MWENYEKITI wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, anaanza leo ziara ya siku tatu mkoani Dar es Salaam, kukagua shughuli za maendeleo na uhai wa Chama.
Akiwa katika ziara hiyo, Rais Kikwete atapata fursa ya kuzungumza na viongozi wa mashina wa CCM katika wilaya zote tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke.
Pia atakutana na wahanga wa makombora yaliyolipuka katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Mbagala Kizuiani. Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Kilumbe Ng’enda, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa, ziara hiyo inakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 33 ya kuzaliwa kwa CCM.
Alisema Rais Kikwete pia ataongoza maandamano siku ya kilele cha sherehe hizo Februari 6, mwaka huu. Maandamano hayo yataanzia Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam na kupita barabara ya Morogoro, Bibi Titi, Lumumba na kuingia viwanja vya Mnazi mmoja.
Katika ziara hiyo, Rais Kikwete leo ataanza kwa kutembelea Wilaya ya Kinondoni, ambapo atafungua Jengo la Ofisi ya CCM wilaya na baadaye kuzungumza na mabalozi wa nyumba kumi katika ukumbi wa Vijana Social. Keshokutwa Rais Kikwete atatembelea Kata ya Sandali, ambako pia atafungua tawi la CCM la DUCE na baadaye kuelekea Mbangala kuwaona waathirika wa milipuko ya mabomu.
Pia atazungumza na viongozi wa mashina katika Uwanja wa Sabasaba, ambapo siku ya mwisho atahitimisha ziara wilayani Ilala, ambako atafanya mazungumzo na viongozi wa mashina. Ng’enda alimewaomba wananchi na wapenzi wa CCM kujitokeza kwa wingi katika ziara hiyo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269