BEKI wa timu ya taifa, Taifa Stars, Kelvin Yondan (kushoto) akijiandaa kumkabili mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Cost, Didier Drogbar, timu hizo zilipochuana leo usiku katika mechi ya kirafiki ya kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Stars ilifungwa 1-0.
FULL STORY
STARS leo ilikomaa hadi kufa kiume licha ya kufungwa bao 1-0, katika kipute cha kishikaji cha kimataifa dhidi ya kina Drogbar na comvoy lote la timu ya Ivory Coast, katika dimba la Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.Katika mchezo huo, Stars ilionyesha kandanda safi na kuwashangaza maelfu ya mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo kushuhudia mchezo huo, na kuwafanya kutoamini timu hiyo kama ina uwezo wa kucheza soka la kisasa.
Mashabiki walifurika kwenye uwanja huo zaidi wakitaka kuwaona wachezaji wa kimataifa wa Ivory Coast, na hasa Didier Drogba, anayecheza soka ya kulipwa katika timu ya Chelsea ya England, pamoja na mchezaji mwenzake Solomon Kalou.
Mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua katika dakika zote 90, ulianza kwa kasi huku ikiichukua dakika nne Ivory Coast iliyosheheni wachezaji wake wanaocheza soka Ulaya, kufanya shambulizi langoni mwa Stars, kabla ya kipa Muharami Mohamed kuokoa hatari hiyo langoni mwake.
Dakika mbili baadae, Stars ilijibu shambulizi hilo kupitia kwa Jerry Tegete, aliyewatoka mabeki wa Ivory Coast, kabla ya kuachia shuti kali lililotoka nje.
Stars iliendelea kufanya mashambulizi ya hapa na pale huku ikishangiliwa na mashabiki wake akiwemo Rais Jakaya Kikwete, kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa wa kusakata soka, na dakika ya saba nusura Stars ifunge bao baada ya Mrisho Ngasa kupiga krosi safi, lakini Tegete alichelewa kuunganisha na mpira huo kuokolewa.
Timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu huku Stars ikifanya mashambulizi kutafuta mabao, lakini uimara wa mabeki wa Ivory Coast uliikosesha mabao.
Ivory Coast baada ya kuona Stars ikiisumbua ngome yake, ilijipanga na kufanya mashambulizi huku mchezaji nyota wake, Drogba, akitafuta nafasi za kufunga lakini mabeki wa Stars walisimama imara kumzuia na kumfanya kuishia kulalamika kwa mwamuzi.
Laiti kama Stars ingetumia vyema nafasi iliyopata dakika za 14, 22 na 23 kupitia kwa Tegete na Ngasa, ingeweza kuwapa Watanzania zawadi ya mwaka mpya, lakini mipira iliyopigwa na wachezaji hao ilitoka nje.
Drogba naye alijitahidi kufurukuta kutafuta mabao, na dakika ya 24 nusura aipatie timu yake bao baada ya kupiga mpira wa faulo uliodakwa na Muharami.
Dakika ya 38 mchezaji huyo wa kimataifa, ndipo alipoipachikia timu yake bao kwa kichwa, baada ya kuwakimbiza mabeki wa Stars kisha kumuhadaa Muharami kabla ya kujipinga na kupiga mpira kwa kichwa uliojaa moja kwa moja wavuni.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Stars kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0, na kipindi cha pili kilipoanza Ivory Coast ilifanya mabadiliko ya wachezaji wake 10, na kumbakiza kipa pekee. Kutokana na hali hiyo, Ivory Coast ilianza mchezo kwa kasi hali iliyowafanya wachezaji wa Stars kupoteana, kabla ya kujipanga tena kuwakabili wapinzani wao.
Hata hivyo, hali hiyo iliyodumu kwa dakika 20 iliisha baada ya wachezaji wa Stars kujituma vilivyo kwa kutowaruhusu wapinzani wao kupenya na kuifanya timu hiyo kupoteza mwelekeo.
Stars nayo ilipopata nafasi iliwaendesha mchakamchaka wapinzani wao na kufanya mashabiki kuishangilia, huku wachezaji wa Ivory Coast wakishindwa kuamini timu waliyocheza nayo.
Bahati ilikuwa mbaya kwa Stars katika mchezo huo kwani dakika ya 73 Tegete alipata nafasi ya kufunga kwa kubaki na kipa, lakini aliachia shuti kali lililogonga mwamba kabla ya kurudi uwanjani na kuokolewa na Ivory Coast.
Stars nayo ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Juma Jabu, Henry Joseph, Jerry Tegete, Nizar Khalfan na Kigi Makasi, na nafasi zao waliingia Stephano Mwasika, Nurdin Bakari, John Boko, Abdi Kassim na Mussa Hassan 'Mgosi'.
Katika mchezo huo Stars iliwachezesha Muharami Mohamed, Shadrack Nsajigwa, Juma Jabu/Stephano Mwasika, Kevin Yondan, Nadir Haroub 'Canavaro', Henry Joseph/Nurdin Bakari, Abdulhalim Humud, Mrisho Ngasa, Jerry Tegete/John Boko, Nizar Khalfan/Abdi Kassim na Kigi Makasi/Mussa Hassan 'Mgosi'.
CIAO.