.

RAIS MAGUFULI AIPA MAELEKEZO TFF, MBT, VYAMA VYA MICHEZO

May 19, 2018

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz               

Faksi: 255-22-2113425


OFISI YA RAIS,
     IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,   
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Vilabu na vyama mbalimbali vya michezo kuweka mikakati itakayoinua kiwango cha michezo na kuiwezesha Tanzania kushiriki na kushinda michuano ya kimataifa.

Wito huo umetolewa leo tarehe 19 Mei, 2018 katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam ambapo Mhe. Rais Magufuli amekabidhiwa kombe la mabingwa wa michuano ya soka ya nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa vijana wa umri wa chini ya miaka 17 ambapo timu ya Tanzania (Serengeti Boys) iliibuka mabingwa huko nchini Burundi, ameipokea timu ya soka ya watoto wa kike waishio katika mazingira magumu (Tanzania Street Children – TSC) ambayo imeibuka washindi wa pili katika michuano ya dunia iliyofanyika nchini Urusi na amekabidhi kombe la ubingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa timu ya Simba Sport Club ya Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amesema Watanzania wanataka kupata furaha kwa kuona timu zao zinashinda na kwamba wamechoka kuona timu zao za Taifa na vilabu vinavyowakilisha katika michuano ya kimataifa vinafanya vibaya.
Ameahidi kuwa Serikali itashirikiana na wadau wote wa michezo kukuza michezo na ametaka katika michuano ya Soka ya Afrika (AFCON) kwa vijana wa umri wa chini ya miaka 17 itakayofanyika mwezi Aprili 2019 ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji, Tanzania ioneshe mfano kwa kuhakikisha ubingwa unabaki hapa nchini.
“Michezo ni furaha, michezo ni afya, lakini pia michezo ni biashara, umefika wakati sasa tukuze michezo yetu, na Serikali ipo tayari kuunga mkono juhudi za kuendeleza michezo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kabla ya kuzungumza na wanamichezo Mhe. Rais Magufuli na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri Mhe. Juliana Shonza na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda wameshuhudia pambano la ligi kuu ya soka Tanzania bara ambapo mabingwa wa ligi hiyo Simba wamefungwa bao 1- 0 na timu ya Kagera Sugar ya Kagera.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Mei, 2018 

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช