Breaking News

Your Ad Spot

Dec 28, 2017

MWENYEKITI WA CCM RAIS DK MAGUFULI AKUTANA NA KAMATI MAALUM ALIYOIUNDA HIVI KARIBUNI KUHAKIKI MALI ZA CHAMA

IKULU
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Desemba, 2017 amekutana kwa mara ya kwanza na Kamati maalum aliyoiunda kwa lengo la kuhakiki mali za chama, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo aliitangaza tarehe 20 Desemba, 2017 Mkoani Dodoma na Mwenyekiti wake anayeiongoza ni Dk. Bashir Ally. 

Katika Mazungumzo hayo Rais Magufuli (pichani), amewataka wajumbe wa kamati hiyo kufuatilia na kuhakiki mali zote za chama, kumhoji mtu yeyote ambaye atahitajika kutoa taarifa juu mali za chama na kubaini thamani ya mali, mahali zilipo, makusanyo ya mapato na wanaozishikilia ama kutumia mali hizo.

Rais Magufuli pia ametoa mwito kwa wanachama wa CCM na wananchi wengine kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zote zinazohusu mali za chama kwa kamati hiyo, na watakaoitwa kuhojiwa waitikie wito huo.

“Nataka mali za chama zikinufaishe chama, nataka mkamhoji mtu yeyote, awe kiongozi, awe mwanachama, awe mfanyabiashara, mtu yeyote. Mkazihakiki mali zote ili chama kipate haki yake” amesema  Rais Magufuli.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Dk. Bashiru Ally amesema kamati imeanza kazi rasmi na ametoa mwito kwa wanachama, wananchi na wote wanaozitumia mali za chama kutoa ushirikiano watakapoitwa kuhojiwa.

“Tumezungumza na Mwenyekiti kwa karibu saa mbili, katueleza matarajio yake, sababu za kuunda tume hii, kazi zake na faida zake kwa chama na kwa nchi, kwa hiyo ametukabidhi vitendea kazi na taarifa mbalimbali na ametueleza kazi yetu ni kuhakiki mali zote za chama kwa kushirikiana na wanachama na wale wanaoshirikiana na chama kuzitumia hizo mali kama vile wapangaji, wasimamizi, nakadhalika” amesema Dk. Bashiru Ally

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages