Breaking News

Your Ad Spot

Nov 12, 2017

MDAU: SOMO LA KILIMO LIRUDISHWE KUFUNDISHWA MSINGI HADI SEKONDARI



Tarehe 26, march, 1973 katika jimbo la Michagan nchini marekani ilisikika sauti ya mtoto mmoja ambaye alikuwa mgeni wa kwanza kwa Prof Carl Victor Page na Dokta Gloria Page. Huyu si mwingine bali ni Larry Page, mwanzilishi wa mtandao wa Google Larry alizaliwa katika familia ya wanasayansi. Baba yake Carl Victor Page alikuwa profesa wa kompyuta katika chuo cha Michigan State University toka mwaka 1965. Mama yake Gloria alikuwa daktari wa kompyuta na alikuwa akifundisha katika chuo cha Lyman Briggs College.

Maisha ambayo alikulia Larry Page yalikuwa maisha ya kupishana na komputa sebuleni, makaratasi yahusuyo kompyuta na hata akienda maktaba ya wazazi wake alikutana na kompyuta tu na vingine vihusivyo kompyuta. Hii ilimfanya Larry kulipenda somo la kompyuta.  alihitimu masomo ya kompyuta na kuanzisha mtandao wa Google mtandao ambao leo hii unatumiwa na watu zaidi ya million ... ,ii imemfanya Larry Page kupata mafanikio makubwa katika umri wa miaka 44 akiwa na dola 46.3 billion sawa na trillion 93 za kitanzania

Makuzi ya Larry  kwa wazazi na kile alichokwenda kusoma kuwadhihirisha uwiano wa mazingira ya nyumbani na elimu anayopata mtoto darasani mazingira ya maliasili zilizopo nyumba zimshawishi mtoto kielimu
Kilimo katika nchi nyingi za kiafrika hususan Afrika  Mashariki kimekuwa ndo njia pekee ya uchumi kwa ailimia kubwa ya wakazi wake. Watu wamekuwa wakijihusisha katika Nyanja mbalimbali za kilimo kama kilimo cha mazao ya chakula na biashara pamoja na ufugaji hivyo watoto wanakua wakiona jembe, ng’ombe, mashamba n.k

Katika nchi za afrika magharibi hususani Kenya Tanzania na Uganda kilimo ndio sekta kuu inayoingizia mataifa haya kipato. Bajeti ya mwaka 2016-2017 ya Tanzania inaanisha kwa 65.5% ya watanzania wengi wamejiajiri katika sekta ya kilmo na 100% ya chakula cha ndani kinatokana na kilimo mwaka wa fedha 2014-2015 na 2015 -2016 kilimo kilichangia 28.8% na 29.0%ya pato la ndani(GDP)

Nchini Kenya , 75% ya malighafi viwandani inatokana na kilimo na ufugaji, 60% ya wakenya wamejiajiri katika kilimo, 45% ya pato la taifa linatokana na kilimo. Uganda nako vilevile, 69% waganda  wanalima, 37% ya pato la taifa linatokana na kilimo
Hii inadhihilisha kuwa kilimo ni sehemu ya maisha ya watu wengi Afrika. Kijana anapotoka shule atakachokuta nyumbani ni mifugo (ng’ombe , mbuzi, kondoo, kuku n.k) mashamba dhana za kilimo kama majembe.

Nchini Tanzania 65.5% ya watanzania wanategemea kilimo kama uti wa mgongo kiuchumi ni idadi kubwa sana ya watu. Asilimia 65.5% ya wakazi million 50 wa Tanzania ni sawa na watu million 42.5 ndo wanategemea kilimo.

Tanzania ina vyuo zaidi ya 40 pamoja na vyuo shirikishi vinavyotoa elimu ya shahada lakini ni chuo kimoja tu kinachotoa shahada ya kilimo nacho ni Sokoine University of Agriculture  SUA (Morogoro) hii inadhihilisha kuwa katika sekta ya elimu ambayo ndo humjengea mtoto misingi  ya maisha na kumuandaa kuja kuyakabili mazingira yake, elimu ya kilimo haitiliwi maanani. Uduni wa elimu ya kilimo inayotolewa kwa vijana na wingi wa idadi ya wategemezi katika kilimo nchini  unatoa taswira ya jinsi jamii yetu inawekeza elimu kwa asilimia kubwa katika vitu ambavyo haviko katika mazingira halisia ya vijana wetu.

Chuo kama UDSM hakina kozi hata moja ya kilimo, chuo kikubwa Tanzania kinachojaza vijana wengi toka mikononi mwa wakulima  hii ni kuwatenga vijana wa kitanznania na mazingira amabayo wamekulia katika moja ya maandiko ya `mwasisi wa  taifa letu Mwalimu Julius K. Nyerere, alisema kuwa watoto wa watanzania wanatakiwa wapate elimu kulingana na kile kilichopo katika mazingira yao kama jamii ya wafugaji wapewe elimu kutoka elimu ya msingi hadi chuo juu ya ufugaji wa kuu, bata, sungura ng’ombe mbuzi n.k. elimu hii itatoa wataalam wa kuanzisha miradi ya kusindika nyama na kutoa nje bidhaa kama hizo. 

Mwalimu Nyerere alilenga kurahisisha mfumo wa viwanda kwa kuwaandaa vijana kielimu kuyakabili mazingira yao.

Leo hii kijana anaanza shule, ukimuuliza unataka kuwa nani atakwambia nesi,mwalimu, injinia, mwanasheria kupata mkulima utahoji shule nzima na kuambulia wawili.

Mwaka jana nilitembelea shule ya Imalilo wilayani Kwimba (Mwanza) nilikutana na wanafunzi wa shule hiyo kama 32, katika kuwahoji malengo yao 30 walitaja fani tofauti na kilimo, vijana wawili wakasema wakishindwa kufikia malengo watarudia kilimo cha wazazi wao.

Jamii itambue kuwa elimu kubwa huanzia nyumbani, mtoto anapofundishwa shuleni juu ya kilimo bora cha nyanya akirudi nyumbani na kumkuta mzazi wake analima nyanya kizamani atamwelekeza kile alichofundishwa shule ili kuboresha kilimo hicho. Elimu yetu imeangazia zaidi mazingira nje na uhalisia wa maisha ya vijana wetu hii ndio maana nchi inazalisha wasomi wanaotegemea ajira serikalini.

Kijana wa mwaka wa mwisho chuo kikuu au chuo chochote anaanza kuwekeza akili yake katika kutengeneza mitandao ya ajira. Ataanza kumpigia mjomba ambaye yuko halmashauri amjulishe kuwa amekaribia kumaliza chuo hivyo amwandalie mazingira ya ajira. Haya yote ni matokeo ya kumtenga kijana na mazingira yake halisia.

Jamii yetu na serikali yetu ikumbuke kuwa elimu nzuri ni ile ambayo inamwandaa kijana kukaniliana na ubovu wa mazingira aliyo nayo. Afundishwe elimu ya kilimo toka akiwa mdogo  ili atokee kukipenda na kuja kufanya mabadiliko akiwa mdogo ili atoke kukipenda na kuja kufanya mabadiliko katika jamii- Samaki Mkunje Angali Mbichi- tusisubiri kijana anamaliza chuo na miaka 30 ndo tumshauri awekeze katika kilimo atafanya kilimo kwa kujilazimisha na sio kupenda. Sekta ya kilimo haitapata mabadiliko daima.

Juhudi za serikali ya awamu ya tano kuwekeza katika viwanda iendane na elimu ya kilimo kwa vijana, kilimo bora cha matunda kitazalisha viwanda vya juice, kilimo bora cha pamba kitazalisha viwanda vya nguo, ufugaji wa kisasa utazalisha viwanda ya kusindika nyama vyote hivi vinahitaji elimu bora kwa vijana wetu

Kama mtanzania na mdau wa elimu na kilimo namuomba waziri wa kilimo chakula, mifugo na uvuvi  Dk Charles Tizeba pamoja na waziri wa elimu Mh. Joyce ndalichako kupitia upya mtaala wa elimu ya msingi  na sekondari ili kuweza kulirudisha somo la kilimo kwa wanafunzi katika shule zote za msingi na sekondari.

Pia serikali ya Raisi Magufuli ianzishe kozi ya kilimo katika  vyuo vyote ambavyo kuna kozi mchanganyiko kama UDSM, UDOM, SAUT, St John, St Joseph n.k

Somo la kilimo liendane na mashamba ya shule na vyuo ambayo yatawapa uzoefu vijana katika kilimo eneo la Tanzania ni kubwa, limejaliwa ardhi yenye rutuba na aina nyingi za mazao tukubali vijana wakue wakijua umuhimu wa kilimo


IMEANDIKWA NA

Gervas K. Yemba
gervasyemba@yahoo.com (0659142408)

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages