.

CCM, DIASPORA NA UTANDAWAZI

Mar 29, 2018

Na Kangoma Kapinga, Mwenyekiti-CCMUK
CCM ni taasisi kubwa ya siasa na uongozi barani Africa, miongoni mwa chache zilizotokea kwenye ngazi ya siasa za ukombozi hadi wakati  huu wa dunia ya utandawazi.Chama chetu kimehimili misukosuko na changamoto za uongozi za Africa na kuweza kuongoza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa amani. Na hatimayeTanzania imesimama wima duniani na inahesabika kama moja ya nchi yenye umoja wa kitaifa, amani na utu wa watu. Na sisi raia wake tumebeba umbile hilo popote tunapojitambulisha duniani. Hayo yote hayakuja kwa bahati nasibu bali yalibuniwa na kujengwa na viongozi wetu chini ya Chama cha TANU na hatimaye CCM.

Kazi ya kuijenga Tanzania yenye sifa nilizotaja hapo juu haikuwa rahisi kama wengi wanavyodhani, bali ilitokana na baadhi ya viongozi waliokiasisi chama chetu kuhakikisha kuwa wanaweka dira iliyohakikisha kila mtanzania popote alipo anapata haki za kijamii na kiuchumi. Hayo yalianishwa pia kwenye katiba ya chama cha TANU na kurithiwa na CCM, kuwa binadamu wote ni sawa na kila mmoja anastahili heshima.

Misingi hiyo madhubuti ndiyo iliyosaidia kujenga jamii yetu iliyo sawa na huru na hivyo kuleta urahisi wa kuwa na umoja wa kitaifa wenye kulinda haki ya kila mmoja ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali bila uonevu wala ubaguzi. Na hata tulipowasha mwenge na kuuweka juu ya mlima Kilimanjaro tulisisitiza yafuatayo, nanukuu: “Tunawasha mwenge na kuuweka juu ya mlima Kilimanjaro ili uangaze nje ya mipaka yetu na kuleta Upendo pale kwenye chuki, matumaini pale kwenye kukata tamaa na heshima pale kwenye udhalilishaji.” 

Makala yangu haina haja ya kurefusha mjadala wa safari ya maendeleo yetu kutoka uhuru hadi sasa, bali nakusudia kujenga hoja itakayodokeza changamoto mpya za kisiasa,kijamii na kiuchumi zinazoongezeka kwa kasi duniani kupitia UTANDAWAZI (Globalisation). Utandawazi ni tendo linaloondoa mipaka  ya kijamii na kiuchumi kutokana na kukua kwa teknolojia ya mawasiliano duniani hivyo kuleta maingiliano ya jamii kirahisi sana na kuondoa vikwazo baina ya nchi mbalimbali pia umejenga jamii pana inayoshabihiana kimaono (Homogeneous society) na hivyo kufanana katika kupata mahitaji mbali mbali. Utandawazi unaifanya jamii kuwa moja duniani kwa maana ya uhuru na kuona fursa za kiuchumi na kuzitafuta ziliko kokote kirahisi zaidi kuliko miaka 40 iliyopita wakati CCM inazaliwa. Lakini pia utandawazi haumuondolei mtu asili yake ya kuzaliwa. Mtanzania ataendelea kuwa hivyo hata kama utandawazi umehamishia baadhi ya maslahi yake kwenda nchi nyingine.

Watanzania wengi walifuata mkondo wa fursa zilizoletwa na utandawazi na kujikuta wapo kwenye nchi mbalimbali duniani. Hivyo walibadili jina lao na kujulikana kama Diaspora. Kwa bahati mbaya sana hilo halikupokelewa vema na sheria za nchi yetu na hivyo wengi wameachwa nyuma na kukosa haki zao za msingi ndani ya nchi yao ya asili ikiwapo Uhuru, heshima na haki mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa nilizoainisha kwenye umbile la utaifa wetu pale juu.

Wana diaspora wengi hawaruhusiwi kumiliki ardhi wala kurithi mali pia hawaruhusiwi kupiga kura kuchagua viongozi wao wa kitaifa hata kwa wale wanaostahili. Nchi nyingi zimeshamaliza tatizo hilo na wananchi wao wanashiriki kupiga kura popote walipo duniani na kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wa nchi zao.Na pia wameshirikishwa vema kwenye maeneo ya kiuchumi kama kuruhusiwa kumiliki ardhi. Mfano ni India au hata nchi majirani zetu wa Africa. Sisi kwetu imekuwa ni hadithi na ahadi zisizokuwa na mwisho huku watanzania wenzetu wa diaspora na vizazi vyao wakikosa haki zao za msingi bila mtetezi.

Kwanini Tanzania tumesita kutoa haki hizo? Hiyo ni kinyume na misingi na ahadi ya waasisi wetu waliotaka kujenga jamii ya Tanzania iliyo sawa na huru. Hizo kasoro zimeachwa kwa muda mrefu sana bila kutafutiwa ufumbuzi licha ya majadiliano katika majukwaa mbalimbali kati ya viongozi wetu wa kitaifa na wadau wengine tukiwamo viongozi wa jumuiya za diaspora ya Tanzania. Na zimewaacha njia panda Watanzania wa diaspora na wasielewe ni nani hasa mwenye wajibu wa kulinda haki zao wakati huu wa utandawazi? Na je kwanini serikali yao imeendelea kupiga danadana suala la haki za wana diaspora? Je wachukue hatua gani ili kupata haki zao za msingi?

Kwa sasa CCM kama mmiliki wa serikali inayotawala inabaki kuwa kimbilio pekee la wana diaspora ili kuidhibiti serikali na kuisukuma iweze kuchukua hatua za dharura ili kuwarudishia wana diaspora haki zao za msingi. Wana diaspora ni watanzania wanaochangia maendeleo ya nchi kijamii na kiuchumi na pia ni waelewa sana wa sera za CCM na wanathamini maamuzi mbali mbali yanayofanywa na serikali hasa hii awamu ya tano ya kujenga nidhamu ya kazi kwani hilo ni sehemu halisi ya maisha ya wanadiaspora, na pia wanaunga mkono kazi mbalimbali zinazofanyika kwenye maeneo mengi ya kimkakati pamoja na dhamira ya kuendeleza sekta ya viwanda nchini na wanaweza wakatumika sana kama daraja la stadi za kazi (best practices). CCM haina budi kubeba jukumu la kuwarejesha wana diaspora kwenye ramani halisi ya utashi wa nchi yetu, ili waendelee kupeperusha bendera ya Tanzania popote walipo kwa ari kubwa zaidi. CCM hatupaswi kupingana na utandawazi bali tujishirikishe nao kwa faida pana za kijamii na kichumi.  

Mwenyekiti wa chama chetu Jemedari Dr JP Magufuli  amejizolea sifa nzuri sana miongoni mwa wanadiaspora kwa kazi kubwa aliyoianza ya kukirejesha chama na serikali kwenye misingi yake halisi, Na wanaamini pia atatumia fursa adimu atakayopata kuliangalia hilo kwa faida pana ya diaspora yetu na umuhimu wake kwa kuwashirikisha katika mageuzi anayofanya, diaspora inaweza kutumika vizuri kama sehemu ya kuongeza mitaji kwenye miradi mikubwa kama ya umeme mfano wa wenzetu Ethiopia (Grand Ethiopian renaissance dam) na wanaamini kuwa sasa ni wakati muafaka wa kurudisha haki za wana diaspora bila kigugumizi cha kuingiza siasa au hisia kali zenye chembechembe zinazoweza kuleta chuki kwa chama chetu na serikali kwa ujumla.
Kidumu chama cha mapinduzi
Kangoma Kapinga
Mwenyekiti-CCMUK.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª