu na yakishaleta matokeo chanya, watu hao husahau walioleta maendeleo hayo.

Serikali ya Awamu ya Tano imetimiza miaka miwili tangu iingie madarakani Novemba 5, 2015. Katika kipindi hiki watanzania wameshuhudia miradi mikubwa ya maendeleo ikianzishwa na kutekelezwa, mfano ujenzi wa barabara,madaraja, ununuzi wa ndege sita, ujenzi wa reli ya kisasa, (standard gauge), utengenezaji wa  madawati na elimu bure kwa elimu ya msingi na mwisho nidhamu ya kazi imerejea katika utumishi wa umma.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages